Madrid, mkongwe pekee Ulaya dhidi ya matajiri wa Qatar, Abu Dhabi, Russia

Thursday April 15 2021
madrid 3

Paris, Ufaransa (AFP). Chama cha Soka Ulaya (UEFA) kinatarajia kutangaza mabadiliko makubwa ya muundo wa Ligi ya mabingwa wiki ijayo, lakini timu zilizofuzu kucheza nusu fainali msimu huu zinathibitisha kiwango cha jinsi klabu kubwa zilivyokwishafanya mageuzi katika kipindi cha miaka kumi iliyopita.


Real Madrid imefuzu kucheza nusu fainali pamoja na Chelsea, inayomilikiwa na tajiri wa Russia, PSG inayomilikiwa na matajiri wa Qatar, na Manchester City, inayomilikiwa na familia ya kifalme ya Abu Dhabi.


City imevuka hatua ya robo fainali kwa mara ya kwanza tangu ianze kufundishwa na Pep Guardiola mwaka 2016 na zawadi yake imekuwa ni kukutana na Paris Saint-Germain (PSG) katika nusu fainali.


Ni mechi kubwa ya aina yake na ya nadra baina ya timu hizo mbili ambazo zimeongoza mageuzi ya soka barani Ulaya chini ya umiliki wa matajiri kutoka Abu Dhabi na Qatar.


Utajiri wa mashirika yanayomilikiwa na serikali za nchi za Mashariki ya kati umeziwezesha PSG na City kuziondoa klabu kubwa kongwe kama ambavyo Chelsea ilifanya baada ya kununuliwa na bilionea kutoka Russia, Roman Abramovich mwaka 2003.


Klabu hiyo ya London pia imefuzu kucheza nusu fainali, ambako itakutana na Real Madrid, timu ambayo imeshatwaa ubingwa wa Ulaya mara 13 na ambayo ndiyo kigogo wa zamani pekee aliyesalia katika hatua hizo za mwisho za Ligi ya Mabingwa.

Advertisement


Real imetawala Ligi ya Mabingwa katika kipindi cha zaidi ya miaka kumi iliyopita pamoja na Barcelona na Bayern Munich. Kwa ujumla, timu hizo tatu zimetwaa ubingwa wa Ulaya mara tisa kati ya 12 ya michuano iliyopita.


Madrid ililingana na Barcelona kwa kuwa klabu yenye mapato makubwa duniani msimu uliopita, kwa mujibu wa uchambuzi uliofanywa na taasisi ya Deloitte, na bado kuna hoja kuwa kwa sasa haina nafasi ya kutwaa ubingwa kulinganisha na timu nyingine tatu zilizofika nusu fainali.


Zinedine Zidane amefanya maajabu katika timu ambayo miezi mitatu iliyopita ilikuwa ikionekana imechoka na inahitaji kufumuliwa, huku uti wao wa mgongo ukiwa na wachezaji wawili wenye umri wa miaka 35, Sergio Ramos na kiungo Luka Modric, pamoja na mshambuliaji Karim Benzema mwenye miaka 33.


"Najivunia kile tunachofanya, lakini bado hatushinda chochote," alisema Zidane jana Jumatano.

Chelsea yavuna ilichowekeza
Licha ya kuiondoa Liverpool katika robo fainali, Real imedhoofishwa na uwekezaji wa dola 688 milioni za Kimarekani (sawa na Sh1.59 trilioni za Kitanzania) kuukarabati uwanja wake, wakati janga la virusi vya corona limepunguza mapato yake.

madrid 1


Chelsea, wakati huohuo, imefanya kinyume na athari za kiuchumi baada ya kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika ununuzi wa wachezaji ikitumia takriban Euro 250 milioni (sawa na Sh693.84 bilioni za Kitanzania) kusajili nyota wa Kijerumani, Kai Havertz na Timo Werner.


Hivi sasa imefika nusu fainali kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2014, ikiwania kutwaa kombe hilo kwa mara ya pili baada ya kufanikiwa mwaka 2012.


Chelsea na Real hazijawahi kukutana awali katika Ligi ya Mabingwa, kitu ambacho kinafanya mechi hizo mbili za nusu fainali kuwa za kuvutia. Lakini bado wale walio nyuma ya mpango wa kutengeneza muundo mpya wa Ligi ya Mabingwa, wanataka kubadili hilo.


Mwenyekiti wa Juventus, Andrea Agnelli, akizungumza kwa nafasi yake kama kiongozi wa Chama cha Klabu za Ulaya, alieleza nia yake ya kutaka klabu kubwa zikutane mara nyingi zaidi.

Vita ya Abu Dhabi na Qatar
Bila ya kujali, mabadiliko ambayo UEFA itayaidhinisha katika mkutano wake Jumatatu ijayo yapo zaidi katika hatua ya makundi, ikiongeza idadi ya klabu na kwa kiasi kikubwa ikianzisha muundo mpya.


Kuanzia hatua ya 16 bora, angalau michuano hiyo haitarajiwi kubadilika.


Kwa njia yoyote ile, kunatarajiwa kuwepo kwa mechi nyingi zaidi baadaye baina ya PSG na City, ambazo mara pekee kukutana katika Ligi ya mabingwa ilikuwa mwaka 2016 katika robo fainali.


Wakati huo, City ilishinda na kufika nusu fainali na kuwa mara pekee kufika hatua hiyo baada ya kununuliwa na Sheikh Mansour kutoka familia ya kifalme ya Abu Dhabi mwaka 2008.


Wakati City ikionekana kuelekea kutwaa ubingwa wa England kwa mara ya tatu katika misimu minne, PSG imesimama mbele yao barani Ulaya.


"Ni mara ya pili kufika nusu fainali, kwa hiyo si historia kwa klabu, lakini tunaanza kuijenga," Guardiola aliiambia BT Sport.

madrid 2


Baada ya kununuliwa na taasisi inayofadhiliwa na serikali ya Qatar Sports Investments mwaka 2011, PSG ilifika fainali ya kwanza msimu uliopita na imepania kufanya makubwa zaidi ikiwa na timu iliyojengwa kwa kutegemea wachezaji wawili ghali katika historia, Neymar na Kylian Mbappe.


"Sisi sasa ni timu kubwa, tukiheshimu timu nyingine," alisema rais wa PSG, Nasser al-Khelaifi wiki iliyopita, akijibu hoja kuwa wawili hao wanaweza kuondoka mwakani badala ya kuongeza mikataba yao.


Ni klabu moja kati ya hiso mbili itakayoenda fainali, lakini zitaendelea kurudi hatua hiyo, na hali inaweza kuwa ngumu tu kwa timu kama Real, kuzizuia.

Advertisement