Hao kina Aziz Ki wanakula Sh400 milioni, mishahara yapanda asilimia 100

Muktasari:

  • ILI kulipa mishahara yote ya mastaa wa Yanga kwa mwezi, unahitaji kuwa na Sh400milioni kwenye akaunti, Mwanaspoti limethibitishiwa na Injinia Hersi, Rais wa klabu hiyo.

ILI kulipa mishahara yote ya mastaa wa Yanga kwa mwezi, unahitaji kuwa na Sh400milioni kwenye akaunti, Mwanaspoti limethibitishiwa na Injinia Hersi, Rais wa klabu hiyo.

Lakini kwa mujibu wa maktaba ya Mwanaspoti kiasi hicho ni ongezeko la zaidi ya asilimia 100 kulinganisha na mwaka jana ambapo mishahara yote ya wachezaji na sekretarieti ilikuwa zaidi ya Sh170milioni nje ya posho ambazo zilikuwa juu.

Habari za ndani ya Yanga ambazo Hersi hakutaka kuziingia kiundani, zinasema kwamba ongezeko hilo la kwenye mishahara limeathiri posho kwani zimeshushwa tofauti na msimu uliopita ingawa bado imekuwa siri kubwa. Yanga wameboresha viwango ambavyo kila mchezaji ataweza kuishi maisha mazuri na kupambania kibarua na mshahara wake. Msimu uliopita Yanga ilikuwa ikiongoza kwa kulipa posho kwenye Ligi Kuu Bara kwani katika mechi za watani walikuwa wakiahidiwa hadi Sh500Milioni lakini sasa ni nadra kuzidi Sh100 milioni.

Hivyo kwa msimu huu wanakadiria kwamba wanahitaji Sh5 Bilioni kwa mwaka mmoja kwaajili ya mishahara tu ya kikosi hicho chenye maingizo mengi mapya ya kigeni yenye gharama kubwa sambamba na muundo mpya wa uongozi ambao na wenyewe umeambatana na mishahara iliyochangamka kwani kuna wataalam wengi wa nyanja mbalimbali.

Hersi ameliambia Mwanaspoti Jijini Dar es Salaam kuwa, ili kusajili timu bora kama yao ya sasa unahitaji kuwa na fedha isiyopungua Sh1.5 Bilioni katika kuwalipa wachezaji ada za usajili na mastaa wa kigeni ndio wachezaji ghali zaidi.

“Kwenye klabu kubwa kama Yanga kuna maeneo mengi ambayo yanaongeza gharama za uendeshaji, nikianza cha kwanza kwa mfano mwanzoni mwa msimu unahitajika kufanya usajili wa wachezaji, ili uweze kufanya usajili uliobora utahitajika kuwa na kiasi kama Bilioni moja mpaka Bilioni moja na nusu mezani,” alisema Hersi.

“Hapo utapata timu imara ambayo itaweza kukusaidia kwenye mashindano, sokoni sasa ukitaka mchezaji bora unatakiwa kuwa na Dola 50,000 mpaka 100,000 hiyo na Sh200 milioni na zaidi. Ukiwa na wachezaji watano tu wa namna hiyo unatakiwa kuwa na Bilioni moja, bado kikosi chako kinahitaji kuwa na wachezaji 27 utaona hesabu zilivyo hapo.

“Usisahau hao wachezaji kila msimu wana ada zao za usajili kwa hiyo bajeti yako inatakiwa kuwa hivyo, hiyo tu peke yake ni eneo la kwanza la gharama,”alisema na kuongeza kuwa ili kumudu kulipa mishahara ya timu yao kwa sasa yenye mastaa kama Stephane Aziz KI, Yanick Bangala, Djigui Diarra, Feitoto na mshambuliaji wao bora Fiston Mayele unahitaji kuwa na Sh300-400 Milioni kwa mwezi. Hesabu hizo ni sawa na kiasi kisichopungua Sh5 Bilioni kwa mwaka ambapo unakuwa na uhakika wa kuhakikisha wa kuwalipa mastaa wote wa timu hiyo lakini kwa makadirio wakikaa mkoani kwa mechi kwa wiki moja inawagharimu Sh100 milioni.

“Chukulia timu inatoka hapa jijini Dar es Salaam inakwenda labda Mwanza, chukulia kama msimu uliopita tulipokwenda kucheza dhidi ya Geita Gold na baadae Simba, unahitajika kukaa karibu wiki moja hapo utahitaji kuwa na kiasi kama Sh100 milioni hapo utalipia chakula, hoteli, usafiri wa ndege kwenda na kurudi na usafiri wa ndani mkiwa hapo Mwanza,”alisema.

Aliongeza kuwa licha ya gharama hizo kuwa kubwa uongozi wake unapambana kuhakikisha unatafuta fedha zaidi kuhakikisha Yanga inajiendesha yenyewe kiuchumi hali ambayo sasa bado wamepiga hatua lakini siyo kwa kiwango walichopanga na ndio maana wanazidi kupambana.