Huyo Nyoni kazaliwa upyaaa

Saturday August 06 2022
Nyoni PIC
By Thobias Sebastian

UKISEMA kiraka wa Simba, Erasto Nyoni amezaliwa upya katika soka wala utakuwa haujakosea kutokana na kiwango bora alichoonyesha katika maandalizi ya msimu ujao hapa Ismalia, Misri.

Msimu uliopita Nyoni hakuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza na hakucheza mechi nyingi huku wengine wakiamini ameshuka uwezo ndio maana anakutana na changamoto hiyo.

Kulingana na mazoezi ya Simba huku Ismalia, Nyoni alikuwa moto na kwenye kiwango bora katika kila zoezi hadi kocha wa timu hiyo kuonekana kuvutiwa naye.

Katika mazoezi ya nguvu Nyoni alifanya vizuri ya kucheza mpira ndio alikuwa kwenye kiwango bora kama ambavyo alionyesha katika mechi nne za kirafiki.

Nyoni alisema anaendelea kufanya mazoezi na kujiandaa zaidi kwani hiyo ndio kazi yake na changamoto kwa binadamu yoyote zinatokea hata katika maisha ya kawaida.

Alisema benchi la ufundi ndilo linalofahamu yupo katika hali gani ya utimamu kwa ajili ya kuipigania timu yeye amefanya kila ambalo lilikuwa ndani ya uwezo wake.

Advertisement

“Ukiangalia kuna mechi nilicheza kama kiungo wa ukabaji baadaye beki wa kati hilo ni jukumu langu kufanya kwa ubora vile ambavyo benchi la ufundi linahitaji baada ya hapo wao ndio wenye uamuzi,” alisema Nyoni aliyebakisha mwaka mmoja ndani ya Simba.

Kocha Zoran alisema wachezaji wote wamefanya vizuri katika maandalizi kama kuna changamoto ni ndogondogo ambazo ni majukumu yake kuzirekebisha.

“Nyoni ni mchezaji mzuri na mzoefu. Anaweza kufanya kazi vizuri anatumika katika nafasi nyingi na ni aina ya wachezaji wa kipekee kutokana na ubora wake alionyesha huku,” alisema Zoran.

Advertisement