Kibwana hana presha ujio wa Djuma

Muktasari:

BEKI wa kulia wa Yanga, Kibwana Shomary, amesema wala hana presha juu ya taarifa za ujio wa beki Mkongoman Djuma Shaaban, kwa vile yeye ni mchezaji anayejiamini na anaweza kupambania nafasi kikosini.

BEKI wa kulia wa Yanga, Kibwana Shomary, amesema wala hana presha juu ya taarifa za ujio wa beki Mkongoman Djuma Shaaban, kwa vile yeye ni mchezaji anayejiamini na anaweza kupambania nafasi kikosini.

Kibwana aliyesajiliwa na Yanga msimu huu akitokea Mtibwa Sugar, hadi sasa ameonesha kiwango bora akishika rekodi ya kuwa mchezaji wa timu hiyo aliyecheza mechi nyingi zaidi, lakini taarifa za ujio wa Djuma kutoka AS Vita ziliwapa presha mashabiki, huku beki huyo akisema kwa msisitizo;

“Sina taarifa za usajili wa mchezaji huyo, lakini hata kama atakuja sio mbaya kwani akija wote lengo letu litakuwa ni kutimiza malengo ya Yanga.”

“Najikubali na nipo hapa kuitumikia timu hii (Yanga), hivyo nitashirikiana na kila mchezaji aliyepo na atakaekuja kwa lengo la kufanikisha malengo ya timu, kuhusu ushindani wa namba nadhani siwezi kuzungumzia maana hayo ni maamuzi ya kocha ndiye ataamua ampange nani,” aliongeza.

Taarifa za chanzo chetu cha kuaminika ni kwamba Makamu Mwenyekiti wa kamati ya mashindano ya Yanga Mhandisi Hersi Said, yupo nchini Congo DRC akifuatilia taratibu za kumleta Djuma Jangwani. Djuma ni miongoni mwa mabeki bora wa kulia Afrika wanaosifika kwa kukaba na kuanzisha mashambulizi kwa umakini wa hali ya juu, hayo ameyathibitisha akiwa na klabu yake katika mashindano mbalimbali.