Wasanii wamlilia Bi Sonia

Thursday July 21 2022
bibi soni
By Nasra Abdallah

Dar es Salaam. Wasanii mbalimbali wamemlilia msanii mwenzao Bi Sonia ambaye amefariki leo Julai 21, 2022 asubuhi akiwa visiwani Zanzibar.
Taarifa za kifo chake zilithibitishwa leo Alhamisi Julai 21,2022 na Mwenyekiti wa Chama cha Waigizaji Tanzania, Chiki Mchoma.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wasanii akiwemo Blandina Chagula maarufu kwa jina la Johari,amesema akiwa kama mzalishaji filamu wamempoteza jembe.


Akifafanua zaidi Johari amesema Bi Sonia alikuwa msanii  mwepesi  kumeza script licha ya umri wake mkubwa.


'"Bi Sonia mbali ya kuwa mwigizaji mwenzetu lakini ni bonge la cast kiukweli tumepoteza jembe kwenye tasnia kwani alikuwa mrahisi kumeza kila script uliyompatia,"


"Sema ndiyo hivyo kazi ya Mola haina makosa tunamuombea apumzike salama "amesema Johari ambaye aliwahi kuigiza naye kama mama yake katika igizo la Tufani wakiwa naye Kaole.


Wakati Vicent Kigosi maarufu Ray, amesema mama huyo ni kati ya wamama wachache waliokuwa wanaiwakilisha vema filamu ,kwani anakumbuka wakati wanatoka katika kuigiza kwenye vikundi na kuhamia kwenye filamu waliondoka naye wakiwa na marehemu Steven Kanumba.

Advertisement


Kwa upande wake Suzan Lewis 'Natasha ' anasema Bi Sonia alikuweza kuwaungunisha wanawake wa tasnia ambao watu wazima na  kuanzisha kikundi cha malezi.


Akiwa Mwenyekiti wao, Natasha amesema walitembelea shule mbalimbali kutoa elimu ya maadili kwa wanafunzi ikiwemo wenye ndoto za kuwa waigizaji.


"Hata wakati akiwa Zanzibar tulikuwa tuna kazi fulani ilikuwa tuje tufanye na aliniahidi kwamba angerejea Dar es Salaam Julai hii lakini ndio hivyo ndoto hizo zimekatikia njiani, inaumiza sana," amesema Natasha.


Mtayarishaji wa tamthiliya ya Jua Kali, Leah Mwendamseke'Lamata' amesema amefanya kazi na Bi Sonia zaidi ya 20 ikiwemo tamthiliya ya Kapuni .


Lamata amemuelezea msanii Bi Sonia kuwa  ni msanii aliyependa kazi yake na alikuwa mama mlezi na mshauri kwake ambaye kwa namna moja au nyingine amechangia yeye kufika hapo leo.


"Kutokana na ukaribu wangu na yeye hata katika kuugua kwake nashukuru niliweza kushirikiana na familia kumuuguza hadi mauti ulipomkuta," amesema Lamata.


Mwigizaji Shamsa Ford kupitia ukurasa wake wa Instagram ameandika; "uliigiza kama mama yangu kwenye movie ya zawadi ya Birthday. Kipaji chako kikubwa cha kuigiza, utakumbukwa Daima," amesema Shamsa.

Advertisement