Waliotikisa dunia kwa 'Jerusalema', sasa waitikisa kwa mzozo wa malipo

Tuesday July 13 2021
mastakgpic
By Mwandishi Wetu

Johannesburg, Afrika Kusini. Mwimbaji Nomcebo Zikode na mtayarishaji muziki, Master KG ambao waliikamata dunia na kibao chao kikali cha "Jerusalema" sasa wanatikisa dunia kwa jambo jingine; mzozo wa malipo kutokana na kazi hiyo.

Wimbo wa "Jerusalema" ambao ulitayarishwa na Master KG na kuimbwa na Zikode, ulitikisa dunia kwa msaada wa kundi la Fenómenos do Semba la nchini Angola ambalo lilitengeneza video ya dansi likionyesha miondoko ya Kwaito huku madansa hao wakiwa wameshika sahani za chakula mikononi.

Kutokana na watu wa sehemu mbalimbali duniani kuzuiwa kufanya matembezi kutokana na ugonjwa wa virusi vya corona wakati huo, video ya changamoto ya kucheza dansi ya wimbo huo (#JerusalemaDanceChallenge) iliyotolewa na kundi hilo ilifanya watu mbalimbali duniani waigize miondoko hiyo na kutuma video zao mitandaoni, hali iliyoongeza wimbo huo kusambaa kwa kasi.

Lakini wawili hao sasa wameingia kwenye mgogoro ambao utaifanya dunia ianze tena kuwafuatilia.

Kwa mujibu wa gazeti la Star la Afrika Kusini, wawili hao wameingia katika mgogoro wa malipo ya mrabaha kutokana na mapato ya wimbo huo ambao ulitazamwa na zaidi ya watu milioni 300 katika mtandao wa YouTube

Gazeti hilo limeandika kuwa habari za kuwepo kwa mgogoro huo ziliwekwa hadharani na Zikode, ambaye ni mwimbaji na mwandishi wa wimbo huo baada ya kutuma ujumbe katika akaunti yake ya mtandao wa kijamii Jumapili.

Advertisement

Nyota huyo aliyeimba kibao cha "Xola Moya Wam" alichomshirikisha Master KG, alisema anawashukuru mashabiki wote ambao walitimiza ndoto yake kwa kuufanya wimbo huo utambe dunia.

“Sauti yangu na mashairi yamekwenda dunia nzima, lakini bado nasubiri nachostahili. Sijalipwa hata senti moja na lebo (iliyorekodi wimbi) kwa ajili ya 'Jerusalema' licha ya wimbo kupata mafanikio duniani," ameandika Zikode."Nimekejeliwa, huku kukiwa na jitihada za kuufanya mchango wangu uonekane mdogo.

“Mapenzi na msaada naoendelea kupata kutoka kwa mashabiki wa 'Jerusalema' ndio umekuwa nguvu yangu katika wakati mgumu.

“Mimi, kama msanii wa kike, siwezi kukaa kimya zaidi. Suala hili sasa liko kwa wanasheria wangu.”

Master KG, ambaye jina lake halisi ni Kgaogelo Moagi, alijibu ujumbe huo kwa kutumia akaunti yake ya Twitter, akisema makubaliano waliyofikia na Zikode ni kugawana mrabaha sawasawa. Alisema Zikode alitaka asilimia 70 za mrabaha, na yeye apate salio la asilimia 30 ya hisa.

“Mwaka jana, Nomcebo alianza ziara ya 'Jerusalema' peke yake na sikuwa na tatizo naye na wiki chache nyuma nilianza ziara yangu na baadaye Nomcebo alienda kwenye vyombo vya habari na kutengeneza habari kuwa namuacha ... Sijui hasa ni kwa nini mambo yawe hivi,” aliandika katika Twitter.

Master KG alisema wakati utakapofika, ukweli utajulikana.

“Hakuna kitu cha kuficha hapa. Nimechoka kuchukiwa kwa sababu ya uongo,” alisema Master KG.

Tovuti ya Star pia imeandika kuwa taarifa iliyotolewa na mtendaji wa kampuni ya Mic Productions, Lionel Jamela inasema maneno ya Zikode hayawezi kuachwa yapite bila ya kusahihishwa.

“Tunaweza kuthibitisha kuwa wakati wa kutengeneza huo wimbo, Master KG (muhusika mkuu) na Nomcebo Zikode (msanii aliyeshirikishwa) walikubaliana kugawana nusu kwa nusu ya malipo ambayo Master KG angepata. Makubaliano ya msanii aliyeshirikishwa ambayo yanaonyesha mgao sawa baina ya wasanii hao wawili, yaliandaliwa Novemba mwaka jana kwa ajili ya pande zote mbili kusaini,” alisema.

Mtendaji huyo aliongeza kuwa Zikode, kwa kutumia wanasheria wake, waliupitia mkataba na wakataka mgao mkubwa zaidi.

“Tangu wakati huo, kumekuwa na kwenda mbele na kurudi nyuma. Mawasiliano ya mwisho na timu ya sheria ya Nomcebo kuhusu majadiliano ya mkataba yalikuwa Juni mwaka jana."

Jamela alisema hakuna malipo yaliyofanywa kwa msanii yeyote kati ya wawili hao kwa kuwa Zikode alikuwa bado hajasaini makubaliano ya msanii mshirikishwa ambayo "kimsingi yanaonyesha kilichokubaliwa kati yake na Master KG kabla ya wote kuingia studio kurekodi Jerusalema”.

Advertisement