Huyo Gomes amedamshi Simba!

Muktasari:

Gomes ameiongoza Simba mechi 17 katika michuano mitatu ya mashindano.

HUENDA mashabiki wa Simba wamepitiwa. Pengine ni kutokana na furaha kubwa waliyonayo kwa sasa kwa chama lao ambalo limekuwa likiwapa burudani kwenye mechi zake.

Lakini ukweli ni kwamba Jumanne ijayo ikiwa ni siku nne tu kabla ya Kocha Mkuu wa Simba, Didier Gomes hajakiongoza kikosi kwa mara ya kwanza dhidi ya Yanga katika mechi ya Kariakoo Derby, Mfaransa huyo atakuwa akitimiza siku 100. Ndio. Gomes alitua nchini na kuanza kazi Simba, Januari 24 na hadi Mei 4 atakuwa ametimiza siku 100 kamili tangu awe na kikosi hicho cha Wekundu wa Msimbazi, huku rekodi zake zikimbeba kinoma.

Kocha huyo alipotua aliibukia mazoezini Mo Simba Arena kwa maandalizi ya michuano maalumu ya kirafiki ya Simba Super Cup na kufanya mambo kwa kubeba taji hilo lililoandaliwa na klabu yake ikishirikisha timu za TP Mazembe ya DR Congo na Al Hillal ya Sudan. Baada ya hapo Gomes alianza kazi Ligi Kuu Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika, na huko jamaa alidhihirisha kwamba Simba haikufanya makosa kumng’oa Al Merrikh ya Sudan na kumleta nchini.

Katika mechi 17 alizoiongoza Simba kwenye michuano hiyo miwili, Simba imepoteza mchezo mmoja na kupata sare tatu, huku mechi 13 ikishinda zikiwamo nne za Ligi ya Mabingwa na nane za Ligi Kuu Bara. Mbali na hizo, pia Wekundu wa Msimbazi chini ya Mfaransa huyo ilishinda mechi moja ya Kombe la FA, ambapo Simba iliifumua African Lyon katika hatua ya 32 Bora kwa mabao 3-0.

Ukichukua mechi zote za michuano hiyo mitatu, Gomes ameiwezesha Simba kufunga mabao 33 na kuruhusu wavu kuguswa mara saba kuonyesha jinsi gani alivyo kocha wa mipango wakati usiku wa leo akiiongoza timu yake dhidi ya Kagera Sugar katika mechi ya ASFC.

Jioni ya jana, Gomes alikuwa akiisikilizia droo ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya robo fainali ambapo atakuwa na kazi ya kuivusha Simba kuingia nusu fainali.

Kama ataivusha Simba hadi nusu fainali ataifikia rekodi ya klabu hiyo ya 1974 wakati michuano hiyo ilipokuwa ikifahamika Klabu Bingwa Afrika.

Pia, kocha huyo ana nafasi ya kuboresha rekodi yake wakati usiku huu wakiikaribisha Kagera kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Kama atashinda mchezo huo itamfanya kuiongoza Simba katika mechi za mashindano 18 na kuvuna pointi na mabao ya kutosha kuo-nyesha kwa-mba, jamaa yupo vizuri na hata wapinzani wao kwenye michuano hiyo lazima wajipange kwani Mfaransa huyo ni moto.


MTIHANI HUU HAPA

Licha ya rekodi hizo tamu ndani ya muda mfupi, lakini Gomes ana kibarua cha kufikia zilizowahi kuwekwa na Dragan Popadic. Kama hujui ni kwamba Simba haijawahi kupata kocha bora wa Kizungu kama ilivyokuwa Popadic aliyeinoa timu hiyo kwa misimu mitatu kuanzia 1994-1996. Ndiye kocha Mzungu aliyedumu Msimbazi kwa muda mrefu kuliko yeyote hadi sasa.

Kocha huyo Mserbia (zamani Yugoslavia), aliipokea timu hiyo toka mikononi mwa makocha Abdallah Kibadeni na Etienne Eshente walioifikisha Simba fainali za Kombe la CAF 1993 na kupoteza nyumbani kwa mabao 2-0 mbele ya Stella Abdijan. Ikiwa mikononi wa Popadic, Simba ilitetemesha Afrika Mashariki na Kati. Timu zilizokuwa zikicheza nayo enzi hizo ziliogopa kufanya madhambi eneo la hatari au kutoa mipira ya kona. Popadic aliwafundisha wachezaji jinsi ya kupiga faulo na kona. Mbali na soka hilo, piai akiwa Msimbazi, Popadic aliiwezesha Simba kunyakua mataji saba tofauti - mawili ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (sasa Kagame) 1995 na 1996. Pia aliipa ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara mbili mfululizo 1994 na 1995. Aliipa pia taji la Ligi ya Muungano 1994 na 1995 baada ya awali kuipa ubingwa wa Kombe la Nyerere 1995.

Hii ina maana Gomes ana kibarua kizito kilichowashinda makocha wengine wa Kizungu