Hakuna matuta, sapraizi kibao

LICHA ya kwamba viongozi wanafanya siri kubwa lakini kuna sapraizi kadhaa ambazo mashabiki wanaweza kukutana nazo kwenye fainali ya leo ndani ya Uwanja wa Amaan.

Simba inaweza kuwaingiza kikosini mastaa watatu Luis Jose, Clatous Chama na Tshabalala huku Yanga ikimwita Saido Ntibazonkiza.

Chama, Luis na Saido hawakuwepo kwenye vikosi hivyo kutokana na majeraha, lakini jana kulikuwa na mikakati ya haraka ya kuhakikisha wanavuka boda.

Ingawa Luis aliliambia Mwanaspoti; “Timu iliyocheza mpaka tunafika fainali ni nzuri, sioni kama kuna sababu ya kufanya mabadiliko, ningependa kuona wale ndio wanamalizia kwa vile wamefanya kazi nzuri. Mimi nipo Dar.”

Mechi ya leo inatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa wa kiuchezaji kutokana na rekodi zao huku Yanga ikitaka kuendeleza rekodi yao ya kutopoteza mchezo ndani na nje ya Bara. Lakini mastaa wamesisitiza hakuna penalti mechi hiyo itamalizika ndani ya dakika 90.

Kocha wa Yanga, Cedrick Kaze na Kaimu Kocha Mkuu wa Simba, Seleman Matola wamesisitiza fainali haina ufundi ndio mchezo wa kipekee kwa timu yoyote duniani lakini kila mmoja kavutia ushindi kwake.

Mara ya mwisho watani wa jadi Simba na Yanga walikutana kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara msimu huu ikiwa ni mechi ya mzunguko wa kwanza na walitoka sare, mechi hiyo ilichezwa Uwanja wa Mkapa, jijini Dar es Salaam.

Azam FC ambayo ilitolewa hatua ya nusu fainali ndiyo inayoongoza kwa kubeba ubingwa huo mara tano ikicheza fainali sita wakati Mtibwa Sugar wakitwaa mara mbili wakicheza fainali mara sita.

Timu nyingine iliyowahi kuingia fainali ni URA ya Uganda ambayo imecheza fainali hizo mara mbili.

Msimu huu Simba na Yanga kila mmoja amepania kuonyesha kiwango chake na Simba mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara wanataka kuonyesha kwamba kutwaa ubingwa wa Bara mara tatu mfululizo na kuingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika hawakubahatisha bali ni kuwa na kikosi bora.

Yanga nao ambao wanaongoza ligi ya Bara pasipo kupoteza mechi hata moja nayo inataka kudhihirisha wanachokifanya Bara hawabahatishi hivyo ubingwa huo wanautaka na ndio maana jeshi lao chini ya Cedric Kaze lipo huku.

Mechi hiyo inayotarajiwa kuwa na mashabiki wengi kutoka Bara na visiwani hapa kutokana na timu hizo kuwa na mashabiki wengi viingilio pia vitabadilika kutoka vile vya awali ambavyo ilikuwa ni 3000, 5000 na 10,000.

Leo viingilio vitakuwa ni Sh5000, 10000 na 15000 na uwanja huo huingiza mashabiki zaidi ya 12000, huku Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano akisema hayatakuwepo masharti yoyote ya Caf ya kuingiza nusu ya mashabiki.

Akizungumzia dabi, Kaze alisema; “Tumecheza na Azam moja ya timu bora na kubwa, tulijaribu kutoa presha ili kupata matokeo ya mapema tulipata lakini baadaye walianza kufika eneo letu kirahisi ndiyo maana walisawazisha na hii inatokana na presha tuliyokuwa nayo.”

“Tulikuwa tayari kucheza na timu yoyote ambayo ingeingia fainali, lakini tunafurahi zaidi pia kucheza na Simba, tutajiandaa kuona ni namna gani tunafanya vizuri kwenye mechi hiyo kuhakikisha tunatwaa ubingwa.

“Simba sio timu mbaya na hata tulizocheza nazo hazikuwa vibaya ila katika mashindani ni lazima kujiandaa kwa kila mechi ili kupata matokeo mazuri, tunawaheshimu Simba,” alisema Kaze na kuongeza kufafanua juu ya mchezaji wake Said Ntibanzonkiza

“Anaendelea vizuri lakini siwezi kusema mechi hiyo atacheza ama hatacheza kwani itategemea na namna atakavyoamka ingawa alianza kufanya mazoezi na wenzake,” alisema Kaze.

Kipa wa Yanga, Shikalo alisema; “Tutaingia na mkakati mzuri fainali na uhakika wa kushinda upo kwa vile timu ipo vizuri na tutajitahidi kuwafurahisha mashabiki wetu.”

Kwa upande wa Kocha Msaidizi wa Simba, Seleman Matola alisema wametinga hatua hiyo wakiwa wamepambana na timu ngumu hivyo wanaamini mechi hiyo watashinda.

“Tumepata matokeo mazuri katika mechi zetu zote zilizopita hivyo hata hii ya fainali tunataka ushindi utakaotuwezesha kutwaa ubingwa wa Mapinduzi.

“Hakuna fainali rahisi sehemu yoyote ile na kwa vile tunautaka huu ubingwa lazima tujiandaa vizuri maana hata wapinzani wetu nao wanajiandaa, tunategemea kuwa ni mechi itakayokuwa na ushindani mkubwa na lazima bingwa apatikane,” alisema Matola huku staa wake, Luis akiwaaminisha mashabiki kila kitu anaamini kitakwenda sawa na watampiga Yanga mapema tu hata yeye asipocheza kwani mziki uliopo Zenji siyo wa kitoto na Miraji yuko fiti sana.

Straika wa Simba, Meddie Kagere alisema; “Sisi tunajua ni nini mashabiki wetu wanataka na ndio maana kila tunapoingia uwanjani tunajitahidi kuwafurahisha. Fainali itakuwa na matokeo mazuri sana.”

Matola na Kaze kwenye mashindano hayo wameonekana kupenda kutumia mfumo wa 4-2-3-1 ili kupata matokeo mazuri vikosi vyao kwenye mechi hiyo vinaweza kuwa hivi.

Mbali na mfumo huo Kaze pia hupenda kubadilisha mfumo kulingana na namna wapinzani wake walivyo, pia hutumia 4-4-2 na 3-5-1-1.


Vikosi vinavyoweza kuanza leo saa 2:15 usiku;

Simba: Beno Kakolanya, David Kameta ‘Duchu’, Tshabalala, Kennedy Juma, Joash Onyango/Wawa, Yassim Mzamiru, Francis Kahata/Chama, Taddeo Lwanga, Meddie Kagere, Hassan Dilunga na Miraji Athuman.

Yanga: Farouk Shikhalo, Kibwana Shomari, Adeyun Saleh, Said Makapu, Abdallah Shaibu, Mukoko Tonombe, Tuisila Kisinda, Zawadi Mauya, Saido Ntibazonkiza, Haruna Niyonzima na Yacouba Sogne.


NINJA AITAKA TENA PENALTI

Katika mechi yao ya nusu fainali Yanga ilipocheza na Azam Fc, Yanga ilishinda penalti 5-4 na Ninja alipiga penalti ya tano.

Matokeo ya dakika 90, timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1 hivyo kulazimika kuingia kwenye matuta ili kupata mshindi.

Wakati Ninja anakwenda kupiga penalti hiyo mashabiki wengi walionekana kukata tamaa wakiamini mchezaji huyo atakosa kwani hana utaalumu wa kupiga penati.

Ninja ameliambia Mwanaspoti mashabiki wamekariri kuona fulani ndiye anayeweza kupiga penalti lakini yeye aliaminiwa na kocha wake.

“Kwanza sijawahi kupiga penalti tangu nijiunge Yanga yaani maisha yangu yote ya Yanga haijawahi kutokea, hii ilikuwa ni mara ya kwanza. Nilifanya hivyo kwa sababu tulifanyia kazi hilo na kocha aliniambia ikitokea tumefika hatua ya matuta basi nipige penalti ya tano na ndiyo nilipiga na kufunga.

“Mechi ya fainali hatutaki tufikie kwenye matuta lakini ikitokea hivyo basi pia nitapiga penalti kwani najiamini na ninaendelea kufanyia kazi mazoezini kama tunavyofundishwa, kocha anapompanga mtu huwa anaangalia mazoezini amefanyaje, mashabiki wanapaswa kuamini kila mchezaji kuwa anaweza kufanya jambo fulani,” alisema Ninja

Kuhusu fainali hizo Ninja alisema; “Labda kuwe na mabadiliko kwa Simba lakini naona tofauti na ilivyokuwa mechi iliyopita, ingawa fainali lazima iwe ngumu kwani lazima bingwa apatikane kwa njia yoyote ile, kikubwa ni kujipanga na ndio maana tunataka kumaliza mchezo mapema yaani tupate ushindi ndani ya dakika 90.

“Tunajiamini lakini hatuwezi kuwadharau Simba maana haya ni mashindano, tunataka ubingwa na wao wanautaka hivyo hii ni kama vita ingawa ratiba imekuwa bgumu kwani mechi hazijapishana,” alisema Ninja