EPL ya kibabe zaidi wikiendi hii
Muktasari:
- Ikiwa itapoteza mchezo huo, mbali na kuzidi kuondoka katika ramani ya ubingwa kidogo kidogo, benchi la ufundi pia litazidi kushambuliwa kwa maneno na mashabiki ambao wameshaanza kusema kocha Erik Ten Hag aondoke
LONDON, ENGLAND. Kasi ya Ligi Kuu England inarejea tena wikiendi hii na kuna baadhi ya timu zina kazi kubwa ya kufanya baada ya kuanza vibaya huku nyingine zikiandamwa na majeruhi.
Hadi sasa ikiwa imepita mizunguko mitatu ukiingia wa nne, bado mambo hayajachanganya ingawa kuna timu dalili zimeanza kuonekana zitakuwa na wakati mgumu kwenye mikikimikiki ya kuwania ubingwa na kuna ambazo zimeonyesha zitakuwa na ushindani kwenye kinyang'anyiro hicho.
Baada ya kuchezwa kwa raundi hizo tatu, hapa tunakuletea mambo mbalimbali yanayozihusu timu kubwa sita kwenye ligi hiyo maarufu zaidi duniani kwenye raundi ya nne itakayoanza Jumamosi mapema saa 8:30 mchana na Man United itakipiga dhidi ya Southampton ugenini kwenye Dimba la St. Mary's.
MAJERAHA
Kwanza mtihani unaonekana kwa washika mitutu kutoka London, Arsenal ambao katika mapumziko ya wiki ya kimataifa walipata pigo baada ya kiungo wao tegemeo, Martin Odegaard kupatwa na majeraha yatakayomfanya kuwa nje kwa wiki tatu.
Odegaard ambaye amekuwa mchezaji tegemeo kwa zaidi ya misimu miwili kukosekana kwake katika eneo la kiungo inaweza kuiathiri kwa kiasi kikubwa timu hiyo ambayo kwa sasa inaweza kumtumia Kai Havertz kama mbadala wake.
Ukiondoa majeraha ya Martin, Arsenal pia inawakosa viungo wengine tegemeo katika eneo hilo kama Mikel Merino (majeruhi) na Declan Rice (kadi nyekundu).
Pia hawatokuwa na mabeki Takehiro Tomiyasu na Kieran Tierney ambao pia wanaumwa.
Hadi sasa taarifa za uhakika kwa upande wa Liverpool ni Harvey Elliott hatokuwepo.
ARTETA ASIZINGUE
Arsenal pia ina kazi kwa sababu mchezo wao wa wikiendi hii watacheza na Tottenham na inaelezwa itakuwa ni mechi ya lazima kwao kupata pointi tatu muhimu ili kuendelea kujiweka katika mizani sawa na wakubwa wengine kwenye mbio za ubingwa.
Wababe hawa ambao wapo nafasi ya nne kwa pointi zao saba baada ya mechi hiyo ya London Derby, itakuwa na kibarua cha kucheza na bingwa mtetezi Manchester City.
Ikiwa itafanya vibaya katika mechi hizo mbili itakuwa imeangusha karibua pointi sita zinazoweza kuiondoa katika nafasi nne za juu hali inayoweza kuwapa wakati mgumu kwenye kurudi.
TEN HAG KUJIULIZA
Mashetani wekundu kutoka mapango ya kale ni moja kati ya timu zinazohitaji sana kushinda wikiendi hii. Man United ambayo ipo nafasi ya 14, baada ya kucheza mechi tatu, ikishinda moja na kufungwa mbili za mwisho, wikiendi ijayo itakuwa na nafasi ya kujiuliza kwa kushinda ili kupunguza maneno na presha kubwa kutoka kwa mashabiki.
Katika mechi mbili zilizopita Man United imepoteza zote, hivyo inahitaji kuutumia mchezo wao ujao dhidi ya Southampton kama sehemu ya kurudi tena kwenye mstari.
Ikiwa itapoteza mchezo huo, mbali na kuzidi kuondoka katika ramani ya ubingwa kidogo kidogo, benchi la ufundi pia litazidi kushambuliwa kwa maneno na mashabiki ambao wameshaanza kusema kocha Erik Ten Hag aondoke.