Wasanii kukusanya mirabaha kuanzia mwakani

Dar es Salaam. Kuanzia mwakani mirabaha itakusanywa na wasanii wenyewe na ofisi ya Haki Miliki Tanzania (Cosota) itabaki kama msimamizi.

Hayo yamesemwa leo Ijumaa Julai 21,2021 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Sanaa ,Utamaduni na Michezo, Said Yakoub katika tukio la ugawaji mirabaha linalofanyika hoteli ya Hayatt Regency jijini Dar es Salaam.

Amesema wasanii hao watakusanya mirabaha yao kupitia kampuni waliyoiunda inayoitwa Tanzania Music Right Society (Tarmiso).

Baadhi ya wasanii waliotajwa kuwepo katika kampuni hiyo yenye watu 30 ni pamoja na Nandy, P.Funk, Fid Q, Aslay, Babu Tale, Abby Chams, Sarafina na Profesa Jay.

Pia wapo Chama cha Muziki wa Dansi (Chamudata), chama cha muziki wa taarabu na waandaji mbalimbali wa muziki.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Cosota, Doreen Sinare, amesema watakuwa wakiwafuatilia utendaji wao wa kazi na pale watakapoenda ndivyo sivyo hawatasita kuwaondoa bila kujali ukubwa wa majina yao.

Katika tukio hilo, kampuni hiyo ilikabidhiwa leseni rasmi ya kuanza kufanya kazi hiyo.