Ifahamu Zalan mpinzani wa Yanga Kimataifa

Ifahamu Zalan mpinzani wa Yanga Kimataifa

Muktasari:

  • Zalan ambao ni mabingwa wa Ligi ya Sudan Kusini huenda ikatumia uwanja wa Al Hilal katika mechi zake za kimataifa kutokana Sudan Kusin kutokuwa na uwanja ambao unakidhi vigezo vya CAF.

MABINGWA wa Ligi Kuu Bara Klabu ya Yanga itaanza kampeni zake kwenye hatua za awali Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kucheza na Zalan FC ya Sudan ya Kusini.

Yanga itaanzia ugenini kwa mchezo wa kwanza utakaopigwa kati ya Septemba 9 hadi 11 huku marudiano ikichezwa kati ya Septemba 16 hadi 18.

Mshindi wa jumla baina ya klabu hizo atacheza na mshindi kati ya Mabingwa wa Ligi ya Ethiopia St. George au Al Hilal ya Sudan.

Zalan ambao ni mabingwa wa Ligi ya Sudan Kusini huenda ikatumia uwanja wa Al Hilal katika mechi zake za kimataifa kutokana Sudan Kusin kutokuwa na uwanja ambao unakidhi vigezo vya CAF.

Timu hiyo kupitia ukurasa wao wa Facebook iliwatakia wapinzani wao Yanga mchezo mwema uliochezwa Agosti 13 dhidi ya Simba wa Ngao ya Jamii, ambapo Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-1.


Ilipotokea

Timu hii imetokea katika mji wa Rumbek uliopo katikati mwa nchi ya Sudan Kusini, Zalan imeanzishwa 1999 na wapinzani wao kwenye mashindano Yanga iliyoanzishwa 1935.

Zalan inashiriki kwenye ligi ya Sudan ambayo kutokana na machafuko ya wenyewe kwa wenyewe imekuwa ikisimamiwa chini ya uangalizi wa Serikali.

Ligi ya Mabingwa

Kutokana na msimu bora kwenye Ligi Kuu ya Sudan Kusin timu hiyo ilitwaa ubingwa na kujikatia tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara yake ya kwanza tangu 1999 ilipoanzishwa.


Mafanikio

Ni muda mrefu kwa timu hiyo kushinda ubingwa wa ligi hiyo kwa mara ya kwanza msimu wa 2021/22 na kushinda pia Kombe la Shirikisho 2018.

Zalan ilimaliza nafasi ya pili kwenye kundi B mwaka 2017 ilipofungwa na Gonzaga mabao 4-2 kwenye ligi ya Sudan (the South Sudan national league ‘SSNL’) mjini Juba kabla ya kutwaa ubingwa 2018 kwa kuifunga Gold Star mabao 4-0.

Msimu wa kwanza wa ligi hiyo ulikuwa 2013 ikiwa ni mwaka mmoja baada ya Sudani Kusini kutangaza kupata uhuru wake.