Julio apongeza uthubutu wa vijana wake

Muktasari:

Timu ya Taifa ya vijana (U-20), Ngorongoro Heroes imeanza vibaya mashindano ya Mataifa ya Afrika (Afcon U-20) nchini Mauritania baada ya kukubali kichapo cha mabao 4-0 katika mchezo uliofanyika jana usiku.

Timu ya Taifa ya vijana (U-20), Ngorongoro Heroes imeanza vibaya mashindano ya Mataifa ya Afrika (Afcon U-20) nchini Mauritania baada ya kukubali kichapo cha mabao 4-0 katika mchezo uliofanyika jana usiku.

Mchezo huo ulifanyika katika Uwanja wa Municipal Nouadhibou ulishuhudiwa Watanzania wakianza kwa machungu ya kipigo hicho kizito cha Kundi C.

Mchezo mwingine wa kundi hilo ulikuwa kati ya Gambia dhidi ya Morocco, wakati Gambia ikichapwa bao 1-0, hivyo kufanya Ghana kuongoza kundi hilo wakiwa na uwiano mzuri wa mabao wakati Morocco ikifuata wote wakiwa na pointi tatu.

Tanzania inaburuza mkia na mchezo unaofuata itacheza Jumatatu dhidi ya Morocco, ambayo katika mchezo wa jana ilionyesha uwezo na ushindani mkubwa.

Kocha wa Ngorongoro Heroes, Jamhuri Kihwelo 'Julio' akizungumzia mchezo baada ya mechi kumalizika, aliwapongeza vijana wake kwa kiwango walichokionyesha licha ya kushushiwa kipigo kizito.

"Kwanza niwapongeze kwa kiwango chao, pili tutaendelea kujifunza hata kwenye michezo mingine inayokuja, ili tuone namna gani tunavyotakiwa kuboresha kwa yale tunayojifunza hapa," alisema Kihwelo.

Alisema kiwango ambacho vijana wake wamekionyesha mbele ya mabingwa mara mbili wa mashindano hayo kilikuwa cha kutia matumaini ya kufanya vizuri zaidi hata kama si msimu huu.

Ngorongoro Heroes italazimika kushinda michezo yake miwili ya Kundi C iliyobaki Morocco na Gambia kama itahitaji kutinga katika hatua ya mtoano ya mashindano hayo.