JICHO LA MWEWE: Mugalu sawa, lakini Kagere anatuachia mawazo mbadala

Tuesday August 02 2022
jicho pic
By Edo Kumwembe

NIMESIKIA Simba imeachana na Meddie Kagere. Huyu ni mmoja kati ya mastaa watatu ambao wameondoka katika kambi ya Simba pale Misri na kurejea nchini kwa ajili ya kukamilisha mazungumzo ya kuachana kwa usalama. Wengine ni Thaddeo Lwanga na Chris Mugalu.

Nimejiuliza maswali mengi kuhusu Kagere kuliko wengine lakini baadaye nikajiuliza kidogo kwa Mugalu. Tuanze na Kagere. Viongozi wanaweza kunisuta kwa umri wake kuwa ana miaka 35. Ni umri mkubwa. Kwa hapo naweza kuungana na viongozi pamoja na Kocha Zoran Maki kwa sababu hiyo.

Lakini nawaza, msimu uliopita Kagere hakuwa bora kama ambavyo timu yake inaamini haikuwa na msimu bora. Nini zilikuwa sababu? Kwa sababu ya umri? Hapana. Sio sana. Nadhani Kagere alikosa huduma muhimu kutoka kwa wachezaji muhimu.

Kuondoka kwa Clatous Chama na Luis Miquissone kulimuacha Kagere akikosa huduma ambazo alizitegemea kutoka kwao. Walibaki wachezaji wengi ambao walikuwa na ubinafsi mwingi na wakati mwingine walikosa maarifa katika eneo la mwisho.

Na labda hapohapo tunaweza kujiuliza kama Kagere alikosa mabao mengi ya wazi msimu uliopita. Hapana. Hakukosa mabao mengi. Tatizo ni kwamba hakuangukiwa na nafasi nyingi kama ilivyokuwa zamani.

Washirika wake kina Kibu Dennis na Pape Sakho walionekana kukosa maarifa ya kumtengenezea nafasi. Labda msimu huu ungeweza kujirudia kuwa wake kwa sababu Simba inaonekana kuwasajili wachezaji ambao wanaweza kumsaidia.

Advertisement

Labda Chama atarudi akiwa fiti zaidi na labda kina Augustine Okrah watampikia mabao kwa kadri anavyohitaji. Ni suala la kufikirika hasa ukikikumbuka msimu mmoja kabla ya huu mbovu Kagere alikuwa moto akifukuzana na John Bocco katika mbio za kiatu cha mfungaji bora.

Nipe Kagere muda wowote ule nitamchukua katika timu yangu kwa sababu Kagere anahitaji kutengenezewa nafasi na kufunga. Kagere huwa namfananisha na Amis Tambwe. Sio wazuri sana kwa vurugu za hapa na pale lakini wanajua kuchukua nafasi zao.

Mpaka leo naamini Tambwe anaweza kucheza katika klabu yoyote ya Ligi Kuu na akapitisha mabao 10. Ni suala la kumtengenezea nafasi nyingi kadri unavyoweza na kisha kumuachia jukumu la kufunga tu. Hapo hawezi kukuangusha.

Lakini inawezekana pia Simba imesajili wachezaji walio bora katika eneo la ufungaji na ndio maana haimuhitaji Kagere kwa sasa. Ukweli ni kwamba kuna mambo inabidi yatokee ili kupisha wengine.

Kwanza kabisa ni muhimu kwa wachezaji wote wa kigeni kufanya mambo makubwa katika msimu wa kwanza tu.

Wakati mwingine huwa inatokea tu wachezaji wazuri wakashindwa katika maisha mapya. Kama ambavyo Cesar Manzoki anasubiriwa kwa hamu, inaweza akatokea kuishia kama Juma Balinya wa Yanga. Alitoka Uganda akiwa mfungaji bora lakini mambo yakakataa Tanzania.

Safu mpya ya ushambuliaji ya akina Habib Kyombo na wengineo lazima waingie kwa moto. Vinginevyo labda tufanye Bocco naye arudi upya na asiwe Bocco wa msimu uliopita. Wageni wakifeli klabuni basi kuna mwenyeji wa kuwaonyesha njia.

Ndio maana kuna wakati najikuta nikijiuliza huenda Kagere angeweza kubakia klabuni na kuwa mshambuliaji wa akiba. Lolote linaweza kutokea na unahitaji washambuliaji wazoefu zaidi kikosini kwako.

Kuna mambo mawili tutaweza kuyapima mwishoni mwa msimu ujao. Tutaangalia ni wapi Kagere alikwenda na ni mambo gani alifanya. Lakini pia tutapima kile ambacho kimeletwa na washambuliaji wapya wa Simba katika kikosi chao. Hili ndilo ambalo litahalalisha maamuzi ya sasa.

Kuna uwezekano Kagere akaenda katika klabu isiyo kubwa kama Simba halafu akafunga mabao 10. Hapo tutakuwa tunajiuliza, ingekuaje kama Kagere angecheza nyuma ya wakali wa Simba? labda angeweza kufunga mabao zaidi.

Turudi kwa Mugalu. Maamuzi ya Simba kuachana na Mugalu yanaonekana kuwa sahihi ingawa nayo yanamuachia Mugalu mwenyewe maswali. Kwanza kabisa Mugalu aliutumia muda mwingi akiwa hospitali kuliko uwanjani. Inaeleweka klabu haiwezi kukaa na mtu ambaye analipwa mshahara wake lakini hachezi kila wikiendi.

Lakini kabla Mugalu hajaumia sijui ni kitu gani kilimtokea. Alikuwa mtu haswa katika siku zake za mwanzo Msimbazi. Rafiki yangu mmoja ambaye ni kiongozi pale Msimbazi aliwahi kuniambia Mugalu alikuwa mchanganyiko wa John Bocco na Meddie Kagere.

Nilikiona kitu hiki katika siku za mwanzo za Mugalu Msimbazi. Alifunga mabao magumu na yenye mvuto kuliko ya kina Bocco na Kagere. Ilionekana Simba walikuwa wamepata straika aliyetimia hasa. Lakini taratibu Mugalu akaanza kuwa mbovu.

Hakuwa yule straika ambaye angeweza kufunga kwa nafasi chache zilizomuangukia au kukaa sana na mpira kama ilivyokuwa kawaida yake. Kitu ambacho kilikuwa kinamuweka kando ya Bocco na Kagere katika sifa za washambuliaji.

Alikosa nafasi za wazi ambazo zilikuwa ni kichekesho kwa watazamaji. Pambano lake dhidi ya AS Vita alikosa nafasi za wazi kiasi cha kuomba atolewe uwanjani. Ilikuwa ni nafuu kwake. Wakati huo mashabiki walikuwa hawajapoteza imani naye.

Lakini katika siku hizi za mwishoni Mugalu alionekana kuwa hoi. Hakuwa sawa kiakili na uwezo wake wa kujiamini ulikwenda chini kiasi hata mashabiki walianza kumchoka na mwishowe hawawezi kulaumu hata maamuzi ya uongozi. Anachoweza kufanya kwa sasa ni kwenda kwingine na kurudisha uwezo wake wa kujiamini.

Kama ilivyo kwa Kagere, Mugalu naye nampa nafasi ya kwenda kuibukia kwingineko. Haiwezekani yale mabao aliyokuwa anayafunga Simba katika siku zake za mwanzo yakatoweka ghafla. Labda kuja jambo la nje ya uwanja alikuwa amefanyiwa.

Mwisho wa kila kitu ni kwamba iwe kwa washambuliaji wapya, au kwa washambuliaji walioachwa kama wangebaki, Simba wanahitaji mfungaji bora katika msimu utakaoanza hivi karibuni. Mtu mmoja inabidi aibuke kama George Mpole au Fiston Mayele kuweza kuwapa furaha Wanasimba.

Advertisement