Fainali ya maajabu, Yale ya Mapinduzi 2011 yanaweza kujirudia tena?

SIKU 9 za kusisimua zilizoanikiza msimu wa 15 wa michuano ya Kombe la Mapinduzi 2021 zinahitimishwa usiku wa leo wakati utakapocheza mchezo wa fainali.

Watani wa jadi wa soka la Tanzania, Simba na Yanga ndizo zitakazokuwa uwanjani kuanzia saa 2:15 usiku kufunga michuano msimu huu ulioshirikisha jumla ya klabu tisa.

Yanga, Simba, Mtibwa Sugar, Azam na Namungo ndizo zilizowakilisha Tanzania Bara, huku Malindi, Chipukizi, Jamhuri na Mlandege ziliowakilisha Zanzibar.

Yanga ilitinga hatua hiyo kwa kuiondosha Azam FC, mabingwa wa kihistoria wa michuano hiyo kwa mikwaju ya penalti kwenye mchezo mtamu wa nusi fainali iliyopigwa juzi jioni kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Baada ya dakika 90 za kawaida ubao ukisomeka bao 1-1, Yanga ikitangulia kupata bao lao kupitia Tuisila Kisinda kabla ya Obrey Chirwa kusawazisha, timu zilipigiana penalti na Yanga kuibuka wababe kwa mikwaju 5-4.

Watani zao Simba klabu ya pili kwa kutwaa mara nyingi kombe la michuano hiyo ilipenya usiku wa juzi kwa kuiondosha Namungo iliyocheza nusu fainali kama ‘best looser’ kwa mabao 2-1 na kuifuata Yanga katika fainali inayopigwa leo.

Mwanaspoti linakuletea maajabu ya fainali hii ya usiku wa leo na kile kinachoweza kutokea Uwanja wa Amaan wakati wababe hao wa soka nchini wakihitimisha michuano hiyo ya 2021.


FAINALI YA PILI KWAO

Kwa wasiofahamu tu hii itakuwa ni fainali ya pili kwa watani wa jadi hao kukutana katika michuano hii.

Yanga kwao ni fainali ya tatu kwa ujumla katika michuano hii, kwani ilitinga mara ya kwanza 2007 ilipoasisiwa na kufanikiwa kutwaa ubingwa kwa kuichapa Mtibwa Sugar kwa mabao 2-1, wakati watani zao itakuwa ni ya nane kwao.

Simba ilitinga fainali michuano ya mwaka 2008, 2011, 2012, 2014, 2017, 2019 na 2020 na katika mara saba za awali, ilitwaa Kombe mara na fainali nne nyingine ilipoteza.

Awali timu hizi zenye mashabiki wengi nchini na nje ya Tanzania, zilikutana kwa mara ya kwanza katika fainali ya mwaka 2011, iliyokuwa ya msimu wa tano tangu kuasisiwa kwa michuano hiyo mwaka 2007.

Yanga ilikubali kichapo cha mabao 2-0, yaliyowekwa kimiani na washambuliaji Mussa Hassan Mgosi dakika ya 33 na Shija Mkina aliyefunga dakika ya 71 na Simba kukabidhiwa Kombe lenye thamani yaSh 3 milioni na kitita cha fedha taslimu Sh 5 milioni, huku watani zao wakiambulia fedha taslimu Sh 3 milioni za ushindi wa pili.


MIFANANO YA AJABU

Kitu cha ajabu ni kwamba, fainali hii inafanana kwa kiasi kikubwa na ile ya mwaka 2011 iliyochezwa usiku wa siku ya Mapinduzi, yaani Januari 12.

Siku hiyo kama hujui ilikuwa ni Jumatano, kama leo inavyopigwa fainali hii ya 2021.

Kingine ni kwamba pia siku fainali hiyo ya 2011 inapigwa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla zikitoka kufanya Uchaguzi Mkuu wa 2010 uliomuingiza madarakani Dk Mohammed Ali Shein aliyekuwa akiingia madarakani kwa mara ya kwanza.

Safari hii pia, fainali inapigwa Zanzibar na Tanzania ikitoka kufanya uchaguzi wa 2020 na kushuhudia Zanzibar ikiwa chini ya Rais mpya, Dk Hussein Mwinyi.

Cha kusisimua zaidi ni kwamba wakati Dk Shein anaapishwa kuwa Rais ilikuwa Novemba 3, 2010 na safari hii Dk Mwinyi naye aliingia madarakani Novemba 2, 2020.


MAALIM SEIF NAYE

Maajabu mengine ya fainali hii ni kwamba Simba na Yanga zinakutana wakati Maalim Seif Sharif Hamad akiwa Makamu wa Kwanza wa Rais kama ilivyokuwa kwenye fainali za mwaka 2011.

Ndio, baada ya uchaguzi huo Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar, iliyokuwa chini ya Dk Shein ilimteua Maalim Seif kuwa Makamu wa Kwanza kama ambavyo ilivyo sasa, akiteuliwa na Dk Hussein Mwinyi.


MTIBWA KUTEMA UBINGWA

Kama hujui ni kwamba wakati fainali ya 2011 inapigwa, waliokuwa watetezi Mtibwa waliondoshwa na kuliacha taji halina mwenyewe.

Mtibwa ilibeba ubingwa 2010 kwa kuifunga Ocean View kwa bao 1-0 na kushindwa kulitetea katika msimu huo wa 2011.

Hali hiyo imejirudia tena msimu huu, kwani msimu uliopitwa walibeba kwa kuinyoa Simba kwa bao 1-0, lakini safari hii imeshindwa kulitetea taji kwa kutolewa hatua ya makundi na kuwaachia msala Simba na Yanga kama ilivyokuwa 2011.

Haya ni maajabu ya aina yake katika fainali hii ya 2021 kufanana kwa kiasi kikubwa na ile ya 2011.


MAAJABU KUJIRUDIA

Katika fainali hiyo ya 2011, mashabiki wa Yanga walikuwa na presha na timu yao dhidi ya mziki wa Wekundu wa Msimbazi kama ilivyo katika msimu huu, Yanga wakionekana kama hawakuitaka fainali hii dhidi ya Simba. Inayoonekana kuwa bora kulinganisha na Yanga, kama ambavyo ilivyo kwa msimu huu.

Kinachoshangaza zaidi ni kwamba wakati mechi hiyo ya fainali ya 2011 ilipokuwa inapigwa Yanga ilikuwa timu ambayo haijapoteza mechi yoyote ya duru la kwanza la Ligi Kuu Bara kama ilivyo sasa, japo kipindi hicho Simba ndiyo iliyokuwa inaongoza msimamo.

Mfanano mwingine wa fainali hiyo ni Simba kupoteza mechi mbele za maafande kabla ya kwenda fainali hizo za 2011 walipolazwa 1-0 na Polisi Dodoma, kama ambavyo msimu huu imeenda Zanzibar ikipoteza mechi mbili pia za maafande Tanzania Prisons na Ruvu Shooting. Na msimu huu Yanga iliwavua ubingwa Simba katika Ligi Kuu Bara.

Kwa mfanano huo, huenda kilichotokea mwaka 2011 kujitokeza kwa Wekundu kutakata mbele ya Yanga na kuwa klabu ya kwanza kuwafunga msimu huu, japo Yanga ya Cedric Kaze inaweza kupindua meza na kuipa timu ubingwa.

Kwa soka ambazo timu zote zimeonyesha mpaka sasa katika michuano hiyo ya Mapinduzi, lolote linaweza kutokea ingawa kwa matokeo iliyopata Simba katika kundi lake mpaka kufika fainali inatishia amani kwa vijana wa Jangwani ambao fainali zao wamepita kimkandamkanda, japo soka lina maajabu yake. Tusubri tuone dakika 90 zitakazoamua fainali hizo za 2021.