Wateule 65 kuchuana tuzo za wauzaji, watoa huduma za harusi

Monday April 12 2021
harusi pic
By Nasra Abdallah

Jumla ya wateule 65 watashiriki kuchuana katika tuzo za wauzaji wa vifaa vya harusi na watoa huduma zitakazotolewa Mei 16, 2021 jijini Dar es Salaam.

Katika tuzo hizo ambazo ni zao la maonyesho ya harusi yaliyokuwa yakifanyika kwa miaka nane mfululizo, jumla ya vipengele 20 vitawaniwa.

Akizungumza na waandishi wa habari Benedict Msofe, kutoka kampuni ya 361 Degrees ambao ndio waratibu wa tuzo hizo, alisema hii ni mara ya kwanza kutolewa kwa tuzo hizo ambazo zimelenga kutambua mchango wa pekee wa  wauzaji na watoa huduma za shehere hizo.

“Tumeamua kuandaa na kuratibu tuzo hizi za harusi ili kuwatambua vinara wa huduma kwenye sekta hii na kwa kufanya hivyo tunaamini kwamba tutaongeza thamani kwa wauzaji na watoa huduma na harusi.

 “Ukiachilia mbali faida kwa watoa huduma, itakuwa ni msaada mkubwa kwa maharusi wa siku usoni kwa kuwa watakuwa na orodha ya wauzaji na watoa huduma za sherehe hiyowaliothibitishwa ili wawe na urahisi wa kujua ni wapi hasa watapata mahitaji yao kwa ajili ya siku zao hizo muhimu,”amesema Msofe.

Alivitaja baadhi ya vipengele vitakavyoshindaniwa kuwa ni pamoja na wapamba ukumbi, mpiga picha bora, mpishi bora wa chakula,mpaka keki bora,mshehereshaji bora, mvalishaji bora,mtoa huduma za usafiri, mkodishaji ukumbi, mpambaji maharusi na mpiga video bora.

Advertisement

Akielezea namna walivyowapata wateule, Meneja Msaidizi wa mradi huo, Keflen Bunani, alisema mapendekezo yalitoka kwa umma wa watanzania na yalikua kwa vipengele tofauti, na baada ya mapendekezo hayo walithibitisha ushiriki kwenye vipengele husika.

Hata hivyo Bunani alisema orodha kamili ya washiriki pamoja na vipengele itatolewa hivi karibuni kupitia ukurasa wao kwenye mtandao wa kijamii na mara moja zoezi la upigaji kura litaanza kupitia tovuti yao ambapo kampuni ya Innovex Tanzania itahusika katika usimamizi wa upigaji kura.

Akizungumza kwa niaba ya washirika wakaguzi kampuni ya Innovex Tanzania, Upendo Fatukubonye alisema, wanayo furaha kuwa sehemu ya jukwaa hilo na kuahidi kuwa shughuli ya upigaji kura utakuwa huru na haki.

Tuzo za harusi ni jukwaa linalotazamia kukuza biashara ya harusi pamoja na ubora wa bidhaa na huduma zitolewazo kwenye maharusi na ni tukio linalotarajiwa kuleta pamoja wauzaji na watoa huduma mbalimbali za harusi pamoja na wadau kutoka katika sekta hiyo kote Tanzania.

Wakati meneja wa Hoteli ya Serena Dar Es Salaam, Seraphin Lusala, amesea wanayo furaha kuwa wenyeji wa tuzo hizo kwa kuwa huduma za harusi ni moja kati huduma zitolewazo kwenye hoteli zao kote nchini.

Advertisement