Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ivory Coast inavyozidi kuikamata Ligi Kuu Bara

Dar es Salaam. Mwanzoni mwa miaka ya 2000, wachezaji kutoka ligi za Uganda na Kenya walionekana kuwa lulu kwa klabu za Tanzania.

Isingekuwa rahisi kwa dirisha la usajili kupita bila kushuhudia kusajiliwa kwa mchezaji kutoka Uganda au Kenya huku kulinganisha na nchi nyingine.

Baadaye upepo ulihamia kwa wachezaji kutoka Rwanda, Nigeria, Burundi, Zambia, DR Congo na Ghana.

Mwaka 2010, Azam FC ilisajili nyota wawili kutoka Ivory Coast ambao walikuwa ni mapacha wa kuzaliwa, mshambuliaji Kipre Tcheche na kiungo Kipre Balou.

Kiwango bora kilichoonyeshwa na mapacha hao ni kama kilizishtua timu zetu na kuzifanya zianze kuitazama Ivory Coast kama miongoni mwa vipaumbele vyao katika kusaka wachezaji wa kuimarisha vikosi vyao.

Hata hivyo hakukuwahi kushuhudiwa ujio wa namba kubwa ya wachezaji kutoka Ivory Coast ambao walijiunga na timu za Tanzania katika dirisha moja la usajili hadi mwaka jana ambapo ilishuhudiwa nyota wanne wakinaswa na timu za Tanzania kutokea Ivory Coast.

Wachezaji hao ni Pacome Zouzoua na Yao Attohoula ambao walijiunga na Yanga pamoja na Aubin Kramo aliyenaswa na Simba ambapo wachezaji hao wote walitokea Asec Mimosas ya Ivory Coast.

Ikumbukwe msimu mmoja nyuma yake, viungo wawili kutoka Ivory walijiunga na timu za Tanzania ambao ni Stephane Aziz Ki ambaye alitua Yanga na Kipre Junior aliyesajiliwa na Azam FC.

Uwezo wa hali ya juu ambao wachezaji hao kutoka Ivory Coast wameuonyesha katika misimu miwili ya hivi karibuni hapana shaka umekuwa chachu ya kuzishawishi kutamani zaidi nyota wanaocheza katika timu mbalimbali zinazoshiriki ligi kuu nchini humo.

Wakati dirisha kubwa la usajili hapa nchini likiendelea, hadi sasa tumeshuhudia usajili wa wachezaji watano ambao wanatoka timu tofauti za Ivory Coast.

Spoti Mikiki inakuletea orodha ya nyota hao watano ambao msimu ujao wataonekana wakiwa na jezi za timu tofauti zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.


Jean Charles Ahoua

Mwaka 2022, Yanga ilimsajili mchezaji bora (MVP) wa Ligi Kuu ya Ivory Coast, msimu wa 2021/2022, Stephane Aziz Ki kutokea Asec Mimosas na mwaka uliofuata ikamnasa nyota bora wa ligi hiyo msimu wa 2022/2023, Pacome Zouzoua.

Katika kuonyesha kuwa hawakubali unyonge, watani wao wa jadi, Simba, mwaka huu nao wamejibu mapigo kwa kumsajili MVP wa Ligi Kuu ya Ivory Coast, Jean Charles Ahoua kutoka Stella Club Abidjan.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22, alionyesha uwezo mkubwa wa kufumania nyavu na kupiga pasi za mwisho ambapo alihusika na mabao 21 akifunga 12 na kupiga pasi tisa zilizozaa mabao.

Ni kiungo mshambuliaji ambaye anatumia miguu yote kwa ufasaha akipendelea zaidi kucheza nyuma ya mshambuliaji wa kati ingawa pia anaweza kutumika katika nafasi zote za winga.

Ahoua kabla ya kujiunga na Stella Club Abidjan, alizitumikia timi za Sewe Sports na LYS Sassandra za hukohuko kwao Ivory Coast.


Anthony Tra Bi Tra

Katika msimu uliopita, Asec Mimosas licha ya kumaliza ikiwa nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Ivory Coast, iliibuka ikiwa kinara katika chati ya timu zilizoruhusu mabao machache zaidi kwenye ligi hiyo inayoshirikisha timu 16 ambapo ilifungwa mabao 15 tu.

Uimara huo wa safu ya ulinzi ya Asec Mimosas ulichangiwa kwa kiasi kikubwa na ubora wa beki wa kati, Anthony Tra Bi Tra mwenye umri wa miaka 25.

Lakini pia aliifanya Asec Mimosas kuwa miongoni mwa timu ngumu kufungika kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo katika mechi 12 ilizocheza iliruhusu nyavu zake kutikiswa mara tatu tu huku ikiishia hatua ya robo fainali.

Beki huyo anayetumia zaidi mguu wa kulia, kimo chake cha mita 1.91 kinamuwezesha kuwa na faida katika kuokoa mipira ya juu pamoja kusaidia mashambulizi pindi timu yake inapofanya mashambulizi ya kona na faulo.

Katika msimu ujao ataonekana akiwa na jezi za Singida Black Stars ambayo imemsajili kwa mkataba wa miaka miwili.


Ande Cirille

Ni beki wa kulia ambaye alikuwa miongoni mwa nyota walioiwezesha Asec Mimosas kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliomalizika ambao alicheza idadi ya mechi nane za mashindano hayo.

Cirille ambaye ana uwezo pia wa kucheza nafasi ya winga hadi anajiunga na Singida Black Stars alikuwa akiitumikia timu ya taifa ya Ivory Coast kwa wachezaji wanaoshiriki Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25, ataitumikia Singida Black Stars kwa muda wa miaka miwili.


Karaboue Chamou

Baada ya kumpoteza Henock Inonga ambaye amejiunga na FAR Rabat ya Morocco, Simba ilisafiri hadi Ivory Coast na kumnasa beki wa kati Karaboue Chamou.

Karaboue ana urefu wa futi 6.2 na yuko vizuri kwenye kucheza mipira ya juu kuzuia na kushambulia.

Mchezaji huyo amesaini mkataba wa miaka miwili ambao utamuweka Simba hadi 2026.

Beki huyo katika msimu uliomalizika aliiwezesha Racing Abidjan kumaliza katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Ivory Coast msimu uliomalizika.


Josaphat Arthur Bada

Uzoefu wa mashindano ya kimataifa ambao ameupata baada ya kucheza mechi 16 za Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika akiwa na kikosi cha Asec Mimosas unamfanya kiungo mshambuliaji Arthur Bada kuwa tegemeo jipya la Singida Black Stars iliyomsajili.

Mchezaji huyo ambaye ana uwezo wa kutumia miguu yote kwa ufasaha, ni mzuri katika kuchezesha timu, kupiga pasi za mwisho na kufunga mabao.

Akiwa na umri wa miaka 21, kiungo huyo mshambuliaji amesaini mkataba wa kuitumikia Singida Black Stars kwa miaka miwili ambao utafikia tamati 2026.