Lyanga atuma salamu, akitaka kiatu cha dhahabu

MSHAMBULIAJI wa JKT Tanzania Danny Lyanga ametuma salama kwa timu watakazokutana nazo kwenye michezo ijayo ya Ligi huku akitaka zijipange kikamilifu kumkabili.

Lyanga amesema hayo juzi Ijumaa baada ya kuisaidia timu yake kupata ushindi wa bao 3-1 nyumbani dhidi ya Mwadui mchezo ambao Lyanga alifunga mabao mawili kati ya matatu waliyoyapata akifunga bao la kwanza dakika ya 11 na lile la pili dakika ya 13.

"Kwa sasa timu yetu ipo chini, bado tunapambana ili kutoka huku na kusogea juu.  mechi zijazo zitakuwa za muhimu kwetu hivyo lazima tupambane ili tupate alama tatu muhimu.

"Nimefikisha mabao nane katika mbio za kuwania kiatu cha mfungaji bora, ndoto yangu kubwa ni kuchukua kiatu cha dhahabu na kwa kufuata mbinu za kocha na juhudi zangu naamini hadi msimu unamalizika nitakua naongoza kwa wafungaji," amesema Lyanga.

Katika mabao nane aliyonayo Lyanga, manne amewafunga Mwadui katika mechi mbili za ligi walizokutana msimu huu. Pia katika mbio za kuwania kiatu hicho juu yake wakiwepo Prince Dube wa Azam mwenye mabao 10 na John Bocco na Meddie Kagere wa Simba wenye mabao tisa kwa kila mmoja.

JKT Tanzania ipo nafasi ya 12 kwenye msimamo wa Ligi Kuu baada ya kucheza jumla ya mechi 25 na kufikisha alama 27.