Maradona atoka hospitali

Muktasari:

Picha hii iliyotolewa na ofisa habari wa Diego Armando Maradona inamuonyesha nyota huyo wa soka wa Argentina (kulia) akiwa ameshikana mkono na daktari wake, Leopoldo Luque mjini Olivos, Buenos Aires province, Argentina, jana Novemba 11, 2020.  AFP

Olivos, Argentina. Gwiji wa soka wa Argentina, Diego Maradona jana Jumatano (Novemba 11) alitoka hospitali akifuatwa na rundo la mashabiki baada ya kufanyiwa upasuaji wa kuondoa damu iliyovia katika ubongo.
Maradona hakuzungumza na waandishi waliojazana nje pamoja na mashabiki waliokuwa wakipiga kelele huku wamevalia barakoa, wakati akitoka Hospitali ya Olivos jijini Buenos Aires akiwa katika gari la wagonjwa, muda mfupi baada ya daktari wake, Leopoldo Luque kuwaambia waandishi kuwa angeweza kurejea nyumbani.
Walinzi binafsi walibeba mabango kwa ajili ya kuzuia gari hilo la wagonjwa lisionekane.
Kundi la mashabiki wa Maradona lililifuata gari hilo baada ya wengi wao kusubiri nje ya kliniki hiyo kwa siku kadhaa, wakiwa wameshikilia picha za nyota huyo wa zamani na wengine kuimba.
Moja ya mabango liliandika "asante ya milel"e.
Awali Luque alituma picha katika akaunti yake ya Instagram akiwa amemkumbatia gwiji huyo mwenye miaka 60, aliyekuwa ana bandeji kichwani.
Maradona anatarajiwa kuendelea na tiba mjini Tigre, kilomita 30 kaskazini mwa Buenos Aires, karibu na nyumba ya binti yake, Giannina.
"Diego amepitia, pengine, kipindi kigumu kuliko vyote katika maisha yake," alisema mwanasheria wake, Matias Morla mapema juzi, akiongeza kuwa "ni miujiza" kwamba damu hiyo katika ubongo ambayo ingeweza kugharimu maisha yake, iligundulika.
"Kinachotakiwa sasa ni mshikamano wa familia na kuwa karibu na maofisa wa afya," alisema Morla. "Kwa kuwa na madaktari na familia yake karibu, Diego atakuwa kama anavyotakiwa kuwa; na furaha."
Nyota huyo aliyeiwezesha Argentina kutwaa Kombe la Dunia alifanyiwa upasuaji Jumanne iliyopita kwa ajili ya kuondoa damu katika ubongo na mifupa ya kichwani.
Alionekana kutokuwa katika hali nzuri wakati alipoonekana kwa muda mfupi Oktoba 30 katika hafla ya sikukuu yake ya kufikisha miaka 60 iliyofanyika Uwanja wa Gimnasia y Esgrima, unaotumiwa na klabu ya Ligi Kuu ambayo anaifundisha.
Alionekana kutembea kwa shida na hakubakia kuangalia mechi ya timu yake.
Siku iliyofuata alipelekwa hospitali ya La Plata, akionekana na dalili za anemia na kuishiwa maji.
Uchunguzi ulibainisha kuwepo kwa damu katika ubongo, na baadaye Maradona akahamishiwa katika hospitali ya madaktari bingwa jijini Buenos Aires.