Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kipigo cha City kilivyobeba rekodi kibao

Muktasari:

  • Kipigo hicho kimeifanya Man City kuwa na mfululizo wa matokeo mabaya na kuweka rekodi kibao huku ikiiacha timu hiyo na sintofahamu katika kutetea ubingwa wake wa Premier

Manchester, England. Juzi Jumamosi Manchester City ilikwenda mapumziko ikiwa mbele kwa bao 1-0 dhidi ya Brighton & Hove Albion katika mchezo wa Premier League lakini mwisho wakapoteza kwa mabao 2-1.

Kipigo hicho kimeifanya Man City kuwa na mfululizo wa matokeo mabaya na kuweka rekodi kibao huku ikiiacha timu hiyo na sintofahamu katika kutetea ubingwa wake wa Premier.

Man City ambayo imetawala Premier kwa misimu minne mfululizo 2020–21, 2021–22, 2022–23 na 2023–24 ikibeba ubingwa, hivi sasa mambo yanaonekana kuwa magumu na kipigo cha juzi kimewafanya kuachwa pointi tano na vinara Liverpool.

Mabingwa hao watetezi ligi ikirejea Novemba 23 mwaka huu baada ya kupisha mapumziko ya kimataifa, watakuwa na mchezo wa Premier League ambapo watakutana na Spurs ambao walianza na mfululizo mbaya wa vipigo.

Kupitia kipigo cha juzi ilichopata Man City mbele ya Brighton, hizi ndizo rekodi zilizowekwa.

Baada ya kupoteza kwa Tottenham Hotspur katika Kombe la EFL, kisha mbele ya Bournemouth kunako Premier League na Sporting Lisbon ndani ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, kipigo cha juzi kilikuwa cha nne mfululizo kwa Man City kwenye mashindano yote. Hiyo ikiwa ni rekodi ya kwanza.

Rekodi ya pili inaonyesha kwamba, mara ya mwisho kwa City kupata mfululizo kama huu ilikuwa msimu wa 2005/06, walipofungwa mechi tatu za mwisho za msimu dhidi ya Fulham, Arsenal na Blackburn Rovers, kisha kupoteza tena mchezo wao wa ufunguzi wa msimu wa 2006/07. Hizi zote zilikuwa mechi za Premier League, chini ya usimamizi wa Kocha Stuart Pearce. Imepita takribani miaka 18 kutokea tena.

Rekodi ya tatu inamuhusu Kocha Pep Guardiola ambaye amepata kipigo cha mechi nne mfululizo kwa mara ya kwanza katika taaluma yake ya ukocha, kwa kuwa hajawahi kuona mfululizo kama huu akiwa na City, Bayern Munich au Barcelona, isipokuwa kwa changamoto ya mikwaju ya penalti.

Hii ni mara ya nne pekee kwa Guardiola kupoteza mechi mbili mfululizo katika Premier League, ikiwa tayari ameshuhudiwa hilo dhidi ya Leicester City na Chelsea mnamo Desemba 2016, Crystal Palace na Leicester mnamo Desemba 2018, kisha dhidi ya Wolverhampton Wanderers na Arsenal kati ya Septemba na Oktoba 2023.


Ikumbukwe kwamba, kabla ya kufungwa na Bournemouth mnamo Novemba 2, 2024, City walikuwa katika mfululizo wa kucheza mechi 32 bila ya kupoteza katika Premier League, rekodi iliyodumu kwa takribani miezi 11 baada ya kipigo cha 1-0 dhidi ya Aston Villa mnamo Desemba 6, 2023.

Wakati Guardiola akiweka rekodi hiyo mbovu katika maisha yake ya kufundisha soka, pia straika wa Man City, Erling Haaland kwa mara ya kwanza alishuhudia timu yake hiyo ikipoteza mchezo wakati yeye akifunga bao.

Rekodi zinaonyesha kwamba, Haaland katika mechi 46 zilizopita za Premier kabla ya kukutana na kipigo cha Brighton, hakuwahi kuondoka uwanjani timu yake ikiwa imepoteza pindi yeye anapofunga bao. Hiyo ilitokea katika mechi 46 mfululizo Man City ikishinda 40 na sare 6.

Brighton wamekuwa wababe tena wa City kwani awali ilikuwa ndio timu ya mwisho ya Premier League kushinda dhidi yao wakati City ikiongoza hadi mapumziko na mwisho wa mchezo kupoteza. Walifanya hivyo mwaka 2021 kwenye Uwanja wa Amex nyumbani kwa Brighton.

5 ZIJAZO ZA MAN CITY:

Novemba 23, 2024: Man City vs Tottenham (Premier League)

Novemba 26, 2024: Man City vs Feyenoord (UEFA)

Desemba 1, 2024: Liverpool vs Man City (Premier League)

Desemba 4, 2024: Man City vs Nottingham Forest (Premier League)

Desemba 7, 2024: Crystal Palace vs Man City (Premier League)