Inonga aumia, awahishwa hospitali

Unaweza kuwa msimu mbaya kwa beki wa Simba, Henock Inonga baada ya kuumia vibaya mguu baada ya kugongana na mshambuliaji wa Coastal Union, Haji Ugando na kuwahishwa hospitali.

Tukio hilo limetokea dakika ya 20 ya mchezo wakati Simba ikicheza dhidi ya Coastal Union ya Tanga katika Uwanja wa Uhuru.

Wakati Inonga akiwania mpira akakutana na Ugando na kusababisha ajali hiyo na mshambuliaji huyo akapewa kadi nyekundu ya moja kwa moja na mwamuzi, Ahmed Arajiga.

Baada ya tukio hilo Inonga alilazimika kutolewa kisha kupakiwa kwenye gari la wagonjwa (Ambulance) kupelekwa hospitali kwa matibabu zaidi.

Kabla ya kutolewa uwanjani hapo wachezaji wa Simba na hata Ugando walionekana kushtushwa na jeraha hilo wakionekana kushika vichwa.

Inonga inakuwa mechi yake ya pili kuumia baada ya ile ya kuwania Ngao ya Jamii dhidi ya Singida Big Stars jijini Tanga na mpaka tukio linatokea leo Simba inaongoza kwa mabao 2-0 yakifungwa na mshambuliaji Jean Baleke.