Manula kufuru Simba, alamba Sh300 milioni

Thursday June 23 2022
manulaapiic
By Charles Abel
By Leonard Musikula

MABOSI wa Simba wameona isiwe tabu baada ya kipa wao Aishi Manula kuwaambia kwamba wakitaka abaki kwenye kikosi, basi wampe mkataba wa miaka mitatu wenye thamani ya Sh300 milioni.

Mabosi hao wamekubaliana na Manula kwa kumpa mkataba wenye thamani hiyo huku ndani yake kila msimu ukiwa na makubaliano ya nyongeza ya mshahara.

Manula alikuwa anatajwa pia kuwaniwa na matajiri wa Ligi Kuu Bara, Azam FC ambao walikuwa tayari kumpa donge nono na tayari walimpa kishika uchumba, lakini baada ya makubaliano na Simba kipa huyo aliamua kubaki zake Msimbazi.

Mwanaspoti limejiridhisha na usajili wa kipa huyo baada ya kufanyika vikao vingi vya kuvutana na mabosi wake kwenye maslahi pamoja na timu nyingine ndani na nje ya nchi kuonyesha nia ya kumhitaji.

Hivyo basi, Manula atakuwa mali ya Simba hadi mwishoni mwa msimu wa 2024-2025 na kwa maana hiyo ndoto ya timu zilizokuwa zikimtaka kufa rasmi.

Mkataba wa Manula kwenye mwaka wa kwanza atakuwa akivuta mshahara wa Sh8 milioni, ule wa pili atachukua Sh9 milioni wakati msimu wa mwisho atavuta Sh10 milioni kwa kila mwezi - mwanja ambao haufikiwi na mchezaji yeyote mzawa ndani ya timu hiyo.

Advertisement

Chanzo cha ndani kutoka Simba kililiambia Mwanspoti: “Tumeshamalizana na Manula. Ni kipa bora mzawa ambaye hakuna timu katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati isiyopenda kuwa naye kikosini. Amekuwa na mchango mkubwa kikosini na angeondoka lingekuwa pigo kubwa kwetu.

“Ndoto za Manula ni kuwa na mwendelezo wa kucheza katika hatua za juu za mashindano ya klabu Afrika ili thamani yake iendelee kukua hivyo anaamini kuwa bado Simba ndio sehemu sahihi ingawa pia atavuna kiasi kikubwa cha fedha katika mkataba wake huu mpya.”

Naye meneja wa Manula, Jemedari Said alisema: “Tumefanya mazungumzo na Simba ambayo yamekuwa na mwelekeo mzuri kwa kila upande. Ipo timu ya Afrika Kusini ya Martzburg ambayo iliulizia uwezekano wa kumsajili Aishi, lakini tukashindwana katika mahitaji yetu upande wa mchezaji.

“Manula ni miongoni mwa makipa bora 10 wanaocheza ndani ya Bara Afrika kwa sasa, hivyo anaweza kucheza katika timu yoyote tu lazima apate mahali ambako patamfanya alinde hadhi na ubora wake. Lakini kingine mchezaji anapoenda nje ya nchi kwa mfano Afrika Kusini maisha ya huko ni tofauti na ya hapa, hivyo angalau kwenye suala la maslahi anapaswa apate kikubwa na sio kiwe sawa au kidogo zaidi ya kile anacholipwa hapa.”

Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally aliliambia Mwanaspoti: “Mazungumzo baina yetu klabu na kipa wa nchi, Manula yameanza na hakuna chochote kitakachoharibika. Wote tunafahamu ubora wa Manula, hivyo sisi Simba hatuwezi kuruhusu kirahisi aondoke.”

Katika miaka mitano ambayo Manula ameitumikia Simba tangu alipojiunga nayo mwaka 2017, ametoa mchango wake kuiwezesha kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu mara nne, kutwaa mataji mawili ya ASFCS, kutinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mara mbili tofauti na kufika hatua kama hiyo kwenye Kombe la Shirikisho Afrika ikiwemo pia kutwaa tuzo ya kipa bora wa Ligi mara mbili tangu na kuchaguliwa katika kikosi bora cha msimu mara mbili tofauti.

Nyota mwingine aliyeongeza mkataba ni kiungo mkabaji, Mzamiru Yassin na atasalia kwa misimu mingine miwili mbele ndani ya Simba.

Mzamiru ameongeza mkataba wenye thamani ya Sh120 milioni na amepandishiwa mshahara na sasa ataanza kuchukua Sh7 milioni kila mwisho wa mwezi.

Kabla ya kukubali kuongeza mkataba mpya, Mzamiru alikuwa na ofa mbili za maana mkononi mwake ya kwanza ni Yanga na walimuwekea Sh120 milioni mkataba wa miaka miwili, ila ameshindwa kukubaliana nao baada ya kupewa pesa hiyo na mabosi wake.

Ofa ya pili ilikuwa ni Singida Big Stars waliokuwa tayari kumpatia Sh130 milioni kwa mkataba wa miaka miwili na inaelezwa walizungumza naye akiwa kwenye kambi Taifa Stars wakati wanajiandaa kucheza na Niger ugenini.

Inaelezwa mabosi wa Simba baada ya kumalizana na Manula, Mzamiru nguvu wanazielekeza kwa nyota wengine muhimu waliopanga kubaki nao ambao mikataba yao inamalizika mwisho wa msimu huu akiwemo beki wa kati, Mkenya Joash Onyango.

Mabosi wa Simba wamepata nguvu ya kuwapa mikataba mipya nyota wao na kusajili wachezaji wengine kutokana na mkwanja mrefu waliopewa na mdhamini wao, Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’ wiki moja iliyopita ili kuhakikisha makali ya timu yanarejea.

Ally alisema mazungumzo ya kuongeza mkataba na Manula yameanza na kabla ya wiki hii kumalizika kila kitu kitakuwa kimekwenda izuri. “Wachezaji wengine wanaomaliza mikataba tunaowahitaji kabla ya wiki hii kuisha yaani timu haijakwenda Mbeya tutakuwa tumemalizana nao ila kuna wengine tutawapa mkono wa kwaheri,” alisema Ally.

Mwanaspoti lilikuwa la kwanza kukujuza Simba kumalizana na Moses Phiri na wengine wapya watatu ambao hawajatangazwa ambao ni Nassoro Kapamba na Victor Akpan

Advertisement