Makocha wamzungumzia Sven

Sunday January 10 2021
sven pic
By Oliver Albert

Dar es Salaam. Simba ilitangaza kuachana na kocha wake Sven Ludwig Vandenbroeck baada ya maridhiano ya pande zote mbili huku wadau wa soka wakimpa tano kwa kuwa na misimamo na kutengeneza nidhamu kubwa kwa wachezaji wa timu hiyo.

Kocha huyo alitimka licha ya kuiongoza Simba kutinga kwa mara ya tatu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na pia aliipa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita, Kombe la Shirikisho (ASFC) na Ngao ya Jamii.

Lakini jana, picha zilisambaa katika mitandao mbalimbali ikimwonyesha kocha huyo akisaini mkataba wa miaka miwili kuinoa timu ya FAR Rabat ya Morocco.

Siku moja baada ya kuiwezesha Simba kutinga hatua ya makundi kwa kushinda mabao 4-0 dhidi ya FC Platinum ya Zimbabwe, kocha Sven alibeba mabegi yake mchana na kutimka kwao Ubelgiji.

Kocha huyo mwenye misimamo mikali aliondoka wakati kikosi chake kikiwa kinaelekea Zanzibar kwa ajili ya kushiriki mashindano ya Kombe la Mapinduzi.

Kabla ya kuondoka alikwenda kuwaaga wachezaji wa timu hiyo walio katika kambi ya Taifa Satrs na kuzungumza na mchezaji mmoja kwa niaba yao, pia alikwend a kuzungumza na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Mohammed Dewji ‘Mo’ na kumuaga.

Advertisement

Sven mwenye miaka 41 alitangazwa kuwa kocha wa Simba Desemba 11, 2019 na aliiongoza timu hiyo kwenye mechi 44 za Ligi Kuu Bara, akishinda 31 alitoka sare michezo nane na kupoteza mitano tu dhidi ya

Kocha mzoefu, Mrage Kabange alisema kuondoka kwa Sven kutaipa wakati mgumu Simba wakati huu wakiwa katika mashindano ya kimataifa huku akimpa tano kocha huyo kwa kusimamia suala la nidhamu kwa wachezaji wake.

“Ujue mnapokuwa katika mashindao halafu ghafla kocha anaondoka au mnamuondoa lazima mtayumba kwa kiasi fulani kwa sababu ni lazima atakuja kocha mpya ambaye nae atakuja na mifumo yake hivyo hadi wachezaji kuzoea inachukua muda kidogo.

“Sven ni bonge la kocha tofauti na watu walivyodhani na ubaya wa Tanzania kila mtu kocha. Nilipenda jinsi alivyokua na msimamo, hayumbishwi anachomini yeye ndiyo hicho hicho, ndiyo maana hata watu walipokuwa wanapiga kelele kwa nini anatumia mshambuliaji mmoja yeye alijifanya kama hawasikii na kuendelea na mfumo wake. Pia aliwafanya wachezaji wa Simba kuwa na nidhamu,” alisema.

Beki wa zamani wa Yanga na timu ya Taifa, Bakari Malima’ Jemba Ulaya’ alisema Sven alifanikiwa kuibadilisha Simba kwa kiasa kikubwa na kuleta nidhamu kwa wachezaji wake.

“Sijui kwa nini imekuwa hivyo, kwani si kitu kizuri timu kubadili badili makocha mara kwa mara. Kuondoka kwa Sven inaweza kuwaathiri kwenye ligi ya ndani na hata mashindano ya kimataifa kwani hadi kocha mpya aje na azoee itachukua muda,” alisema Jembe Ulaya.

Advertisement