Manara aomba radhi tena

ALIYEKUWA Msemaji wa Klabu ya Yanga, Haji Manara amemuomba radhi Waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo, Mohammed Mchengerwa kutokana na kauli yake ya kwamba Waziri huyo alitoa maelekezo kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kumpa adhabu kubwa kutokana na makosa ya utovu wa nidhamu.

Manara amesema baada ya kufuatilia amegundua kwamba Waziri hakutoa maelekezo hayo kwa TFF bali ameweka viwango vya viongozi na wadau wa michezo kuheshimu mamlaka zinazosimamia michezo nchini ili kuwa na tija katika uendeshaji.

"Nadhani kulikuwa na kutoelewana na ilikuchukuliwa hivyo na baadhi ya vyombo vya habari na mitandao kuandika kwamba; " Waziri amshukia Manara" lakini na mimi niliingia kichwakichwa kwa kuwa ilikuwa wiki ileile na hata katika press conference (mkutano na wana habari) yangu na ile ya wazee wa Yanga na baadhi ya viongozi wetu wa matawi ziliingia kichwakichwa kama nilivyoingia mimi,"

"Sababu jambo lilitokea wiki ileile na wiki ileile na kukawa na presha ya vyombo vya habari, mimi katika maelekezo yangu nikajikosea na nikaikosea Serikali na Waziri kwa sababu nilisema waziri ametoa maelekezo kwa TFF,"

"Baadae nilipofuatilia nikazungumza na maofisa wa Wizara wakaniambia hapana, hiyo ni Standard (viwango) ambayo Waziri ameiweka ya kwamba lazima viongozi wa michezo waheshimu mamlaka zinazoisimamia, kwani amekuwa akizungumzia suala la maadili kwa viongozi wa taasisi,"

"Nikagundua nia ya Waziri hakulenga kujikita kwenye jambo langu bali ilikuwa ni standard (viwango) ambayo ameviweka na ni jambo jema ambalo amelifanya waziri,"

"Inawezekana baadhi ya watu Serikalini, Baraza, Wizara na hata waziri mwenyewe, yawezekana hawakuelewa tafsiri ya lugha yangu niliyoisema, basi kwa utashi wa kimaadili lazima useme samahani kama kuna mmoja yoyote nimemkosea niseme Samahani." amesema

Hii ni mara ya pili kwa Manara kuomba radhi baada ya awali kumwomba Rais wa TFF, Wallace Karia kutokana na kile kilichoelezwa kumtolea maneno machafu wakati wa mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikosho la Azam (ASFC) dhidi ya Yanga uliopigwa Julai 2, Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

Hata hivyo licha ya kuomba msamaha huo ila Kamati ya Maadili ya TFF baada ya kujiridhisha kwamba alifanya makosa hayo ilimfungia miaka miwili kutojihusisha na masuala ya soka ndani, nje ya nchi na faini ya sh20 milioni.