Mamelodi yaishusha Simba kileleni

MIAMBA ya soka la Afrika Kusini, Mamelodi Sundowns imeishusha Simba kwenye kilele cha 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya jioni ya leo Jumapili kupata ushindi mnono wa mabao 5-1 dhidi ya CR Belouizdad ya Algeria kwenye mechi iliyopigwa jijini Dar es Salaam.
Simba ilikuwa ikiongozwa orodha hiyo kwa kukusanya alama sita kutokana na mechi zao mbili, lakini ushindi wa Mamelodi umeifanya iwaengue kileleni kwa tofauti na mabao ya kufungwa na kufungwa.


Ushindi wa mechi ya leo iliyoletwa Tanzania baada ya wenyeji Belouizdad kuhamishia hapo kutokana na kwao kuwa na changamoto na covid 19, imeifanya Mamelodi kufikisha mabao saba ya kufunga na kufungwa moja, huku Simba ikiwa na mabao mawili tu, japo kila moja ina pointi sita.
Katika mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, wenyeji walijikuta wakicheza pungufu kwa dakika 87 baada ya mchezaji wao, Chouaib Keddad kulimwa kadi nyekundu mapema na Mamelodi kupewa penalti iliyowekwa kimiani na Themba Zwane.
Mabao mengine yaliwekwa kimiani na Peter Shalulile, Zwane aliyeongeza jingine, Lebohang Kgosana Maboe  na Kermit Erasmus. bao la kufutia machozi la Waalgeria lilifungwa na Amir Sayoud dakika ya 44 ya mchezo huo ambao haukuhudhuriwa na mashabiki wala kurushwa hewani.
Hata hivyo Simba ina nafasi ya kurejea kwenye kiti chake katika 16 Bora kama itaibuka na ushindi Ijumaa ijayo watakapoifuata Al Merreikh ya Sudan katika mechi yao ya Kundi A.

MSIMAMO 16 BORA
        P  PTS
1. Mamelodi         2   6
2. Simba            2   6
3. AC Horoya      2   4
4. Esperance    2   4
5. AS Vita          2   3
6. Al Ahly          2   3
7.Wydad            1   3
8.MC Alger         2   2
9.TP Mazembe       2   2
10.Zamalek         2   2
11.Kaizers         1   1
12.Teungueth       2   1
13.Al Hilal        2   1
14.Belouizdad      2   1
15.Petro Luanda        2   0
16.El Merreikh     2   0

Imeandikwa na ELIYA SOLOMON