Washindi Miss Tanzania wakabidhiwa zawadi

Thursday June 02 2022
miss tanzaniapic
By Mwandishi Wetu

Dar es Salam. Waandaji wa shindano la Miss Tanzania kampuni ya ‘The Look’ kwa kushirikiana na wadhamini wa shindano hilo Startimes, Benki ya CRDB, na kampuni za bima za Sanlam na Strategis, wamekabidhi zawadi kwa walimbwende walioingia katika tano bora katika kinyang’anyiro cha Miss Tanzania 2022 ambapo mlimbwende Halima Kopwe kutoka Mtwara aliibuka kidedea, Mashindano hayo yalifikia kilele mnamo Tarehe 20 Mwezi Mei 2022.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi zawadi iliyofanyika Makao Makuu ya Benki ya CRDB yaliyopo barabara ya Ali Hassan Mwinyi Jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa kamati ya Miss Tanzania,  Azama Mashango alisema zawadi hizo ni sehemu ya ahadi ambazo zilitolewa kwa washiriki wa shindano hilo, huku akiwashukuru wadhamini wote waliojitokeza kufanikisha Miss Tanzania 2022.

“Leo hapa tunakabidhi zawadi kwa walimbwende walioingia katika tano bora kama ambavyo taratibu za mashindano zinavyojieleza. Zawadi zitakazokabidhiwa ni pamoja na bima ya maisha yenye jumla ya thamani ya Sh50 milioni kwa muda wa miaka mitano kutoka kampuni ya Sanlam life, bima ya gari kwa mshindi wa kwanza kwa ajili ya kukinga na majanga yatokananyo na ajali, kutoka sanlam general, bima ya safari kwa safari zote za mashindano ya nje kwa mwaka mzima kutoka kampuni ya strategies , na zawadi za fedha taslimu,” alibainisha Azama.

Akikabidhi zawadi ya bima ya gari kwa mshindi wa kwanza wa Miss Tanzania 2022, Mkuu wa Kitengo cha Bima Benki ya CRDB, Moreen Majaliwa alisema zawadi hiyo itamsaidia kumkinga mshindi huyo ambaye alipewa zawadi ya gari aina ya benz katika majanga yanayosababishwa na ajali.

 “Thamani ya gari aliyopewa mrembo wetu Halima ni Sh30 milioni, ni gari ya thamani kubwa, hivyo inapaswa kuwekewa ulinzi wa kibima ili aweze kufurahia matunda ya shindano hili. Benki yetu kupitia kitengo cha bima tumesema tutamsaidia kufanikisha hili kwa kumkatia bima ya mwaka mzima ili kumkinga na majanga,” alisema Moreen.

Moureen alisema kuwa kwa kutambua mchango wa mashindano hayo katika kuwainua vijana wakike na kulitangaza Taifa, Benki hiyo kwa kushirikiana na washirika wake wa kampuni za bima za Sanlam na Strategis pia wametoa bima ya maisha zenye jumla ya Sh50 milioni, pamoja na bima ya safari ya mwaka kwa walimbwende ambao watashiriki mashindano ya kimataifa.

Advertisement

 “Shindano la Miss Tanzania limekuwa daraja la mafanikio kwa vijana wengi wa kike wenye sifa za urembo. Lakini pia limesaidia kubadilisha mtazamo wa jamii juu ya kujishughulisha na maswala ya urembo. Sasa hivi wengi wetu tunatazama Sanaa ya Urembo kama ajira kwasababu ya mafanikio ambayo yanatokana na shindano hili dunia kote,” aliongezea Moureen.

Pamoja na zawadi hizo, Benki ya CRDB pia iliwafungulia washindi hao akaunti na kuwawezesha kupokea zawadi zao za fedha ambapo mshindi wa kwanza alikabidhiwa kiasi cha Sh10 milioni,  mshindi wa pili Sh5 milioni, mshindi wa tatu Sh3 milioni, mshindi wa nne Sh1 milioni, na mshindi wa tano Sh1 milioni. Benki hiyo pia iliahidi kutoa elimu ya fedha bure ilikuwasaidia kufikia malengo yao ya kifedha.

Akizungumza kwa niaba ya walimbwende hao baada ya kukabidhiwa zawadi mshindi wa taji la Miss Tanzania 2022, Halima Kopwe alitoa shukrani za dhati kwa waandaaji wa shindano hilo, pamoja na wadhamini kwa zawadi hizo.

“Zawadi hizi zinaonyesha ni kwa namna gani mashindano ya urembo yameanza kupewa heshima na wadau mbalimbali. Hii itasaidia kuwavutia wasichana wengi ambao wana ndoto ya kushiriki na kukuza ajira katika eneo la urembo,” alisema.

Advertisement