Kisa Yanga, Zoran ajifungia kwa saa 2

Muktasari:

  • SIKU mbili tu kabla ya kuvaana na Yanga katika mechi ya Ngao ya Jamii, benchi la ufundi la Simba chini ya Kocha Zoran Maki limejifungia na mastaa wa timu hiyo kwa ajili ya kuwekana sawa ili kuhakikisha keshokutwa, Jumamosi wanatoka na ushindi mbele ya watani zao.

SIKU mbili tu kabla ya kuvaana na Yanga katika mechi ya Ngao ya Jamii, benchi la ufundi la Simba chini ya Kocha Zoran Maki limejifungia na mastaa wa timu hiyo kwa ajili ya kuwekana sawa ili kuhakikisha keshokutwa, Jumamosi wanatoka na ushindi mbele ya watani zao.

Simba na Yanga zitavaana kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa katika mechi ya kuzindua msimu mpya wa Ligi Kuu Bara 2022-2023, huku Kocha Zoran ikiwa ni mara yake ya kwanza kuiongoza timu hiyo mbele ya Yanga jambo lililomfanya aanze mapema tu kujipanga.

Katika kuhakikisha inapata matokeo mazuri ya ushindi kwenye mchezo huo, wachezaji na benchi la ufundi Simba walifanya kikao kizito cha karibu saa mbili ili kuhakikisha wanaweka mipango mikakati mizuri kwa lengo la kutimiza malengo

Kocha Zoran alisema lengo la kukutana na wachezaji wake wote ni kwa kuwa hakuwa amepata muda wa kuwa nao pamoja kwani wakati yupo Misri kwa ajili ya maandalizi ya msimu (pre-season) kuna wengine walikosekana kwa sababu mbalimbali.

Zoran alisema katika kikosi chake aliwaeleza wachezaji waione Simba kuwa ni timu kubwa inayohitaji kufanya vizuri msimu ujao kwa kuchukua mataji, na wanatakiwa kulifanya hilo katika mchezo wa kwanza wa Jumamosi dhidi ya Yanga.

Alisema katika kujadiliana kwenye kikao wanafahamu utakuwa ni mchezo mgumu, lakini kila mchezaji kwa nafasi yake anatakiwa kupambana ili kuhakikisha ushindi unapatikana wachukue taji la kwanza msimu ujao.

“Nimeongoza timu nyingi kwenye mechi za dabi kama hii. Hakuna hata moja iliyowahi kuwa rahisi, ila kutokana na maandalizi ambayo tumefanya huko nyuma na tunayoendelea kufanya wakati huu na uwajibikaji wa wachezaji wangu nina imani tutakwenda kupata ushindi,” alisema Zoran.

“Baada ya kumaliza kujadili mchezo wa Yanga tumekubaliana na wachezaji kila mmoja kuipambania timu, kujitoa katika majukumu ya nafasi yake ili kuhakikisha tunashinda kila mechi katika mashindano yote.

“Tunahitaji kushinda vikombe vitatu ambavyo msimu uliopita tulivipoteza vya Ngao ya Jamii, Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) na Ligi Kuu Bara - hayo yote hayawezekani bila ya wachezaji kujitoa ili kushinda kila mechi iliyopo mbele yetu.

“Ligi ya Mabingwa Afrika tutacheza hatua mbili za mwanzo tunahitaji kwanza kufika hatua ya makundi na baada ya hapo kuweka hesabu nzuri dhidi ya wapinzani wetu ili kufika hatua ya mbele kama malengo yalivyo.”

Katika hatua nyingine, Zoran alisema upande wa benchi la ufundi kwa kushirikiana pamoja wamewafuatilia wapinzani wao katika vyanzo mbalimbali na vile ambavyo wamevipata wanavifanyia kazi kwenye mazoezi.

“Tunafanya yote haya ili kuhakikisha tunashinda mechi hiyo kwani ushindi utaongeza ari na morari kwa wachezaji na hata mashabiki kuelekea msimu ujao kwani tutakuwa tumeanza kwa mafanikio,” alisema Zoran anayekwenda kuiongoza Simba katika dabi yake ya kwanza.


KIBU, OKWA

Mfungaji bora wa Simba msimu uliopita, Kibu Denis alisema hakuna mechi dhidi ya Yanga iliyowahi kuwa rahisi na ameligundua hilo tangu alipokuwa anacheza katika kikosi cha Mbeya City.

Kibu alisema wachezaji wa Simba wako katika hali nzuri na morali ili kuhakikisha wanakwenda kupambana kupata ushindi na kuchukua taji hilo ambalo msimu uliopita walishindwa kulipata.

“Msimu huu timu yetu ina mabadiliko makubwa kuanzia wachezaji wapya hadi benchi la ufundi. Maandalizi yalikuwa mazuri kule Misri kwani ukiangalia wachezaji wote wapo tayari na wana hamu ya kucheza mechi hiyo,” alisema Kibu aliyemaliza na mabao manane msimu uliopita.

Akizungumzia mechi iliyopita dhidi ya St George katika tamasha la Simba Day, Kibu alisema: “Binafsi sikutegemea kama naweza kupewa nafasi ya kuanza katika mechi iliyopita kutokana na kwamba sikuwepo Misri, ila nina imani ushindani wa kuwania nafasi ya kucheza katika kikosi chetu .. nitakuwa nafanya vizuri katika kila mechi zaidi ya mechi ile ya St George.

“Simba ni timu kubwa katika kuonyesha ukubwa wake na siyo jambo lingine zaidi ya mataji na wachezaji, kila mmoja anafahamu hilo, tumeweka ahadi na tunakwenda kupambana ili kuchukua mataji msimu huu.”

Kwa upande wake straika mpya, Nelson Okwa alisema ametua Simba ili kuongeza makali ya kikosi hicho kuwania kuchukua mataji na kwamba anaendelea na mazoezi ya timu na yake binafsi ili kufanya vizuri na kutoa mchango wake ndani ya chama lao.