Duh! baada ya Fei Toto sasa Mayele, Bangala

YANGA inaendelea kupambana kumrejesha kundini kiungo wao fundi Feisal Salum 'Fei Toto' lakini wakati hali haijapoa kuna tishio jipya tena limeshuka klabuni hapo mastaa wao wakubwa wawili nao wakitakiwa na klabu nyingine.
Taarifa kutoka ndani ya Yanga ni kwamba mabosi wa juu wa klabu hiyo juzi walinasa taarifa nzito wakipata uhakika kwamba mshambuliaji wao Fiston Mayele anapigiwa hesabu kali za kutakiwa na klabu bingwa mtetezi wa Kombe la Shirikisho Afrika RS Berkane.
Berkane, inataka straika huyo hatari anayejua kufunga na akili yao imetua kwa Mayele ambaye amekuwa na uwezo wa juu sana msimu huu, walianza kuwashawishi watu wao wa karibu ili avunje au kununua mkataba wake wampe pesa ndefu ambayo ataishangaa.
Inaelezwa Mayele ametengewa kiasi cha Dola 550,000 kama atakubaliana kuvunja mkataba wake na Yanga ili atue haraka nchini Morocco.
"Kuna mawakala walifanya kazi na Mayele huko nyuma hao ndio wamepewa kazi ya kumshawishi atutingishe ili avunje mkataba na Yanga na kama atashindwa basi aununue," alisema mmoja wa mabosi wa juu kabisa wa Yanga.
Mbali na Mayele Mkongomani mwenzake naye Yannick Bangala, ambaye naye aliongeza mkataba kama mshambuliaji huyo hivi karibuni, naye kuna taarifa za uhakika kuwa tajiri mmoja wa Simba anamsumbua akitaka kumhamishia upande wa pili.
Yanga inafahamu kuwa Bangala ameulizwa maswali kuhusu mkataba wake na kumuuliza kama ameshapewa fedha zote au hajapewa kabisa ili wampenyezee ofa ya kufuru kuja kuungana na Henock Enonga.
"Hapa ndani pia Simba nao wametuma salamu zao kwa Bangala wanamtaka tunajua kila kitu ambacho wanakifanya tunawasubiri tuone mwisho wao.
Hata hivyo, mabosi wa Yanga wanaendelea kupambana kuhakikisha mastaa hao wanasalia akiwemo pia beki mzawa Dickson Job ambaye mkataba wake unaelekea mwisho.
Yanga tayari imeshakaa na Job kuhakikisha anasalia na Mwanaspoti linafahamu huenda wiki hii wakafunga biashara hiyo kwa kumsainisha dili nono.