Wasanii wakacha kuhudhuria jukwaa la Basata

Thursday April 29 2021
bastapic
By Nasra Abdallah

Dar es Salaam. Licha ya Naibu Waziri Habari, Utamaduni , Sanaa na Michezo, Pauline  Gakul kuhoji wasanii kutohudhuria makongamano yanayoandaliwa na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) na kutaka hatua kuchukuliwa, mahudhurio ya wasanii yameendelea kuzorota.

Leo Alhamisi Aprili 29, 2021 Mwananchi DIgital limeshuhudia wasanii wasiozidi 30 waliohudhuria jukwaa la maadili katika sanaa na wengi wakiwa ni wachoraji wa taasisi ya Nafasi Art Space.

Kaimu katibu mtendaji wa Basata,  Matiko Mniko amesema huenda wasanii wengine wamebanwa na kazi na baadhi hawapendi kuonekana hadharani mara kwa mara kwa maelezo kuwa wanalinda sanaa yao.

"Ni kweli kumekuwa na ushiriki mdogo wa wasanii katika majukwaa kama haya kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo hizo nilizozitaja," amesema.

Licha ya uchache wao, amesema watatumia jukwaa hilo kuwafuata wasanii katika maeneo waliyopo nchi nzima na kubainisha kuwa jukwaa hilo huandaliwa mara moja kwa mwezi kutoa fursa kwa wasanii, wadau na jamii kujadili mambo mbalimbali na kutoa mapendekezo namna bora ya kuendesha sanaa.

Naye mwanamuziki mkongwe nchini, John Kitime amesema mmomonyoko wa maadili umechangia kwa kiasi kikubwa kuondolewa kwa maofisa utamaduni waliokuwa wakifanya kazi nzuri ya kufuatilia wasanii.

Advertisement
Advertisement