Geita Gold, Mpole ndoa yavunjika aisee!

Muktasari:

  • BAADA ya mvutano wa muda mrefu baina ya klabu ya Geita Gold na mshambuliaji wake, George Mpole hatimaye ndoa yao imevunjika rasmi leo.

BAADA ya mvutano wa muda mrefu baina ya klabu ya Geita Gold na mshambuliaji wake, George Mpole hatimaye ndoa yao imevunjika rasmi leo.

Kupitia barua iliyovuja ya mshambuliaji huyo kusitishiwa mkataba ilisema, "Uongozi wa klabu ya Geita Gold, unakutaarifu rasmi ya kwamba mkataba wako wa ajira kati ya klabu na wewe (Mpole) umemalizika rasmi leo baada ya pande mbili kukubaliana na uko huru kujiunga na klabu yoyote kuanzia leo,"

"Tunachukua fursa hii pia kukushukuru kwa kazi, ushirikiano na utendaji mzuri uliouonyesha kwa klabu kwa kipindi chote tangu tumekuwa pamoja mpaka tulipokubaliana kusitisha mkataba wetu. Pia tunakutakia kila la kheri katika maisha yako ya mpira wa miguu," imesema taarifa hiyo.

Sakata la George Mpole na klabu yake limeanza kufukuta tangu Oktoba 13, mwaka huu baada ya mchezo wa raundi ya saba ambapo nyota huyo hakuungana na wenzake kwa maandalizi ya michezo iliyofuata.

Mpole hakuonekana kambini kwenye michezo mbalimbali ya timu hiyo kwa kile alichoeleza kuumwa na yuko nyumbani kwao mkoani Mbeya anatibiwa kwakuwa madaktari wa timu hiyo wameshindwa kumpa tiba huku baadhi ya taarifa zikidai mshambuliaji huyo anadai stahiki zake za mshahara wa mwezi wa 10.

Hata hivyo, Novemba 17, mwaka huu klabu yake ilimpa wiki moja ya kuripoti kwenye kituo cha kazi ili kuendelea na program za timu na kama angeshindwa kuhudhuria angechukuliwa hatua kali za kinidhamu, baada ya kutoonekana kwa muda mrefu huku uongozi ukiwa hauna taarifa yoyote.

Hivi karibuni Mpole alirejea Geita kujiunga na timu hiyo ambapo Desemba 4 alikuwa sehemu ya kikosi cha timu hiyo kilichocheza dhidi ya Mtibwa Sugar na kulazimishwa sare ya 2-2 katika Uwanja wa Nyankumbu huku akiishia benchi.

Afisa habari wa klabu hiyo, Hemed Kivuyo amethibitisha barua taarifa hizo ni za kweli kuwa Geita Gold imesitisha mkataba na Mpole.

Naye, Mwenyekiti wa bodi ya timu hiyo, Constantine Morandi akisisitiza kuwa klabu hiyo haina uhitaji na mchezaji huyo na inamtakia kila la kheri katika safari yake ya soka.