Dejan avaa mabomu Simba

Dejan avaa mabomu Simba

Muktasari:

  • Mshambuaji mpya wa Simba, Dejan Georgijevic (28) raia wa Serbia amefunguka machungu yake baada ya timu yake kupoteza Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga na ameahidi makubwa klabuni hapo.

BAADA ya maneno kuwa mengi mtaani kuhusu ujio wake Msimbazi na kiwango alichokionyesha kwenye mechi mbili alizocheza akiwa ndani ya uzi wa Simba, Dejan Georgijevic amefunguka kupitia ukurasa wake wa Instagram huku akitoa ahadi nzito kwa Wanamsimbazi.

Straika huyo ni kama amewajibu wale wanaombeza kwa kuandika ujumbe uliojawa na hisia kali za kuapania kufanya makubwa ili kuwadhihiirishia kuwa kwanini yupo hapa nchini kusakata kandanda.

"Licha ya kwamba nimekuwa sehemu ya Familia ya Simba kwa siku chache tu, nashiriki uchungu na mfadhaiko wa kupoteza mechi yetu dhidi ya wapinzani wetu wa kudumu. Ninajihesabu kama mshindi wa kuzaliwa kwa njia sawa na mtu wa nchi yangu, Novak Djokovic" anaendelea na kuandika kuwa;

"Kwa heshima niliyo nayo kwa mamilioni ya wasaidizi wa Simba, nitateseka, nitajitahidi, nitajitolea na kufanya lolote liwezekanalo ili kutoa huduma bora kwa timu yangu, kufunga mabao na kuwafurahisha mashabiki, kujivunia na kuwa upande wa ushindi kila wakati" ameandika Dejan kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Dejan alijuinga rasmi na Simba Agosti 7 akitokea Nk Domzale ya nchini Slovenia huku akipewa jezi na Saba mgogoni.