Majaliwa: Mkutano wa CAF utafungua njia kwa Tanzania

Majaliwa: Mkutano wa CAF utafungua njia kwa Tanzania

Waziri mkuu Kassim Majaliwa amesema mkutano mkuu wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), ambayo inafanyika leo Jumatano jijini Arusha itafungua fursa kwa Tanzania ya kuandaa mashindano makubwa.

Akifungua mkutano huo ambao unafanyika katika ukumbi wa mikutano ya Kimataifa ya Arusha AICC amesema anaamini mkutano huo utafungua njia kwa Tanzania kuwa mwenyeji wa mikutano mingine ya CAF pamoja na FIFA.

Amesema Tanzania kupitia TFF imekuwa na mahusiano mazuri na CAF pamoja na FIFA na imekuwa ni chachu ya kuhamasisha na kuimarisha maendeleo ya Mpira wa Miguu nchini na ukanda mzima wa Afrika mashariki.

"Ujenzi wa vituo viwili vya michezo nchini chini ya TFF kwenye miji ya Tanga na Dar Es Salaam ni kielelezo cha mahusiano mazuri na tunaishukuru sana FIFA kwa uwekezaji huo". amesema Majaliwa.

Ameongeza kuwa ni matarajio ya Tanzania kuwa FIFA itaendelea kubuni miradi mingi ya kuendeleza mchezo wa mpira wa miguu kwa nchi zinazoendelea kama Tanzania ambazo zimekuwa zikikabiliwa na changamoto ya ujenzi wa miundombinu ya mchezo.

Majaliwa amesema Tanzania kwa upande wake iko tayari kuendelea kuimarisha uhusiano wake na FIFA na wanachama wake CAF .

"Mashindano ya mpira wa miguu kwa Shule yani African schools football programme mliyoanzisha ni njia sahii ya uwekezaji wa muda mrefu na maendeleo ya mpira wa miguu barani Afrika". amesema Majaliwa.