Kisa mabadiliko Simba, Mo Dewji atema nyongo

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya klabu ya Simba, Mohammed 'Mo' Dewji ameamua kuvunja ukimya kuhusu mchakato wa mabadiliko ya uendeshaji wa klabu.

Mo Dewji kupitia mtandao wake wa kijamii wa Twitter amebainisha kinachokwamisha mchakato huo wakati yeye yupo tayari kufuata taratibu zote.

Katika ukurasa huo, Mo Dewji ameandika; "Nasikitika kwamba tunafanya vikao na FCC na kukubaliana kumaliza halafu tunapata barua za kuanza upya.

"Labda wabunge wapo sahihi kwamba kuna njama za kutukwamisha, hii ni mbaya sana, mipango yetu mikubwa inacheleweshwa,".

Mchakato wa mabadiliko ya uendeshaji wa klabu hiyo ambao unampa mwekezaji asilimia 49 ya hisa na wanachama asilimia 51 huko kwenye Tume ya Ushindani wa Biashara (FCC).

Awali FCC iliipa klabu ya Simba notisi ya siku 21 kuchunguza mchakato huo.

Ingawa pia, FCC iliwahi kutoa taarifa na kubainisha moja ya vitu ilivyohitaji kwenye mchakato huo ni ufafanuzi juu ya kiasi halisi ambacho mwekezaji, Mo Dewji anatakiwa kuwekeza ili kuondokana na mkanganyiko uliokuepo.

Taarifa hiyo ambayo iliyoonyesha imetoka kwa mkurugenzi ilieleza kwamba pamoja na mambo kadha wa kadha ambayo hayakukamilika, tume ilitaka ufafanuzi wa kiasi halisi ambacho mwekezaji anatakiwa kuwekeza kwani kilichopo kwenye makubaliano ya awali ni tofauti na kinachotamkwa kwenye vyombo vya habari.

Badae Simba iliweka wazi kiasi ambacho kipo kwenye makubaliano kuwa ni Sh 19.6 Bilioni huku ikibainisha mwekezaji ameamua atalipa zaidi ya kiwango kilichoainishwa kwenye makubaliano ili ifike bilioni 20.
Simba walifafanua kwamba walipeleka suala lao FCC Julai 23, 2020 kwa lengo la kutimiza masharti ya kukamilisha mchakato na iliendelea kuwa na mawasiliano chanya na FCC hadi Oktoba 16, 2020 ilifanya kikao baina ya pande hizo mbili kwenye ofisi za Simba kwa lengo la kukamilisha mchakato.

Siku chache baada ya kikao, Simba ilieleza kupokea barua yenye tarehe ya nyuma yaani Oktoba 13, 2020 iliyowataarifu wadaawa wote wa mabadiliko ya uendesha wa klabu ya Simba juu ya uamuzi wa FCC kusitisha mchakato wa mabadiliko ya uendeshaji ili kupitia masuala mbalimbali ya kisheria na kikanuni yaliyojitokeza wakati wa mchakato.

Barua hiyo iliarifu Simba kwamba FCC itawajulisha wadaawa kuanza tena kwa mchakato huo wa kupitia maombi ya klabu ya kubadili mfumo na siku tisa baadae, Oktoba 22, 2020 klabu ilipokea barua kutoka FCC ikiwataka kuwasilisha taarifa za ziada zinazohitajika kwenye kuidhinisha maombi ya klabu na kubadili mfumo wa uendeshaji.

Katika mtandao wake wa kijamii, Mo Dewji ameeleza kusikitishwa kukaa vikao na FCC  na kukubaliana kumaliza halafu wanapata barua za kuanza upya.