Wakorea 37 waanza kutengeneza filamu mlima Kilimanjaro

Wasanii mashuhuri kutoka nchini  Korea Kusini wakipanda mlima Kilimanjaro kwa ajili ya kurekodi tamthilia  zitakarushwa katika Tv Mbalimbali nchini  humo, picha na Fina Lyimo

Muktasari:

  • Watalii 37 kutoka Korea ya Kusini wameanza safari ya kupanda mlima Kilimanjaro kwa lengo la kutengeneza filamu (TV show) itakayoonyesha maisha katika mlima huo.

Moshi. Watalii 37 kutoka Korea ya Kusini wameanza safari ya kupanda mlima Kilimanjaro kwa lengo la kutengeneza filamu (TV show) itakayoonyesha maisha katika mlima huo.

Filamu hiyo itakayotengenezwa ndani ya siku sita za kupanda mlima Kilimanjaro kupitia lango la Marangu imelenga kutanganza mlima huo kupitia kipindi cha televisheni nchini humo cha kituo cha TV N, na kupewa jina la “Once in a life time climb Kilimanjaro’’.

Wakizungumza leo Jumapili Septemba 25, 2022, mmoja wa waigizaji kutoka Korea ya Kusini, Son Hojun amesema amekuwa akisikia  taarifa nyingi kuhusu mlima Kilimanjaro ya kwamba ni mgumu hivyo anayo shauku ya kupanda aone uhalisia wa mlima huo kwa kutengeneza historia ya kutengeneza filamu.

"Nimepata fursa ya kushiriki kipindi cha televisheni kwa kwenda kuigiza kwa kupanda mlima   mashuhuri duniani, hii ni fursa na ni jambo la kujivunia na pia kuutangaza mlima huu nchini Korea Kusini"

Kiongozi wa wasanii hao ambaye ni mwigizaji na mwana mziki, Hyo Jung amesema anayoshauku ya kufika kileleni na kufanya kipindi cha TV kuwa na mvuto zaidi, hali itakayovutia watazamaji wengi.

Mkurugenzi wa kampuni ya utalii ya Jay Adventures, inayopandisha watalii hao, Jay Kim amesema kampuni hiyo imekuwa ikileta watalii wengi kutoka Korea Kusini kupanda mlima kilimanjaro na kwamba itaendelea na jitihada za kuutangaza utalii wa mlima Kilimanjaro katika nchi hiyo.

Ofisa Mkuu wa uhifadhi kitengo cha utalii, Charlse Ngendo amesema kundi hilo maalumu limekuja kutengeza filamu katika mlima huo ambayo itarushwa nchini Korea ya kusini na kutangaza vivutio vyote vilivyopo nchini.

Amesema Korea ya Kusini ni nchi muhimu katika utalii kwa kuwa uchumi wake umeimarika na watu wake sasa wanasafiri nchi mbalimbali duniani na kwamba hii ni fursa ya kuutangaza mlima Kilimanjaro.

"Tunaamini filamu hii itatangaza mlima Kilimanjaro na kutangaza nchi yetu na kufanya Wakorea wengi kuja kupanda mlima pamoja kutembelea vivutio vingine, ujio wao ni fursa kwa  soko la utalii katika nchi yetu huko Korea ya Kusini" amesema Ngendo

Watalii hao watatumia siku sita kupanda mlima huo, huku wakichukua picha za matukio mbalimbali watakayofanya katika mlima huo, kwa ajili ya kutengeneza filamu, ambayo itaenda kuonyeshwa katika TV mbalimbali nchini humo, hatua ambayo itavutia watalii wengi kupanda mlima Kilimanjaro kutoka Korea kunsini.