Chama avunja ukimya, aapa kuanza na moto

Muktasari:

  • KIUNGO fundi wa Simba, Clatous Chama amevunja ukimya baada ya kushindwa kucheza mechi iliyopita dhidi ya Mbeya City akitaja mambo mawili yaliyokwamisha na kuahidi kuwasha moto akipewa nafasi ya makocha wake.

KIUNGO fundi wa Simba, Clatous Chama amevunja ukimya baada ya kushindwa kucheza mechi iliyopita dhidi ya Mbeya City akitaja mambo mawili yaliyokwamisha na kuahidi kuwasha moto akipewa nafasi ya makocha wake.

Chama aliyerejeshwa Msimbazi kutoka RS Berkane ya Morocco, alisema kuchelewa kukamilika kwa vibali vyake ambavyo hatimaye vilipatikana saa 8 mchana, saa chache kabla ya mechi hiyo ya Mbeya kuanza ndicho kilichomkwamisha kwani kikosi kilishpelekwa kwa wahusika.

Jambo jingine ni kushi-ndwa kupata muda wa kutosha kufanya mazoezi ya pamoja na wenzake ikiwemo kocha Pablo Franco kupata muda wa kumuangalia hali yake ya utimamu wa kimwili.

Habari njema kutoka kwa Chama ni kwamba fundi huyo sasa yupo vizuri kiutimamu wa mwili na anamatani kupata nafasi ya kucheza ili kutoa mchango wake katika kikosi cha Simba.

Chama alisema anafahamu kuna wengi wanahamu ya kumuona anacheza katika kikosi hicho, jambo ambalo hata kwa upande wake lipo hivyo kwani anataka kwenda kuipigania timu.

Alisema suala la kucheza lipo kwa benchi la ufundi ila kama ikitokea akapewa nafasi hiyo atahakikisha anajitoa kadri ambavyo anaweza ili kufanikisha malengo ya timu msimu ya kupata ubingwa.

“Muda ukifika nikicheza kwa mara ya kwanza tangu kurejea kwangu naamini nitakuwa na mwanzo mzuri wa kutimiza malengo niliyonayo pamoja na yale ya timu,” alisema Chama na kuongeza;

“Jambo jema zaidi tusiangalie yale yaliyofanyika nyuma bali nipo na mwanzo mpya ambao natamani kufanya mengi mazuri zaidi ya niliyofanya hapo awali.”

Katika hatua nyingine kwenye mazoezi ya Simba tangu kurejea kutoka Mbeya, Chama ni miongoni mwa wachezaji waliofanya vizuri kwenye aina tofauti za programu walizotoa makocha wa Simba.

Awali, Chama alianza mazoezi yake binafsi ya nguvu akifanya pembeni akiwa amevaa raba, huku kocha wa viungo, Daniel De Castro akimsimamia kutengeneza utimamu wa mwili wake.

Baada ya hapo Chama alijiunga katika mazoezi ya pamoja na wenzake huku kwenye yale ya kucheza alionyesha uwezo wake mkubwa wa kupiga pasi za mwisho, kufunga mabao pamoja na kumiliki mpira.

Huenda kiungo huyo akawepo kwenye kikosi cha Simba kitakachovaana na Mtibwa Sugar kwenye mechi ya Ligi Kuu iliyopangwa kupigwa Uwanja wa Manungu, leo.