Kinachoibeba Yanga hiki hapa

Muktasari:

  • Yanga inaongoza Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na pointi 65 huku Simba ambao ndio wapo nafasi ya pili kwenye msimamo wamekusanya pointi 57 na inaongoza kundi D kwenye Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kukusanya pointi 10 sawa na US Monastir utofauti ukiwa ni mabao ya kufunga na kufungwa.

Dar es Saalam. Rais wa Yanga, Hersi Said ametaja siri ya mafanikio waliyoyapata hivi karibuni ikiwa ni pamoja na kutinga hatua ya robo fainali Kombe la Shirikisho Afrika na kuongoza ligi kwa kumuacha mpinzani pointi nane kuwa ni ubora wa kikosi, benchi la ufundi na umoja uliopo baina ya timu na uongozi.

Yanga inaongoza Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na pointi 65 huku Simba ambao ndio wapo nafasi ya pili kwenye msimamo wamekusanya pointi 57 na inaongoza kundi D kwenye Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kukusanya pointi 10 sawa na US Monastir utofauti ukiwa ni mabao ya kufunga na kufungwa.

Hersi alisema mafanikio waliyoyapata hayajaja kwa njia rahisi wamepambana hadi kufikia hapo wameputa kwenye nyakati ngumu lakini umoja wao na jitihada za wachezaji na benchi la ufundi kitu kilichowafanya wafike kwenye nyakati hiyo waliyopo.

"Mwanzoni wa msimu malengo kwenye mashindano ya kimataifa ni kufika hatua ya makundi lakini timu imefanikiwa kuvuka hadi hatua ya robo fainali ni jambo zuri kwetu na sasa timekuwa na malengo mengine makubwa," alisema Hersi na kuongeza;

"Hii ni kutokana na ubora wa wachezaji, benchi la ufundi na umoja uliopo baina ya timu na uongozi sasa tunalenga kufika ghatua ya nusu na hatimaye kucheza mechi ya ubingwa haya yote yanawezekana kutokana na ubora wa kikosi tulichonacho na uchu wa mafanikio uliopo kutoka kwa wachezaji na benchi la ufundi."

Alisema ili kuwa bora zaidi wanahitaji kufanya uwekezaji mkubwa kwenye usajili na kuongeza nguvu ya kuwaweka wachezaji katika hali nzuri kwa kuwapa mahitaji yao kwa wakati akisisitiza kuwa kipindi cha wachezaji kufurahia kupigiwa makofi kimeshapita sasa wanataka kupata kitu ili kuendesha maisha yao na familia.

"Wachezaji wameshavuka kipindi cha kufurahia kupigiwa makofi kutokana na mazuru wanayoyafanya wanahitaji fedha hivyo motiosha iliyowekwa na rais kwa kununua bao pia sisi kama viongozi tunawapa motisha na ndio mafanikio mazuri tunayoyaona," alisema Injinia huyo na kuongeza;

"Tumeshapata nafasi ya kutinga hatua ya robo fainali tukiwa na mchezo mmoja ambayo tunaenda kucheza nje ya Tanzania ni mchezo muhimu kwetu tunaupa kipaumbele tunahitaji matokeo mazuri ya ushindi ili kuendelea kuongoza kundi."

Hersi alisema matokeo ya ushindi dhidi ya TP Mazembe yanafaida kubwa kwao kwanza wanakutana na timu ambazo hazitakuwa na ushindani mkubwa na watapata fursa ya kuanzia ugenini mchezo wa hatua ya robo fainali ambayo ni faida.