Lazima mpigwe

Lazima mpigwe

Muktasari:

  • KUANZIA mtandaoni hadi vijiweni kwa sasa ni tambo tu za watani, kila upande ukivutia kwake ukitamba kuwa lazima mtu apigwe kesho wakati Simba na Yanga zitakapokutana kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa. Makocha wa timu zote wamewapa dozi nene nyota wao kabla ya mchezo huo.

KUANZIA mtandaoni hadi vijiweni kwa sasa ni tambo tu za watani, kila upande ukivutia kwake ukitamba kuwa lazima mtu apigwe kesho wakati Simba na Yanga zitakapokutana kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa. Makocha wa timu zote wamewapa dozi nene nyota wao kabla ya mchezo huo.

Mechi hiyo itapigwa kuanzia saa 11:00 jioni na ni Ngao ya Jamii, huku kila mmoja akitambia kikosi. Tuanzie pale Jangwani. Juzi usiku mabosi wa klabu hiyo walimleta aliyekuwa Kocha Mkuu wao, Cedric Kaze na fasta jana wakamsainisha kama Kocha Msaidizi ili kumsaidia Nasreddine Nabi aliyechekelea kuletewa msaidizi huyo akiamini akishirikiana naye na majembe yake yaliyokamilika kesho, anaona kabisa anapindua meza kibabe baada ya Julai 25 kuaibika kule Kigoma katika fainali ya Kombe la ASFC.

Kocha Kaze alitemeshwa kibarua Machi 7, mara baada ya Yanga kulazimishwa sare ya 1-1 na Polisi Tanzania katika mechi ya Ligi Kuu na nafasi yake kuja kujazwa na Nabi na juzi alitua nchini kabla ya jana kusainishwa mkataba na kwenda kambini Avic, Kigamboni kutambulishwa kwa wachezaji.

Kaze amerejea Yanga baada ya siku 199 na ujio wake umemfanya Nabi kuchekelea akiamini kwamba kazi itakuwa rahisi wakati msimu mpya akieleza alimpitisha baada ya kupitia wasifu wa makocha kadhaa akiwemo Mwinyi Zahera. “Namkaribisha ndio ni kocha mzuri anajua majukumu ambayo tunakwenda kushirikiana naye hapa, tulifanya maamuzi kwa pamoja na viongozi wa klabu na jukumu letu sasa ni kwenda kuipa mafanikio klabu hii,” alisema Nabi.

Ujio huo mpya wa Kaze, umepokewa pia kwa mikono miwili na baadhi ya wadau wa soka nchini akiamini unaenda kuijenga Yanga kwenye eneo la ufundi kama ilivyokuwa kwa watani wao, Simba waliomuongezea Thierry Hitimana.

MASTAA WAMPA MZUKA

Akizungumza na Mwanaspoti Nabi alisema ameridhishwa na ubora wa wachezaji hao akiwamo Djuma Shaban, Fiston Mayele, Khalid Aucho, David Bryson na wengine waliokuwa na matatizo mbalimbali yaliyowazuia kucheza mechi zilizowang’oa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Rivers United ya Nigeria. Djuma ameliambia Mwanaspoti Jijini Dar es Salaam kwamba ; “Hii ni mechi ya heshima na ndio imebeba uelekeo wa msimu wetu mpya.”

Kocha Nabi mwenye uraia wa Tunisia na Ubelgiji, alisema hakuna matokeo wanayoyahitaji zaidi ya ushindi ambapo amewaambia wachezaji wake haitakuwa freshi kwao kupoteza mechi ya tatu mbele ya mashabiki wao.

“Nimeona viwango vyao mechi imenipa kipimo cha kuona wapo wachezaji ambao wanaweza kutusaidia katika huu mchezo,hata wakati tunawaacha tuliwaachia kitu cha kufanya na wanaonekana walifuata,” alisema Nabi na kuongeza;

“Wameonyesha kiwango kizuri nafikiri sasa kazi inayokwenda kufanyika ni kuwaunganisha na wenzao kisha tuchague timu moja kuna uwezekano mkubwa wa kuwa na mabadiliko ndio ila ni mapema kusema yatakuwa eneo gani.

“Najua ugumu wa hii mechi kuna mambo ambayo yanatupa umuhimu wa pekee katika mechi hii dhidi ya Simba, tunawaheshimu na nafahamu kwamba itakuwa mechi ngumu lakini nimewaambia wachezaji wakumbuke tulipoteza kombe mbele yao lakini pia tumepoteza mechi mbili kuba mbele ya mashabiki wetu hapa nyumbani hii ni sehemu ya kubadilisha hilo.


GOMES MBINU MPYA

Msimbazi nako katika kuonekana hawataki kutibua furaha ya mashabiki wao baada ya kubeba Kombe la ASFC kwa kuifumua Yanga pale Kigoma, Kocha Mkuu, Didier Gomes na wasaidizi wake wamekuja na mbinu mpya.

Gomes na wenzake wameiangalia Yanga kwenye mechi zao zilizopita na kubaini mambo matatu ambayo kama watayafanyia kazi, basi watapiga mtu Kwa Mkapa, baada ya kushindwa kufanya hiyo katika mechi za Ligi Kuu Bara msimu uliopita ya kwanza ikitoka sare ya 1-1 na nyingine ya marudiano kupasuka 1-0.

Mambo matatu ambayo Simba imebaini ni makosa wanayoyafanya mara kwa mara katika beki yake, ubora wa safu yao ya kiungo na jinsi wanavyoshambulia katika mbinu tofauti na kocha Gomes akaamua kuyahamishia uwanjani kwa wachezaji wake mazoezini kwa muda wa siku tatu mfululizo.

Mbali na kuwapa kazi mabeki wake kukaba kwa nafasi, lakini aliwapa mbinu mabeki wake wa pembeni, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na Shomary Kapombe kupandisha mashambulizi ili kusaidia nafasi za kufunga kwa wachezaji wenzao na mabeki hao walifanya kwa umakini mkubwa mazoezini kule Bunju.

Tshabalala na Kapombe baada ya kupata mipira walikuwa wakitakiwa kupiga pasi na krosi za maana kwa viungo na washambuliaji ambao kazi yao ilikuwa kutengeneza shambulizi la maana na kufunga.

Kazi hiyo aliifanya pia kwa mabeki wake wa kati, Joash Onyango, Pascal Wawa na Hennock Inonga waliokuwa na kazi ya kuzuia mashambulizi katika maeneo yote na kusaidia viungo kupeleka mipira mbele.

Baada ya kumalizana na mabeki hao Gomes alihamia kwa viungo na kuwapa majukumu mawili, Sadio Kanoute, Taddeo Lwanga, Rally Bwalya, Erasto Nyoni, Mzamiru Yassin na Abdulsamad Kassim ambao walitakiwa kukaba na wanapopata mpira walitakiwa kuumiliki kwa muda mrefu bila kupoteza.

Mazoezi hayo ya mbinu yalikwenda kumalizika kwa washambuliaji, Mugalu, Kibu, John Bocco, Meddie Kagere, Yusuph Mhilu, Ibrahim Ajibu na Hassan Dilunga ambao kazi yao ilikuwa ni kufunga mabao kutokana na nafasi ambavyo itakuja.

Washambuliaji hao walitakiwa kufunga mabao kutokana na mipira ambayo itatoka katikati kwa viungo au pembeni kwa mawinga na mabeki ambao kuna muda walipiga pasi na krosi.


WASIKIE WADAU

Nyota wa zamani wa Simba, Abdallah Kibadeni alisema; “Maandalizi hayo ya Simba kama yatakuwa sahihi kulingana na ambavyo wamewaona Yanga yanaweza kuwasaidia kupata ushindi lakini kama ikiwatofauti wanaweza kujikuta wanapoteza.” Kiungo wa zamani wa Simba, Henry Joseph alisema; “Ngumu kutabiri timu gani itapata ushindi kwani kila moja haitaki kupoteza kwahiyo hapa jukumu litakuwa kwa wachezaji kuyafanya yale waliyopatiwa na makocha wao pamoja na uwezo binafsi ili kushinda mchezo huo. “

Nyota wa zamani wa Bandari, Jemedari Said alisema;”Sina shaka na kurejea Kaze, cha kujiuliza na viongozi wanatakiwa kukiweka wazi kama ni kukiri walikosea walipomuondoa kwa kuwa alikuwa kashinda mechi 14 sare nane na kupoteza mchezo mmoja, mimi niliamini aliondolewa kwa mihemko ila takwimu zilikuwa zinambeba.”


Imeandikwa na Khatimu Naheka, Thobias Sebastian na Clezencia Tryphone.