Dirisha dogo moto utawaka Ligi Kuu

Zimebaki siku 26 kabla ya dirisha dogo la usajili kufunguliwa Desemba 16 huku presha ya matokeo ikizidi kupanda kwa kila timu kati ya 16 zinazoshiriki Ligi Kuu Bara.

Sajili zilizofanyika katika dirisha kubwa lililopita zimelipa kwa baadhi ya timu huku nyingine zikizua maswali kutokana na kushindwa kufikia malengo tarajiwa.

Raundi tisa za mechi zimeshapigwa na timu takribani zote, ukiacha Simba na Mashujaa ambazo zitakutana zenyewe.

Mwananchi linakuletea mahitaji kwa timu zote 16 za Ligi Kuu kulingana na mechi zilizocheza na udhaifu ulioonekana hadi sasa.


YANGA

Licha ya Yanga kuwa na rekodi nzuri kwenye ligi ikiongoza kuwa timu iliyovuna pointi nyingi, imefunga mabao mengi na kuruhusu nyavu zao kutikiswa mara chache zaidi bado ina shida kwenye safu ya ushambuliaji.

Yanga msimu huu imefunga mabao 26 kati ya hayo 18 yamefungwa na viungo huku washambuliaji wakiwa na idadi ndogo zaidi ya kupachika mabao ambapo kati ya hayo wao wamefunga mabao manne.

Kocha wa timu hiyo, Miguel Gamondi amesema katika kikosi chake hapendelei kuwa na mchezaji mmoja ambaye atategemewa peke yake kuibeba timu, anachotaka ni kuona kila mmoja uwanjani anaibeba Yanga. Hata hivyo,  amesema anahitaji mshambuliaji wa kuongeza nguvu.


SIMBA

Simba dirisha kubwa la usajili ilisajili wachezaji 11 ambao kati ya hao ni wachezaji wawili tu ambao wameonyesha ubora na kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara huku wengine kati yao wakikosa kabisa nafasi ya kucheza na mmoja kuvunjiwa mkataba mapema zaidi.

Usajili wa timu hiyo ulikuwa ni Ayoub Lakred, Willy Onana, Che Fondoh Malone, David Kameta, Aubin Kramo, Fabrice Ngoma, Shaban Chilunda, Abdallah Hamis, Luis Miquissone, Hussein Abel na Hussein Kazi. Kipa Luis Jefferson kutoka Brazil alivunjiwa mkataba baada ya kupata majeraha kwenye mechi za kirafiki kambini Uturuki kabla ya msimu haujaanza na hakuwahi hata kuja nchini.

Katika usajili huo, wachezaji ambao wamefanya vizuri na kuingia moja kwa moja katika kikosi cha kwanza ni Che Malone na Ngoma huku wengine wakianzia benchini na wengine kama Hamis, Kameta na Kazi hawajapata nafasi ya kucheza kabisa hivyo watakuwa na jukumu kubwa la kuhakikisha wanafanya usajili wa maana ambao utawasaidia kuipambania timu kufikia malengo.

Licha ya kuwa na uhitaji wa kusajili bado watahitaji kuhakikisha wanawaondoa wachezaji ambao hawana uhitaji nao kama eneo la kipa hakuna umuhimu wa kujaza makipa wengi wakati wanaotumika zaidi wanafahamika.


AZAM FC

Licha ya kusajili wachezaji wengi wenye majina makubwa na wenye uzoefu bado timu yao haijawa katika uora uliotarajiwa.

Dirisha dogo likiwa linaenda kufunguliwa Januari wana haja ya kuongeza mshambuliaji, beki namba mbili na beki wa kati kwaajili ya kusaidiana na Daniel Amoah baada ya usajili wa Malickou Ndoye kushindwa kuwa na manufaa na kumlazimisha kocha kuwatumia wachezaji wengine tofauti kama Edward Charles.

Kwenye eneo la ushambuliaji Idris Mbombo ameshindwa kuendana na kasi ndani ya misimu yote miwili aliyocheza hivyo benchi lina kazi ya kufanya kuongeza nguvu eneo hilo.


DODOMA JIJI

Kwasasa ipo chini ya kocha msaidizi Kassim Lyogope baada ya kocha mkuu kutokomea kusikojulikana bila taarifa. Time imekuwa bora msimu huu tofauti na msimu uliopita lakini pia inahitaji maboresho dirisha dogo kutokana na matokeo yao.

Dodoma Jiji ipo nafasi ya nne kwenye msimamo baada ya kukusanya pointi 15 kwenye mechi kumi ilizocheza, imefunga mabao 10 ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara tisa. Huu sio wastani mzuri maeneo yote mawili hivyo watahitaji maboresho.


KMC

Tangu ameichukua kocha  Abdihamid Moalin imekuwa bora sasa ipo nafasi ya tano kwenye msimamo kwenye mechi tisa walizocheza wamefungwa mabao 11 huku wao wakifunga mabao tisa.

Amekiri kuwa na safu mbovu ya ulinzi huku akiwakingia kifua baadhi ya wachezaji wanaocheza eneo hilo kuwa majeraha yamechangia wao kuruhusu mabao mengi akisema endapo watarudi kwenye hali zao za kawaida timu yake itapunguza makosa japo atakuwa na ulazima wa kuongeza nguvu dirisha dogo.


JKT TANZANIA

Ni msimu wake wa kwanza tangu imepata daraja msimu uliopita ikiwa na rekodi nzuri. Makali yake yameendelea baada ya kuonyesha ushindani kwa timu kongwe kama Mtibwa Sugar na Geita Gold ambao wanaburuza mkia huku wao licha ya ugeni wao wapo nafasi ya sita.

JKT pamoja na kujaza wazoefu wengi kwenye kikosi chao eneo la ushambuliaji limekosa mtu sahihi kwani kwenye mechi kumi wamefunga mabao manane tu huku ukuta wao pia ukiruhusu mabao 11 hivyo ni kazi kwa Malale Hamsin ambaye ndiye kocha mkuu kufanyia kazi udhaifu huo.

Eneo la kiungo la timu hiyo linaundwa na wakongwe Said Ndemla na Hassan Dillunga ambaye amepata majeraha linaonekana kuwa imara, lakini ukuta na washambuliaji kuna shida.


SINGIDA BIG STARS

Licha ya kujaza majina makubwa kwenye kikosi chao bado wanapambana kujiweka kwenye ushindani kwani maeneo yote wamekamilika lakini hawaonyeshi ubora ule uliokuwa unatarajiwa na wengi.

Singida Big Stars kwenye mechi tisa walizocheza wamefunga mabao 11 na kuruhusu nyavu zao zitikiswe mara 11 ni wastani mbaya kwao kwani ni wazi kuwa kila mchezo wanaruhusu bao na wao pia wanafunga.


KAGERA SUGAR

Tangu kuumia kwa Anuary Jabir wamekuwa wakipitia wakati mgumu eneo la ushambuliaji ambalo kwenye mechi tisa wamefunga mabao saba na kocha wa timu hiyo Mecky Maxime amekiri kuwa na uhitaji wa mchezaji mwingine eneo hilo.

“Siridhishwi na mwenendo mbovu wa matokeo wanayoyapata na naangushwa sana na eneo la umaliziaji japo ukuta pia una makosa, nitafanya maboresho dirisha dogo ili kujihakikishia nafasi ya kubaki na kuwa na timu shindani,” anasema.TABORA UNITED

Inanolewa na Mserbia Goran Kopunovic ambaye licha ya kuwa nafasi ya tisa kwenye msimamo amesema sio matarajio yake na anapambana ili aweze kupanda nafasi ya juu kidogo na baadaye kuongeza nguvu.

Goran ambaye kikosi chake kimefunga mabao matano kwenye mechi kumi walizocheza wakiruhusu nyavu zao kutikiswa mara saba amesema dirisha dogo ataongeza nguvu eneo la kiungo mkabaji, kiungo mshambuliaji, beki na mshambuliaji.


NAMUNGO

Baada ya kuachana na kocha wao mkuu Cedrick Kaze kutokana na matokeo mabaya, sasa timu ipo chini ya Denis Kitambi kwa lengo la kusukuma jahazi baada ya timu hiyo kukusanya pointi nane kwenye mechi tisa walizocheza wakifunga mabao manane na kufungwa tisa.

Kitambi anasema bado wana nafasi ya kufanya vizuri hadi kufikia dirisha dogo ni mapema sana kwake kuweka wazi mahitaji anayotakiwa kuboresha kwani bado anaona nafasi ya kufanya vizuri zaidi kwenye mechi zilizobaki kabla ya dirisha kufunguliwa.

Kwa utafiti uliofanywa na gazeti hili kwenye mechi hizo licha ya kuwa na mkongwe Ralient Lusajo eneo la ushambuliaji watahitaji kuboresha nafasi hiyo na kuimarisha ukuta wao.


MASHUJAA

Mashujaa ni msimu wao wa kwanza kwenye ligi msimu huu wameonyesha ushindani kwenye mechi nane wakiwa na kiporo cha mchezo mmoja dhidi ya Simba safu yao ya ushambuliaji imeonekana kuwa butu imefunga mabao matano tu.

Pamoja na hayo kocha mkuu wa timu hiyo Abdallah Mohamed ‘Baresi’ ambaye analia na safu yake ya ushambuliaji pia ameweka wazi kuwa na ukuta wake haupo imara kwani una wastani wa kuruhusu bao kila mchezo.


IHEFU FC

Inahitaji maboresho maeneo yote kuanzia ulinzi hadi ushambuliaji ni msimu wake wa pili kwenye ligi tangu imepanda lakini bado haina makali hadi sasa kwenye mechi tisa ilizocheza imefunga mabao saba na kuruhusu nyavu zao kutikiswa mara 12.

Ihefu FC yenye rekodi ya kuifunga Yanga tangu imepanda daraja ikiwa kwenye uwanja wake wa nyumbani inanoilewa na Moses Basena ambaye amerithi mikoba ya Zuber Katwila ambaye ametimkia Mtibwa Sugar.


COASTAL UNION

Ni muda sahihi kwa kocha David Ouma kuwa kocha mkuu akichukua nafasi ya Mwinyi Zahera kuwasoma wachezaji aliowakuta na kuandaa ripoti yake nafasi ambazo atataka kuongeza nguvu ili kuinusuru timu hiyo kushuka daraja.

Coastal Union kwa mujibu wa msimamo wa Ligi Kuu inaonyesha mechi tisa ilizocheza imefunga mabao manne tu ikiwa ndio timu iliyo na mabao machache zaidi ya zote Ligi Kuu kufikia sasa na imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara nane.

Mabao manne ni idadi ndogo sana kwa timu ambayo inahitaji kubaki Ligi Kuu au kuonyesha ushindani.


TANZANIA PRISONS

Ni timu ya pili kuruhusu mabao mengi zaidi Ligi Kuu hadi sasa imefungwa mabao 15 na imefunga mabao tisa tu katika mechi tisa hadi sasa hivyo timu hiyo itahitaji usajili maeneo yote mawili ili kuongeza nguvu kwenye eneo la kushambulia na kujilinda.

Timu hiyo inayonolewa na Freddy Felix ‘Minziro’ amekiri kuwa ana shida katika maeneo yote hivyo ripoti yake itazingatia nafasi zote kuanzia kiungo, beki na washambuliaji kwani mechi zao zote hata wakishinda lazima waruhusu bao hivyo ukuta wao haupo imara.


GEITA GOLD

Ipo chini ya kocha Hemed Morocco ambaye amerudi Ligi Kuu baada ya kutimkia visiwani Zanzibar ambako ameondoka akiiacha timu ya KMKM ikiwa imetwaa taji la ligi. Amerudi na mguu mbaya Geita Gold ambayo ipo kwenye nafasi ya pili kutoka mkiani ikikusanya pointi saba.

Timu hiyo ina shida kwenye safu yake ya ushambuliaji kwenye mechi tisa ilizocheza imefunga mabao matano tu huku ikiruhusu mabao 11 hivyo kocha kwenye ripoti yake anahitaji usajili maeneo yote.


MTIBWA SUGAR

Ndio timu inayoongoza kwa ukuta wao kuruhusu mabao mengi ya kufungwa (16) hivyo ni wazi kuwa benchi la ufundi litakuwa linakuna kichwa namna ya kubadili upepo.

Mtibwa mbali na kuruhusu mabao mengi huku pia ikishika mkia katika msimamo, habari njema kwao ni safu yao ya ushambuliaji ambayo imefunga mabao 10 na kuwa na wastani wa kufunga bao katika kila mechi, ikiwa imezidiwa na timu tatu tu za Yanga (26), Azam (19) na Simba (18) katika orodha ya kufunga mabao mengi zaidi kwenye ligi msimu huu. Imeshinda mchezo mmoja tu hadi sasa ikitoka sare mbili na kufungwa mechi sita na ina pointi tano kwenye mechi tisa.