Fraga anarudi Simba

WATETEZI wa Ligi Kuu Bara, Simba ipo njiani kurejea Dar es Salaam ikitokea Tabora ambapo jana jioni ilimalizana na KMC katika mechi yao iliyopigwa Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, lakini taarifa njema kwa mashabiki wake ni kurejea kwa fundi wa mpira kutoka Brazili, Gerson Fraga.

Brazili huyo aliachwa kwenye dirisha dogo la msimu uliopita baada ya kuwa majeruhi wa muda mrefu tangu alipoumia kwenye mechi kati ya timu yake na Biashara United iliyopigwa Septemba 20, mwaka jana kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar na Simba kushinda mabao 4-0.

Jereha la goti lilimfanya mabosi wake kumtema na kumsajili Taddeo Lwanga kutoka Uganda ambaye naye kwa sasa ni majeruhi wa muda mrefu, huku ikielezwa kuwa huenda akatemwa jumla kwenye dirisha hili dogo la usajili na Mbrazili huyo kurejeshwa kikosini.

Simba ilimsajili Fraga Juni 25, 2019 kwa mkataba wa miaka miwili akitokea ATK ya Ligi Kuu India, akiwa miongoni wa Wabrazili waliosajiliwa msimu huo, akiwamo Tairone Santos na Wilker Henrique.

Taarifa kutoka ndani ya Simba, inaelezwa Fraga ameomba kurejea kikosini kwangu kwa sasa yupo fiti baada ya kujiuguza hadi kupona.

Mabosi wa Simba baada ya kuliona hilo walimfahamisha kocha wao, Pablo Franco kuwa Fraga anataka kurejea nchini ili aje kuziba nafasi ya Taddeo Lwanga atakayekuwa nje kwa msimu mzima.

Fasta Mhispania huyo, aliomba kuziona video za Fraga, kisha akawaambia kamam vipi Fraga aje kukinukisha kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi 2022 ili amuone kabla ya kuridhia asaini mkataba wa kuichezea Simba.

Fraga kama ataonyesha kiwango bora kwenye michuano hiyo ya Mapinduzi itakayoanza Januari 2 ndio atapewa mkataba wa miaka miwili kuitumikia Simba, ila akishindwa kuonyesha ubora atapewa posho na tiketi ya kurudi kwao Brazil.

Fraga aliichezea Simba msimu wa 2019-2020 na kuifungia mabao matatu ya Ligi Kuu na moja kwenye nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (ASFC) walipoifumua Yanga kwa mabao 4-1.

Katika mchuano hiyo ya Mapinduzi, Simba imepangwa Kundi C, sambamba na timu za Selem View na Mlandege, kinara wa kundi lao atafuzu nusu fainali.