Zari aomba watoto wa kike wasaidiwe taulo

Wednesday June 02 2021
zari pc
By Nasra Abdallah

Mjasiriamali Zarina Hassan ’Zari’ ameiomba jamii iwasaidie watoto wa kike wapate taulo za kujisitiri wakati wanapokuwa kwenye hedhi.

Zari ametoa rai hiyo leo Jamatano Juni 2,2021 alipokuwa kwenye hafla ya kugawa taulo hizo kwa shule za sekondari na msingi za mkoa wa Dar es Salaam.

Katika hafla hiyo mgeni rasmi alikuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Omar Kumbilamoto

Zari ambaye pia ni mzazi mwenzake na msanii wa Bongofleva nchini Tanzania, Naseeb Abdul ‘Diamond Platnumz’, amesema si lazima kwa mtu atoe taulo nyingi bali anaweza kutoa hata mbili kulingana na uwezo wake.

Amesema ni vema jamii ikajenga utamaduni wa kuona jukumu hilo ni lao badala ya kuwaachia wachache.

"Kutoa ni moyo si utajiri, tujenge utamaduni wa kutoa hata kama ni kidogo kwakuwa kufanya hivyo tunakuwa tumemsaidia mtoto wa kike kutimiza ndoto zake” amesema

Advertisement

Zari amesema ni lazima jamii ikatae utaratibu wa mtoto wa kike kukosa masomo kwasababu ya kutokuwa na taulo ya kumsitiri wakati wa hedhi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa kampuni ya Keds, Victor Zhang , walioandaa hafla hiyo, amesema misaada hiyo ni sehemu ya kurudisha kile wanachokipata kwa jamii.

Zhang amesema ni katika utaratibu huo ndani ya miaka mitatu kuanzia mwaka 2019 hadi mwaka huu wametoa taulo zenye thamani ya Sh45 milioni na kuahidi kufanya hivyo ili kutatua matatizo yaliyopo katika jamii.

Awali akiwawakilisha walimu wakuu wa shule, Mkuu wa shule ya Zanaki,  Julieth Matowo, amesema watoto wanapokosa masomo kwa kutokuwa na taulo za kujisitiri hurudi nyuma kimaendeleo darasani na pia hupata msongo wa mawazo.

“Pamoja na kwamba shule zina utaratibu wa kugawa taulo hizo lakini kutokana na kuwepo kwa idadi kubwa ya wanafunzi haziwatoshelezi huku wanaopata shida hiyo wengi ni wanaotoka mazingira magumu,”amesema Julieth.

Naye mmoja wa wanafunzi waliopata taulo hizo, Sitti Athuman, ameishukuru kampuni hiyo kwa msaada wao na kuomba utaratibu huo uendelee  kwa nchi nzima.

Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Ustawi wa jamii, Dk  Joyce Nyoni, amesema bado kuna changamoto nyingi katika kukabiliana na masuala ya hedhi salama.

Amezitaja changamoto hizo ni uelewa mdogo kwa jamii, wasichana kushindwa kumudu gharama za  taulo hizo, upatikanaji wa maji safi  na maji salama na ubora wa vyoo ana umuhimu wa elimu ya hedhi salama.

Advertisement