Dabo alia na mastaa Azam

Muktasari:

  • Azam ambayo inacheza kesho haijawa na matokeo mazuri tofauti na ilivyoanza msimu, kwani kati ya michezo minne ya hivi karibuni, imeambulia sare tatu na kushinda mchezo mmoja ikibaki nafasi ya pili kwa pointi 37 baada ya michezo 17.

Saddam Sadick, Mbeya. Kocha wa Azam, Yousuph Dabo amekiri wachezaji wake hawafanyi vizuri kwenye michezo ya hivi karibuni akiwataka kubadilika, huku akiwatupia kijembe mashabiki wanaozipa nafasi Yanga na Simba kwenye mbio za ubingwa.

Azam ambayo inacheza kesho haijawa na matokeo mazuri tofauti na ilivyoanza msimu, kwani kati ya michezo minne ya hivi karibuni, imeambulia sare tatu na kushinda mchezo mmoja ikibaki nafasi ya pili kwa pointi 37 baada ya michezo 17.

Katika michezo hiyo ya Ligi Kuu, imepata sare ya 1-1 dhidi ya Simba, ikashinda 2-1 kwa Geita Gold, suluhu ya bila kufungana mbele ya Tabora United na 1-1 dhidi ya Tanzania Prisons.

Katika mechi hizo matajiri hao wameruhusu mabao ya kufungwa matatu, wakifunga manne idadi ambayo ni ndogo kulinganisha na ubora na uwezo wa kikosi hicho ndani na nje ya uwanja.

Dabo alisema matokeo hayo yametokea kwa kuwa wachezaji hawajaonyesha kiwango na sasa wanakwenda kujipanga tena kurekebisha makosa eneo la ushambuliaji na beki.

Kuhusu vita ya ubingwa msimu huu, kocha huyo alisema wanaozipa nafasi timu za Yanga na Simba wasubiri muda kwani ndio raundi ya pili imeanza na lolote linaweza kutokea.

“Ni kweli kiwango hakijawa bora wachezaji wanakosa umakini kushindwa kutumia nafasi kufunga lakini wanaruhusu mabao tunakwenda kulifanyia kazi ili mchezo ujao na Singida FG kesho tufanye vizuri.

“Kuna ambao wameshaamua pakupeleka ubingwa, hawajui bado ligi haijaisha na ndio kwanza raundi ya pili imeanza, Azam hatujajitoa kwenye mbio hizo na tunaamini tutapambana,” alisema kocha huyo raia wa Senegal.

Alikiri ushindani kuwa mkali akieleza kuwa mzunguko wa pili kila timu inajipanga kuwania pointi tatu.