Hersi: Tumealikwa nchi tatu kwa ajili ya maandalizi

Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said, amesema timu hiyo itafanya usajili bora zaidi msimu ujao tofauti na ilivyokuwa kwa msimu uliopita.

Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Klabu hiyo, Hersi, amesema moja ya malengo makubwa kwao kama uongozi ni kuona wanafanya vizuri zaidi ili kukidhi mahitaji ya mashabiki na wanachama wa kikosi hicho.

"Niwahakikishie ndugu zangu, msimu ujao tutafanya usajili mzuri ukiambatana na benchi bora la ufundi, lengo ni kufikia mafanikio ya ndani na nje ya nchi," amesema.

Hersi aliongeza, tayari wameshapata mialiko ya zaidi ya nchi tatu kwa ajili ya kuweka kambi ya maandalizi ya msimu mpya 'Pre Seasons'.

"Tuna timu zinazotoka Ulaya ambazo zimetuomba kwenda kwao na hiyo itakuwa ni surprise (mshangao), nchi nyingine ni Kenya na Afrika Kusini ambazo tumepokea mialiko yao na tutakaa na kuifanyia kazi,"amesema.

Aidha Hersi amesema, sababu kubwa ya kupata mialiko kwa upande wa Kenya ni kwa ajili ya kufungua Uwanja wao wa kisasa wa Kisumu huku kwa upande wa Afrika Kusini wakiwa wamealikwa na Kaizer Chiefs ambao msimu uliopita waliwaalika katika Kilele cha Wiki ya Mwananchi.