Fundi wa Lupopo ajipeleka Simba

Dar es Salaam. Kocha Mkuu wa Simba, Roberto Oliveira 'Robertinho' mjanja sana kwani wakati akijipanga kumalizia mechi za msimu huu katika michuano ya kimataifa na ya ndani, lakini tayari ameanza kuweka mambo sawa kwa msimu ujao ili kuhakikisha Wekundu hao wanatisha zaidi uwanjani.

Moja ya mambo aliyoanza kufanya kazi kwa sasa ni kusaka baadhi ya nyota wa eneo la kiungo kwa msimu ujao na tayari mabosi wa klabu hiyo wameanza kuchangamka kwa kupiga hodi FC Lupopo ya DR Congo kumuulizia mkata umeme mmoja anayekipiga timu hiyo Kombe la Shirikisho Afrika na fundi huyo wa mpira, Harvy Ossete amesema hana hiyana kutua Msimbazi kama wanamtaka kweli.

Robertinho na vijana wake wamecheza mechi ya mwisho leo hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika ikikubali kichapo cha mabao 3-1 kutoka kwa Raja Casablanca nchini  Morocco wakati tayari wameshakata tiketi ya robo fainali kwa mara ya tatu ndani ya misimu mitano iliyopita.

Lakini kigogo mmoja wa Simba inaelezwa amenyanyua simu na kuwapigia mabosi wa FC Lupopo inayoshika nafasi ya tatu kwenye Kundi A la Shirikisho kumuulizia kiungo huyo mkabaji anayekipiga na nyota wa Kitanzania George Mpole.

Ossete ambaye ni raia wa Jamhuri ya Congo, anatajwa kuwa kati ya viungo wanaotazamwa kwa sifa ambazo Robertinho anazihitaji kikosini, akiwa na uwezo wa kukaba kama ilivyo kwa Sadio Kanoute, anachesha timu na anaweza kucheza kama beki wa kati akihitajika japo si eneo lake halisi.

Inaelezwa mabosi wa klabu hiyo tayari wameshapigiwa simu juu ya dili hilo, huku wakala wa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23 na aliyewahi kuichezea Diables Noirs, inayoshiriki makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, akitafutwa ili kuweza kulainisha mambo.

Kiungo huyo fundi wa mpira alipotafutwa na Mwanaspoti alisema licha ya kwamba ni mchezaji wa FC Lupopo, lakini anatamani kucheza Ligi Kuu Bara kwani ni kati ya ligi zinazomvutia na iwapo Simba ipo siriazi naye hatakuwa na hiyana kujiunga nayo, mradi tu wamalizane na mabosi wake.
"Kama mchezaji huwa nafuatilia kile kinachoendelea kwenye ligi nyingine, wapo wachezaji wengi ninaowafahamu na kuheshimu kile ambacho wanafanya kama vile Mayele (Fiston)," alisema Ossete na kuongeza;

"Bado sijawa na taarifa rasmi juu ya kutakiwa na Simba, ila sio jambo baya kuhusishwa na timu kubwa kama hiyo ya Tanzania hiyo inanipa picha kuwa kazi yangu inaonekana, bado nina mkataba (Lupopo) na ninauheshimu hivyo kwa lolote wanapaswa kufanya mawasiliano na klabu yangu."

Inadaiwa uamuzi wa mabosi wa Simba kuanza kumfuatilia kiungo huyo imetokana na ripoti ya kocha Robertinho ambye alikakariwa pia na Mwanaspoti kwamba ameanza kuangalia wachezaji wa kuongezwa kikosi kwa msimu ujao kupitia mechi za Ligi Kuu na zile za kimataifa za msimu huu.

Hata hivyo, mabosi wa Simba wanapawa kuvunja benki kama kweli imempania kiungo huyo kwani itapaswa kuununua mkataba alionao na klabu yake ya sasa unaoisha Juni 30, 2025.
Akimzungumzia mchezaji huyo, Mfungaji Bora wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita, George Mpole anayecheza na Ossete ndani ya FC Lupopo, alisema ni mchezaji mzuri anayewezaa kuisaidia Simba.

"Ni mchezaji mzuri sana, najua ubora wake kwa sababu nacheza naye timu moja, pia ni kijana anayeweza kuitumikia timu hiyo kwa muda mrefu, iwapo watamnasa," alisema Mpole aliyebeba tuzo hiyo akiwa na Geita Gold kwa mabao 17 akimzidi Fiston Mayele wa Yanga aliyemaliza na 16.

Katika wiki hii ya kimataifa, Ossete alikuwa sehemu ya kikosi cha Jamhuri ya Congo ambacho kilicheza michezo miwili ya nguvu ya kuwania nafasi ya kwenda Ivory Coast kwa ajili ya fainali za mataifa ya Afrika dhidi ya Sudan Kusini.

Mchezo wa kwanza ambao walipoteza wakiwa nyumbani kwa mabao 2-1, alicheza kwa dakika 90 huku ule wa marudiano ambao walishinda kwa bao 1-0 akicheza dakika moja.
Simba ambao wamekuwa hawana mbadala wa nguvu pindi ambapo akikosekana mmoja kati ya Mzamiru Yassin au Kanoute,itawabidi kuingia mfukoni na kutoa zaidi ya Sh. 200 milioni ili kunasa saini ya mchezaji huyo ambaye bado ana mkataba na FC Lupopo hadi 2025.

Mbali na Simba kuhitaji na kiungo mpya wa nguvu lakini pia inaelezwa kuwa Robertinho amewaeleza viongozi kuwa anauhitaji na mshambuliaji mmoja wa kati ambaye ataongeza nguvu kwenye kikosi chake kuhusu nani na nani wanaweza kuwapisha njia ambao wapo njiani kutua Simba ni suala ambalo maamuzi ya mwisho itakuwa mwisho wa msimu.