Marangach aliyedaiwa kumchoma moto Cheptegei kwa petroli naye afariki dunia

Muktasari:
- Marangach aliyekuwa mpenzi wa Cheptegei amefariki dunia wakati akipatiwa matibabu
Kenya. Aliyekuwa mpenzi wa mwanariadha wa Olimpiki wa Uganda Rebecca Cheptegei, Dickson Marangach amefariki dunia jana jumatatu.
Marangach amefariki akiwa Chumba cha Wagonjwa Mahututi (ICU) Hospitali ya Rufaa ya Moi, wakati akipatiwa matibabu ya moto wa petroli alioungua huku mwili wake ukiwa na majeraha ya zaidi asilimia 30.
Taarifa kutoka Shirika la Utangazaji la BBC, zinasema alikuwa katika hospitali hiyo ambayo marehemu Cheptegei pia alitibiwa kabla hajafariki dunia.
Katika tukio hilo, Cheptegei alifariki dunia Septemba 5, 2024 wakati akipatiwa matibabu ya majeraha aliyoyapata baada ya kumwagiwa petroli kisha kuchomwa moto na mpenzi wake huyo.
Kwa mujibu wa Nation ya Kenya, umauti ulimkuta katika Hospitali ya Rufaa ya Moi huko Eldoret, Kaunti ya Uasin Gishu nchini Kenya ikiwa ni siku mbili tangu kuchomwa moto na Marangach huku sababu ikitajwa ugomvi uliosababishwa na mgogoro wa kiwanja pamoja na nyumba.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Dk Owen Menach amesema Cheptegei, aliyelazwa ICU, alifariki dunia saa 11 alfajiri.