Mamelodi na Yanga, namba zinaongea

Muktasari:

Hii ni michuano mikubwa barani Afrika huku kila timu ikiwa na nafasi ya kufanya vizuri kutokana na matokeo ya michezo ya kwanza ambapo mchezo mmoja tu ndiyo ulishuhudia bao likifungwa.

Michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya robo fainali, itatamatika wikiendi hii wakati timu nane zitakapokuwa uwanjani, kuwania nafasi nne za kwenda nusu fainali.

Hii ni michuano mikubwa barani Afrika huku kila timu ikiwa na nafasi ya kufanya vizuri kutokana na matokeo ya michezo ya kwanza ambapo mchezo mmoja tu ndiyo ulishuhudia bao likifungwa.

Mechi iliyopigwa jijini Dar es Salaam kati ya Simba na Al Ahly ndiyo pekee ilikuwa na bao, baada ya Wekundu wa Msimbazi kulala kwa bao 1-0, lakini mechi nyingine zote ikiwemo Yanga na Mamelodi, TP Mazembe na Petro, Es Tunis walipovaana na Asec Mimosas zote zilimalizika kwa suluhu.

Michezo yote wikiendi hii ni muhimu, lakini mashabiki wamekuwa wakisubiri kwa hamu kubwa vita  kati ya Yanga na Mamelodi, baada ya mchezo wa kwanza kuonyesha kuwa kila timu ina nafasi ya kufanya makubwa kwenye mechi ya pili.

Yanga iliondoka jana ikiwa na baadhi ya wachezaji wake ambao walikuwa wakisumbuliwa na majeraha, Pacome Zouazoa, Khalid Aucho na Yao Kouassi Atohola huku kocha wao Miguel Gamondi akisema lolote linaweza kutokea ugenini.

Kwenye takwimu za timu hizo pamoja na wachezaji mmoja mmoja zinaonyesha kuwa kila timu ipo tayari kwa ajili ya mchezo huo na hakuna anayeweza kumbeza mwenzake kwa kuwa kuanzia kwenye hatua ya makundi, namba zinaonyesha kuwa lolote linaweza kutokea.

Kuna vipengele ambavyo Yanga wanaonyesha kuongoza, lakini vingine Mamelodi wanatawala na katika takwimu hizo kuanzia hatua ya makundi na mechi za kwanza za robo timu hizo ndiyo zinaongoza kwenye maeneo mengi.

Bao kwa mchezo:
Kipengelea hiki kinaonyesha kuwa Yanga ipo juu ya Mamelodi ikiwa na wastani wa bao 1.3 kwenye mchezo mmoja, Mamelodi ipo nafasi ya sita ikiwa na wastani wa bao 1.0 kwa mchezo. Hivyo Yanga inaonekana kuwa na nafasi ya kufunga zaidi kuliko Mamelodi.

Kwenye hatua ya makundi, Yanga ilikuwa bora kuliko Wasauzi hao baada ya kufunga mabao tisa, huku Mamelodi ikiishia kwenye mabao sita.

Staa wa Yanga Yanga Pacome Zouazoa amehusika kwenye mabao manne akifunga moja na kutoa pasi moja ya bao, yupo nafasi ya pili nyuma ya kinara Sankara Karamoko ambaye kwa sasa hayupo kwenye michuano hiyo.

Anayefuata hapa ni Saidi Ntibazonkiza wa Simba ambaye ametoa pasi mbili na kufunga mabao mawili mchezaji wa Mamelodi aliyepo hapa ni anaingia Lucas Ribeiro na Marcelo Allende ambao wanashika nafasi ya 18 na 19 wakiwa wamehusika kwenye mabao mawili.

Umiliki wa mpira:

Kumbuka mchezo kati ya Yanga na Mamelodi, bado Wasauzi hao walikuwa juu ndiyo uhalisia kwa kuwa hadi kwenye chati ya jumla ya timu zote zilizopo hatua ya robo timu hiyo inaongoza kwa kumiliki mpira ikiwa na wastani wa 65.8 kwa mchezo mmoja.

Timu inayofuata ni Petro ambayo ina wastani wa 57.1 na Esperance 56.4. huku Yanga ikiwa nafasi ya nane na wastani wa 48.6.

Mashuti kwenye mechi:
Yanga pamoja na kwamba haimiliki sana mpira, lakini inaongoza kwenye wastani wa mashuti kwenye mchezo mmoja, ikiwa ndiyo bora kuliko timu nyingine zote nane ikiwemo Mamelodi Sundowns.

Kwenye eneo hili ambalo pia wikiendi Yanga ilifanya vizuri, ina wastani wa jumla wa kupiga mashuti 5.0 kwa mchezo mmoja ikifuatiwa na Mamelodi ambao wastani wao wa mashuti ni 4.7 sawa na Simba,  timu ya tatu ni Ahly yenye 4.3.

Kwenye yale yaliyolenga lango Joseph Guede wa Yanga anashika nafasi ya tano  hapa akiwa na wastani wa 1.4 anafuata Clement Mzize 1.3, Pacome Zouazoa 1.2, mchezaji wa Mamelodi anaibukia nafasi ya 30, Aubrey Modiba ambaye ana 0.8.

Uhalisia wa hapa unaonyesha kuwa Yanga ina uwezo mzuri wa mipira ya kushtukiza ambayo imewafanya wawe na mashuti mengi kuliko timu ambazo zinamiliki sana.

Nafasi nyingi za kufunga:
Hili ni eneo ambalo Yanga wanatakiwa kulifanyia kazi kidogo kwenye mchezo ujao, vijana hao wa Jangwani ndiyo wanaongoza kwa kupoteza nafasi nyingi za kufunga kuliko wapinzani wao Mamelodi.

Kinara hapa ni Al Ahly ambayo imepoteza nafasi 20, ikifuatiwa na Simba nafasi 18, lakini Yanga ipo juu ya Mamelodi ikiwa nafasi ya sita baada ya kupoteza nafasi 12 za kufunga mabao, huku wapinzani wao wakiwa wamepoteza nafasi 11.

Ili kuona kuwa Yanga imekuwa ikitengeneza nafasi hapa wachezaji wake wawili ndiyo wanaogoza kwa kutengeneza nafasi nyingi kwa ujumla Pacome Zouzoua, ameshatengeneza nafasi 17, sawa na Aziz Ki, huku mchezaji wa Mamelodi aliyepo hapa ni Marcelo Allende ambaye ametengeneza nafasi 16. 

Hivyo wachezaji wa Yanga wanatakiwa kuwa na utulivu kama wanataka kupata ushindi kwenye mchezo ujao Afrika Kusini.

Pasi zinazofika kwa walengwa
Kipengele hiki ni eneo lingine ambalo Mamelodi inaongoza ikiwa na wastani wa pasi 493.6, ikiwa inafuatiwa na Esperance de Tunis yenye 398.9 timu inayofuata hapa na Al Ahly ambayo ina wastani wa pasi zinazofika 398, huku Yanga ikiwa nafasi ya sita ikiwa na wastani wa pasi 348.1.

Kwa upande wa Simba yenyewe inashika nafasi ya mwisho kwa timu zilizotinga nane bora ikiwa na wastani wa pasi 318, ni eneo ambalo limekuwa gumu kwa timu nyingi ndiyo maana kuna gepu kubwa kati ya timu moja na nyingine.

Lakini kuonyesha kuwa Mamelodi kwenye eneo hili ipo vizuri, tano bora ya wachezaji waliopiga pasi nyingi zilizofika inashikwa na wachezaji wake watatu.
Teboho Mokoena ndiye kinara wa jumla akiwa na wastani wa pasi 76.3, nafasi ya pili inashikwa na Gomolemo Grant Kekana mwenye 70.2 kwenye mchezo mmoja.

Marcelo Allende anashika nafasi ya tano akiwa na wastani wa 61.0, huku mchezaji mmoja wa Yanga anayeibuka hapa ni Pacome Zouazoa ambaye anashika nafasi ya 33 akiwa na wastani wa 43.5.

Kama Yanga itataka kuuchezea sana mpira kwenye mchezo wa pili, basi hili ni eneo ambalo inatakiwa kulifanyia kazi kubwa kwenye uwanja wa mazoezi.