Doumbia atoa msimamo Yanga

Muktasari:

  • Doumbia aliyesajiliwa dirisha dogo akiwa kwenye michuano ya Fainali za CHAN za Vijana akimchomoa Gael Bigirimana, ameshindwa kupenya kikosini mbele ya mabeki wa kati wa timu hiyo akiwamo nahodha Bakar Mwamnyeto, Dickson Job na Ibrahim Abdallah ‘Bacca’ aliyeingia kwenye mfumo wa Kocha Nasreddine Nabi na kuonyesha kiwango kikubwa.

Dar es Salaam. Beki wa kati wa kimataifa kutoka Mali, Mamadou Doumbia hajaonekana uwanjani kwa muda mrefu akiwa na jezi ya timu hiyo kwenye mechi za mashindano, lakini mwenyewe amemua kuvunja ukimya na kueleza hali anayokutana nayo Jangwani tofauti na matarajio yake na kuweka msimamo.

Doumbia aliyesajiliwa dirisha dogo akiwa kwenye michuano ya Fainali za CHAN za Vijana akimchomoa Gael Bigirimana, ameshindwa kupenya kikosini mbele ya mabeki wa kati wa timu hiyo akiwamo nahodha Bakar Mwamnyeto, Dickson Job na Ibrahim Abdallah ‘Bacca’ aliyeingia kwenye mfumo wa Kocha Nasreddine Nabi na kuonyesha kiwango kikubwa.

Beki huyo aliyesajiliwa kutoka klabu ya Stade Malien ya Mali tangu atue Yanga amecheza dakika 45 katika mechi ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) dhidi ya Rhino Rangers, mchezo uliopigwa Januari 29 na watetezi hao wa taji hilo wakishinda mabao 7-0 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Akizungumza na Mwananchi, Doumbia alifunguka; “Wakati mwingine soka ni katili sana, nimecheza michuano mikubwa na yenye ushindani wa juu, lakini nimekuja huku sichezi, hilo haliwezi kuondoa kwenye malengo na maisha yangu ya soka. Najua katika soka changamoto ni kawaida, ila inahitaji moyo wa ujasiri na kutokata tamaa kwani kila jambo lina wakati, ninachojua mimi ni beki mzuri ukifika wakati wangu nitacheza na watu wananiona.”

Licha ya kutocheza beki huyo aliyesaini mkataba wa miaka miwili, alisema; “Katika maisha haiwezekani kila siku mambo yakakwendea vizuri, kuna wakati unapitia changamoto ambazo zitakujenga na kuinuka kufanya vitu kwa ubora wa juu, nakiamini kipaji changu.”

Doumbia aliingia dirisha dogo sambamba na kiungo Mudathir Yahya na mshambuliaji Kennedy Musonda ambao wamepata namba.

“Najiuliza na inanifanya nishangae maana mchezaji unapochukuliwa dirisha dogo ni kwa ajili ya kucheza na kuongeza nguvu,” alisema. Nabi aliwahi kusema; “Bado hajaingia kwenye mfumo wangu, apambane.”