Mafundi wa shoo hawa hapa!

Mafundi wa shoo hawa hapa!

Muktasari:

  • Kutakuwa  na dakika 90 za kibabe pale Uwanja wa Benjamin Mkapa jioni ya leo wakati Mabingwa wa Tanzania, Simba watakapokutana na watani wao Yanga kwenye pambano la Ngao ya Jamii.

Dar es Salaam. Kutakuwa  na dakika 90 za kibabe pale Uwanja wa Benjamin Mkapa jioni ya leo wakati Mabingwa wa Tanzania, Simba watakapokutana na watani wao Yanga kwenye pambano la Ngao ya Jamii.

Mchezo huu ni ishara ya kuanza kwa msimu mpya wa Ligi Kuu Bara 2021-2022, lakini utamu wa mchezo huo ni kwamba zinakwenda kukutana klabu mbili kongwe kitu cha kuongeza presha kila timu ikiwa imetoka kufanya usajili wa maana ambao wakilenga kutaka kupata mafanikio.

Hapa chini tunawaangalia wachezaji kutoka timu zote ambao watakuwa na burudani kila watakapogusa mpira, yaani wapaka rangi a.k.a mafundi wa mpira ambao mashabiki wana hamu ya kuona watapa ladha gani katika mchezo huo wa kibabe wa Kariakoo Derby.


Feisal Salum (Yanga)

Kiungo wa Yanga huyu ambaye siku za karibuni amekuwa katika kiwango bora sio tu ndani ya klabu yake bali hata anapokuwa katika majukumu ya kulitumikia taifa, Feisal kama ambavyo wengi humuita Fei Toto anajua kuuchezea mpira na hata kuupiga kwa madaha hatua ambayo huleta burudani.

Inaweza kutokea Yanga wako kimya, lakini Fei toto anaweza kufanya kitu ambacho kikarudisha nguvu ya mashabiki wao kushangilia lakini pia wenzake kuamka na kuanza kupambana.


Rally Bwalya (Simba)

Fundi mwingine akiwa katika kikosi cha Simba, wengi wanamuona ni kama injini mpya ndani ya kikosi cha Wekundu hasa baada ya kuondoka Clatous Chama na Luis Miquissone, Bwalya anayetumia mguu wa kushoto ana vitu vingi akiw ana mpira.

Ana uwezo wa kupiga pasi zenye kufika lakini pia akawatingisha wapinzani anavyotaka kutokana na kuwa na hali ya kujiamini kila anapokuwa na mpira.


Sadio Kanoute (Simba)

Kiungo mpya ndani ya Simba anacheza pale chini mbele ya mabeki, lakini uwepo wake hapo sio kitu, jamaa anajua sana kupiga pasi zenye machi na sio zile za kushoto na kulia zile za kwenda mbele.

Atakuwa silaha muhimu kwa Simba hasa wakati wa kuanzisha mashambulizi kama Yanga itakuwa na watu wavivu wa kukaba mbele, burudani itakuwa kubwa kutoka kwa huyu raia wa Mali.


Djuma Shaban (Yanga)

Huyu ni beki mpya wa Yanga akiwa na dakika zake 90 za kwanza akiwa na jezi ya timu hiyo katika mechi ya klabu ya nyumbani kuwa kwake beki kusikusumbue jamaa anajua kuamsha.

Makali ya Djuma ni kasi yake ya kupandisha mashambulizi sio rahisi kuchukua mpira miguuni kwake pia anajua kupunguza watu na kuwafinya anavyotaka huku akiingia ndani ya eneo la hatari, jamaa ni zaidi ya beki.


Duncan Nyoni (Simba)

Kiungo mpya ndani ya Simba ametua akitokea kwao Malawi anatumia sana mguu wa kushoto ana vitu flani hivi vya kuamsha visigino na pasi flani fupifupi tamu zinazofika.

Mbali na kujua kutoa pasi jamaa anajua kupiga mashuti kama ataondoa presha ataweza kufanya vitu vikubwa vitakavyopagawisha mashabiki.


Jesus Moloko (Yanga)

Winga mpya wa Yanga huyu aliyekuja kuziba nafasi ya Tuisila Kisinda, hana kasi kama ya Kisinda lakini ana vitu vyake akiwa na mpira na hasa akikutana na beki asiyejua kujiamini.

Ubora wake wa kukimbia na mpira lakini pia kuwapunguza mabeki ni kitu ambacho kinaweza kumsaidia akauteka umati wa mashabiki wa klabu yake Jumamosi. USIKOSE uchambuzi wa mechi ya watani kesho Jumapili hapahapa.