Fei Toto asaini Azam, asema anaipenda Yanga

What you need to know:

MCHEZAJI mpya wa Azam FC, Feisal Salum 'Fei Toto' amesema kuwa licha ya kusaini mkataba wa miaka mitatu kuitumikia klabu yake hiyo mpya lakini bado anaipenda Yanga.

MCHEZAJI mpya wa Azam FC, Feisal Salum 'Fei Toto' amesema kuwa licha ya kusaini mkataba wa miaka mitatu kuitumikia klabu yake hiyo mpya lakini bado anaipenda Yanga.

Fei Toto ameyasema hayo leo Juni 8 wakati anatambulishwa rasmi baada ya uongozi wa Yanga kukubali kumuuza Azam na amewashukuru viongozi wa Yanga pamoja na mashabiki kwa ujumla kwa kipindi alichokaa nao lakini bado anawapenda.

"Napenda kumshukuru sana Rais Samia kwa kufanikisha hili jambo na nazidi kumuombea dua pia nawashukuru viongozi wa Yanga na mashabiki wote kwa muda wote tuliokaa pamoja," alisema Feisal.

Kuhusiana na pesa alizochangiwa na mashabiki na wapenzi wa soka kwenda Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) amesema kuwa hafahamu watu waliomchangia lakini kwa kuwa sio pesa yake halali ataipeleka kwenye vituo watoto yatima, msikitini na kanisani.

"Na pia ile pesa walionichangia sijui nani aliyetoa na nani hajatoa kwahiyo ile pesa nitaangalia kuipeleka kwa watoto yatima, msikitini na kanisani wasiwe na wasiwasi hii si haki yangu ni yao," alisema Feisal

Feisal amesaini mkataba wa miaka mitatu leo mchana kwenye makao makuu ya klabu hiyo Dar es Salaam na kuthibitishwa na Mkurugenzi Mkuu wa klabu hiyo, Yusuf Bakhresa pamoja Ofisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, AbdulKarim Amin 'Popat'.