Fiston afunguka kilichomuangusha Yanga, alivyoikacha Simba

Muktasari:

  • “Kabla ya msimu kumalizika, niliongea na Kaze nikiwa Misri. Alitaka nije kucheza Tanzania lakini nilimwambia bado nafikiria mbele zaidi kwani nguvu zangu bado zinaruhusu.” Fiston

NDO hivyo. Mchezaji wa Yanga, Fiston Abdoulrazak ameamua kufanya maisha mengine nje ya Yanga.

Fiston alitua Yanga dirisha dogo la usajili msimu huu kwa kandarasi ya miezi sita lakini ameshindwa kuonyesha uwezo wake kutokana na kukosa nafasi ndani ya kikosi hicho na Mwanaspoti limefanya naye mahojiano maalum juu ya maisha yake ya soka.


VIWANJA VYAMZINGUA, AKOSA RAHA JANGWANI

Anaelezea changamoto ya viwanja hasa vya mikoani kumkwamisha; “Viwanja ni vibaya mno. Hata mchezaji uwe una uwezo gani wa soka, ni ngumu kuonyesha uwezo huo hasa kwa mchezaji anayetoka nchi zenye vizuri na kila kitu.”

Fiston alianza kuichezea Yanga mechi ya kwanza dhidi ya Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine ambao ulijaa maji.

Pia anasema kuna matarajio mengi yalikuwepo lakini hakuyakuta ikiwamo nguvu ya mashabiki kama ilivyokuwa kabla kutua nchini alipoona nguvu hiyo kwenye mitandao ya kijamii.

Anasema hajawahi kufurahia maisha ndani ya Yanga na hajathaminiwa kama alivyotarajia, kwani soka ndiyo ajira yake hivyo alitegemea kucheza lakini imekuwa tofauti.

“Malengo na maamuzi yangu baada ya changamoto hizi najua mwenyewe ila baada ya kufanya maamuzi ndio nitaweka kila kitu wazi.”

“Kabla ya Yanga kuonyesha nia yoyote binafsi nimetangaza nia yangu siwezi kubaki katika timu hii hata kama wakinihitaji vipi kuongeza mkataba mpya”


AMKUMBUKA KAZE, AMKUBALI SAIDO

Anasema Cedric Kaze ndiye sababu ya yeye kuja nchini na ni kutokana na kumwamini kwani alishafanya kazi chini yake.

“Kabla ya msimu kumalizika, niliongea na Kaze nikiwa Misri. Alitaka nije kucheza Tanzania lakini nilimwambia bado nafikiria mbele zaidi kwani nguvu zangu bado zinaruhusu.”

“Hata hivyo, aliniambia Yanga inahitaji kumaliza msimu ikiwa bingwa na wanahitaji msaada wangu. Nilimheshimu sana hivyo, niliamua tu kufanya maamuzi ya kujiunga nae na aliniunganisha na Hersi Said na nilisaini na klabu hii.”

Kutokana na uwezo wake aliamini atacheza hata kama Kaze asipokuwepo, tofauti na matarajio yake na kuongeza kama angekuwa kiongozi wa Yanga asingemwondoa Kaze ili amalize msimu kwani anaamini angemaliza ngwe yake vizuri.

Kuhusu Saido Ntibazonkiza alitamani sana acheze ssana na Saido kwani anaamini wangeelewana na hata Kocha Kaze anawafahamu na wao kila mmoja anajua aina ya uchezaji wa mwenzake na wanapambana sana kama ilivyo kwa kina Tuisila Kisinda.


HIKI KINAIUA YANGA

Kati ya mambo anayoyashuhudia na hayampendezi ni timu kubadilika kila mara na kushindwa kutengeneza muunganiko mzuri.

“Timu haikai pamoja muda mrefu. Mkikaa pamoja mnajuana na kufahamiana vizuri. Wenzetu wanaofanya vizuri ni kwa sababu wachezaji wamekaa muda mrefu pamoja,” anasema na kuongeza ni ngumu kwa kutarajia makubwa kutoka kwa mchezji wa kigeni ndani ya msimu mmoja na anahitaji muda kuzoea mazingira.


AITAJA AZAM FC

“Angalau Azam jinsi wanavyoishi navutiwa nao na hata ingekuwa nafasi ya ngapi kwenye msimamo wa Ligi Kuu, wanajua namna gani ya kuishi na mchezaji,” anasema na kuongeza hajazungumza na timu yoyote hadi sasa na mkataba wake na Yanga utakapomalizika atasonga mbele zaidi.


MBIO ZA UBINGWA

Simba ipo kileleni mwa msimamo wa ligi na Fiston anaamini kukaa kwao pamoja ndio kumewapa mafanikio. Hata hivyo anaamini hata Yanga ipo kwenye nafasi ya ubingwa.

“Yanga ikiamua kuchukua ubingwa inaweza kwa kuwa ina wachezaji wazuri kama Sarpong, Tusila, Mukoko, Saido, Mimi, Lamine, Farouk, Yacouba wote hawa ni wazuri sana, hivyo kuchukua ubingwa inawezekana endapo watazoeana zaidi,” anaeleza Fiston ambaye anamkubali zaidi Haruna Niyonzima kutokana na umahiri wake wa kucheza soka.


ALIVYOIKACHA SIMBA

Mwaka 2013, Simba ilionyesha nia ya kumsaini baada ya kutamba kwenye michuano ya Challenji iliyofanyika Kenya.

Simba ilimkosa baada ya kutua Diables Noirs na mwenyewe anasema sio wao tu hata TP Mazembe waliwahi kumtaka lakini akaitosa;

“Hata TP Mazembe wakati huo walikuwa wakinitaka pia nikaenda Mamelody Sundowns, mpira ndio kazi yangu hivyo naangalia masilahi pia,” anasema na kutamba angekuwa Simba angekuwa amefunga mabao mengi.


ANAJIVUNIA HAYA

Moja ya mafanikio anayojivunia kupitia soka ni kuwajengea wazazi wake nyumba na yake binafsi eneo ambalo aliyekuwa Rais wa Burundi, Marehemu Pierre Nkuruzinza alikuwa akiishi.

“Sio mchezo kujenga eneo ambalo Rais wetu alikuwa akiishi, lakini kwa kidogo Mungu alichonibariki niliweza kujenga na naendesha maisha yangu na mke wangu na wanangu,” anasema Fiston ambaye tangu ametua Yanga amecheza mechi nne na kufunga mabao mawili.


WASIFU

Jina - Fiston Abdoulrazak

Kuzaliwa - Septemba, 05, 1993

Mahala alipozaliwa - Bujumbura,
Burundi

Urefu: 1.75 m (5 ft 9 in)

Nafasi - Mshambuliaji


TIMU ALIZOPITA


2009ñ12 - LLB AcadÈmic

2012 - Rayon Sports

2013 - Diables Noirs

2014/15 - Sofapaka

2015/16 - Mamelodi Sundowns

2016/17 - Bloemfontein Celtic

2017 - 1∫ de Agosto

2018 - Al-Zawraa

2018 /19 - JS Kabylie

2019/20 - ENPPI SC

2021 - Yanga