Kilichomng’oa Mkude Simba ni hiki hapa

JONAS Mkude ‘Nungunungu’ hakuwamo kwenye kikosi cha Simba tangu alipocheza mara yake ya mwisho nchini Afrika Kusini ambako Wekundu wa Msimbazi walilala 4-0 dhidi ya Kaizer Chiefs katika mechi yao ya kwanza ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Alienguliwa katika maandalizi ya mechi ya marudiano dhidi ya Kaizer iliyopigwa Dar es Salaam ambayo Simba licha ya kushinda 3-0 iling’olewa katika hatua hiyo kwa mara ya pili ndani ya misimu mitatu ya michuano hiyo inayosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Hadi timu zinaenda mapumziko ya kupisha kalenda ya FIFA, Mkude amekosa mechi nne za Simba - ya marudiano dhidi ya Kaizer, ya Kombe la Shirikisho (ASFC) dhidi ya Dodoma Jiji, na mbili za Ligi Kuu Bara dhidi ya Namungo na Ruvu Shooting.

Sababu ya kukosekana kwake inayotajwa ni kosa la nidhamu alilofanya hadi kupewa barua ya kusimamishwa.

Katika miaka mitatu au mitano nyuma ilikuwa ngumu Mkude kukosekana katika kikosi cha Simba bila ya kuwepo sababu maalamu na hata kama ikiwa hivyo lazima mashabiki hujitokeza kumuulizia kuanzia mitandaoni mpaka katika vijiwe vya soka.

Raundi hii imekuwa tofauti kwa Mkude kwani Simba imecheza zaidi ya mechi tano katika nyakati tofauti bila ya kiungo huyo maarufu kama Nungunungu na hakuna tena presha ile ya mashabiki iliyokuwapo awali.

Mwaka 2017, Simba ilikuwa na kiungo, James Kotei ambaye alikuwa akicheza kwa ubora mpaka kocha wa wakati huo, Joseph Omog alikuwa akimuweka nje Mkude jambo ambalo mashabiki hawakukubaliana nalo, walipiga kelele za kutaka acheze na alikuwa hivyo.

Kutokana na jambo hilo Mwanaspoti inakuletea makala inayochambua yaliyochangia Mkude kupoteza nafasi ya kucheza katika kikosi cha Simba na kutokuwa tena midomoni kwa mashabiki ambao walikuwa hawataki kumuona akiwa nje.


NIDHAMU

Mkude amekuwa na matukio mengi ya ukosefu wa nidhamu katika kikosi hicho cha Simba kwani kwa muda usiozidi miezi sita ndani ya msimu huu tayari amesimamishwa mara mbili.

Ukiondoa wakati huu, Mkude amekuwa akiandikwa kuhusu masuala mengi ya ukosefu wa nidhamu na kuna wakati anakutana na adhabu kama sasa na lakini mara nyingine hupita kimya kimya au kusamehewa.

Siku chache kabla ya kuanza kazi kwa Gomes, alimkuta kiungo huyo akiwa katika adhabu aliyopewa na kocha aliyetangulia Sven Vandenbroeck.

Baada ya Gomes kuanza kazi alitoa msamaha juu yake lakini wiki chache zilizopita Mfaransa huyo alimuondoa Mkude katika kikosi cha Simba kutokana na masuala hayo ya ukosefu wa nidhamu.

Ukweli usiopingika ni kwamba hakuna anayefurahishwa na matukio ya mara kwa mara ya utovu wa nidhamu wa Mkude na iko wazi hiyo ni moja ya sababu zilizomfanya Nungunungu kupoteza namba kikosini.


TADDEO LWANGA

Katika dirisha dogo msimu huu Simba walimsajili, Lwanga kama mchezaji huru akitokea nchini Misri na mwanzo alipokuwa akitumikia kikosi hicho alionekana mchezaji wa daraja la kawaida.

Lakini baada ya kuonyesha kiwango bora, Lwanga amekuwa mchezaji wa kutegemewa katika nafasi ya kiungo mkabaji.

Awali Mkude alikuwa na uhakika wa kucheza katika nafasi hiyo lakini tangu kuingia kwa Lwanga imekuwa kinyume kwani Mganda huyo amekuwa anafunika katika kila mechi.

Ujio wa Lwanga katika kikosi cha Simba umezima ufalme wa Mkude katika nafasi ya kiungo mkabaji na kuonekana ni mchezaji wa kawaida tu.

Upepo umebadilika. Mfalme kwenye kiungo cha ulinzi cha Simba sasa ni Lwanga. Hii ni taa nyekundu kwa Nungunungu.


MATOKEO

Suala lingine ambalo limechangia Mkude kupoteza nafasi ya kucheza katika kikosi cha Simba ni ubora wa matokeo mazuri mfululizo ambayo wanayapata wakati huu katika mashindano yote.

Pengine Simba isingekuwa inapata matokeo ya ushindi mfululizo labda mashabiki wa timu hiyo wangeibuka na kumtaka kumuona kiungo wao huyo akicheza, lakini sio kwa dozi hizi za 3G wanazotoa.


MASHABIKI

Kipindi cha nyuma Mkude alipokosekana kikosini mashabiki wa timu hiyo walikuwa huwambii kitu, walikuja juu wakishinikiza achezeshwe.

Jambo hili liliwaweka njiapanda hata viongozi wa klabu hiyo kwa sababu mchezaji anapokosea anatakiwa kuadhibiwa bila ya kujali umuhimu wake kikosini ili kuondoa makundi, lakini hapohapo wakawekwa katika wakati mgumu kutokana na presha ya mashabiki.

Wengi waliamini kwamba hali hii ilichangia kumfanya Mkude ajisahau.


MFUMO

Suala lingine ambalo limechangia Mkude kupoteza namba katika kikosi cha Simba ni mifumo ambayo imetumiwa na makocha wawili waliopita.

Sven Vandenbroeck na Didier Gomes wote wanapenda kutumia zaidi (4-2-3-1), katika eneo la Mkude ambapo kunakuwa na viungo wawili wakabaji wanaweza kutumika wengine.

Mkude amezidi kuwa na wakati mgumu katika mfumo wa 4-1-3-2, ambao Gomes kuna nyakati huutumia na huanza na kiungo mmoja wa ukabaji ambaye ni Lwanga.


UBORA WA WACHEZAJI

Katika nyakati tofauti Simba wamekuwa wanasajili wachezaji kwenye maeneo mbalimbali ili kuboresha na kuongeza nguvu kwenye kikosi chao.

Jambo hilo limefanya Simba kuwa wachezaji wengi bora kwenye nafasi zote kiasi kwamba akikosekana mmoja, mwingine anaweza kuziba nafasi kwa ubora.

Tangu Mkude amekutana na changamoto hiyo ya kusimamishwa nafasi yake amecheza Mzamiru Yassin na Erasto Nyoni ambao wote wawili kila mmoja kwa nafasi yake amekuwa imara na kuzima ufalme wa Mkude.


PESA NYINGI

Katika kipindi cha miaka mitatu ambayo Simba wamechukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara mfululizo na kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mara mbili, wachezaji na makocha wamekuwa na mafanikio makubwa ikiwamo kuvuta mkwanja wa maana.

Katika wakati huu si jambo la kushangaza mchezaji ambaye anacheza katika kikosi cha kwanza Simba kupata posho Dola za Kimarekani 5,000, ambayo kwa pesa ya Kibongo ni zaidi ya Sh11 milioni.

Posho hizo zimekuwa nyingi kwa wachezaji wa Simba ambao huingiza kiasi kikubwa cha pesa na kama unafanyia malengo utakuwa umefika mbali kimaisha.

Huenda Mkude ameridhika na mkwanja alioingiza.