Durant afunga pointi 31 Nets ikiizamisha Timberwolves NBA

Muktasari:

  • Kevin Durant jana JUmanne alifunga pointi 31 wakati Brooklyn Nets ilipozinduka kutoka katika kipigo ilichopewa na Los Angeles Lakers na kuibuka na ushindi dhidi ya Minnesota Timberwolves katika mechi ya Ligi ya Taifa ya Mpira wa Kikapu Marekani (NBA).

Minneapolis, Marekani. Kevin Durant jana Jumanne alifunga pointi 31 wakati Brooklyn Nets ilipozinduka kutoka katika kipigo ilichopewa na Los Angeles Lakers na kuibuka na ushindi dhidi ya Minnesota Timberwolves katika mechi ya Ligi ya Taifa ya Mpira wa Kikapu Marekani (NBA).


Durant aliongoza kwa ufungaji wakati Nets iliposhinda kwa pointi 127-97 katika mechi hiyo iliyocheleweshwa kwa saa 24 kutokana na maandamano yaliyosababishwa na kuuawa kwa risasi kwa kijana mweusi mwenye miaka 20, Daunte Wright akiwa katika taa za barabarani Jumapili.


Durant, akicheza mechi ya pili tangu arejee uwanjani baada ya kupona majeraha yaliyomfanya akae nje kwa miezi miwili, hakupoteza muda kuonyesha makali yake, akifunga pointi nane katika dakika tano za mwanzo.


Timberwolves, ambayo ina rekodi mbaya NBA baada ya kushinda mechi 14 tu lakini ikapoteza 41, haikuonekana kutoa ushindani na wakati fulani iliachwa kwa tofauti ya pointi 45 katika robo ya nne.


Kwa upande wa Nets, Durant alisaidiwa na mlinzi Joe Harris, ambaye alimaliza mchezo akiwa amefunga pointi 23, na Landry Shamet, ambaye aliongeza pointi 19 akitokea benchi. DeAndre Jordan pia alifunga pointi 13 kuchangia ushindi huo.


Anthony Edwards, ambaye alikuwa chaguo la kwanza la Wolves katika usajili wa wachezaji chipukizi, aliwaongoza wenyeji kwa kufunga pointi 27.


Baada ya mchezo huo, Durant alisema timu yake ya Nets ilijua kuwepo kwa hali ya wasiwasi zinazotokana na ubaguzi wa rangi Minneapolis.


"Nadhani (wachezaji) wanajua dhahiri kinachoendelea nchini, tuna mazungumzo kuhusu hili kila wakati," alisema Durant. "Lakini tunapokanyaga uwanjani, tunajua kazi yetu ni nini."


MVP huyo wa zamani alisema Nets wamefurahia kuepuka safari ambayo isingekuwa na faida.


"Nimefurahia NBA ilihakikisha mechi inachezwa na hatukuja bure, tulimalizia," alisema Durant.


Katika mchezo uliofanyika Charlotte, Kyle Kuzma alifunga pointi 24 na kuiwezesha Los Angeles Lakers kushinda kwa pointi 101-93 dhidi ya Hornets.


Wakati Kuzma aliongoza wafungaji upande wa Lakers, zilikuwa ni pointi 13 za Alex Caruso aliyetokea benchi ambazo ziliifanya mechi hiyo iipe ushindi Lakers.


Caruso alifunga 3-pointer na kuifanya Lakers iongoze kwa pointi 95-91 zikiwa zimesalia sekunde 45 na baadaye akafunga pointi nyingine mbili kwa mipira ya adhabu na kuiwezesha kushinda kwa tofauti ya pointi sita.